Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni
Sefue akongea wakati wa mkutano na wanahabari Ikulu jijini Dar es salaam
leo kuhusu sekta ya Gesi asilia nchini. Nyuma yake mwenye laptop ni Meneja wa
Sekta Kupunguza Umaskini na Kusimamia Maendeleo ukanda wa Afrika wa Benki ya
Dunia Dkt Albert Zeufack, akiwa ameongozana na mabalozi wa nchi kadhaa
pamoja na Timu ya wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo na
inayowakilisha Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la
Fedha la Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China, Uingereza
na Ujerumani
******
YALIYOSEMWA NA KATIBU MKUU KIONGOZI LEO WAKATI WA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
Katika miaka ya karibuni kumekuwepo kwa ugunduzi mkubwa wa gesi asili nchini
Tanzania katika maeneo ya mwambao na maeneo ya kina kirefu cha bahari ambapo
mpaka sasa jumla ya futi za ujazo trilioni 33 zimegunduliwa. Kazi ya utafutaji
inaendelea na upo uwezekano wa ugunduzi zaidi.
Kiasi hicho kilichothibitika hadi sasa hakitoshi kutuingiza kwenye ligi ya
wazalishaji gesi wakubwa duniani. Hata jirani zetu Msumbiji wanayo gesi asilia
iliyothibitika nyingi zaidi kuliko sisi.
Lakini kiasi cha gesi asilia kilichothibitika katika nchi yetu kinatosha
kutuwezesha kuwa wazalishaji muhimu wa gesi asilia, na tukijipanga vizuri na
kuisimamia kwa umakini sekta hii ndogo, inaweza kutusaidia kuharakisha
maendeleo.
Kinyume chake, tusipojipanga na kuisimamia vizuri tunaweza, kama nchi, tusipate
faida kubwa. Mbaya zaidi ipo mifano ya kutosha ya nchi ambazo uvumbuzi wa gesi
na mafuta umevuruga uchumi wao.
Hivyo, kabla hatujaenda mbali ni muhimu kama taifa tuwe na uhakika wa
tunachokitaka na tujijengee uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ikiwemo kwenye
kutunga sera, kuandaa mkakati na kutunga sheria itakayosimamia uendelezaji wa
sekta ndogo ya gesi.
Katika kufanya hivyo, hatuna sababu ya kuvumbua upya gurudumu. Duniani upo
uzoefu wa kutosha wa nchi ambazo hazikusimia vizuri sekta hii na kuharibiwa.
Ipo pia mifano na uzoefu wa kutosha wa waliosimamia vizuri na kufanikiwa.
Sisi tunaoanza leo tuna fursa ya kuepuka makosa waliyofanya wengine na tuna
fursa ya kuchukua uzoefu wa waliofanya vizuri. Lakini lazima tuchukue hatua
sasa. Tukichelewa itakuwa vigumu kurekebisha makosa baadaye.
Serikali imepania tusifanye makosa na
inaandaa utaratibu bora wa kusimamia uendelezaji wa sekta ndogo ya gesi asili.
Tunataka kuhakikisha kunakuwepo uwajibikaji, uwazi na uongozi bora ili Taifa
letu lipate mapato stahiki yatokanayo na uvunaji wa rasilimali hii, na mapato
hayo yatumike vizuri kama msingi wa kujenga uchumi endelevu wa kisasa,
utakaonufaisha wananchi wengi zaidi.
Mchakato wa kupata maoni ya wadau wote
ndani ya nchi unaendelea, lakini pia tunahitaji uzoefu na ushauri kutoka
kwingine duniani. Na ndio maana kwa karibu wiki moja sasa tumekuwa na ugeni wa
Timu ya wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo kutokana na maombi yetu.
Timu hiyo inawakilisha Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la
Fedha la Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China, Uingereza na
Ujerumani.
Tumekuwa na majadiliano kadhaa na Timu hii ambayo imekutana na wadau mbalimbali
ikiwemo Serikali, taasisi za umma, makampuni ya utafutaji wa mafuta na gesi,
sekta binafsi, asasi zisizo za kiserikali, wanazuoni, baadhi ya viongozi wa
vyama vya upinzani na wenyeviti wa Kamati za Bunge. Mikutano hii ililenga kuipa
Timu hii mawazo na maoni wa wadau muhimu ndani ya Tanzania ili wayazingatie
katika ushauri wao kwetu. Mazungumzo yote yalikwenda vizuri na yana manufaa
makubwa.
Napenda kusisitiza mambo yafuatayo:-
(i) Timu
hii tumeiomba sisi. Kama mnavyoona ina uwakilishi mpana wa Washirika wa
Maendeleo. Hivyo, badala ya kujadiliana na mmoja mmoja tumepata fursa ya
kuzungumza nao wote kwa pamoja.
(ii) Uamuzi
wa mwisho kuhusu sera, mkakati na sheria zitakazotawala sekta hii, ni wetu kwa
asilimia mia moja. Lakini katika kuamua tunataka tupate uzoefu wa wengine,
ushauri wa kitaalam na taarifa zote muhimu za kutuwezesha kufanya maamuzi
sahihi. Kwa mfano, tunachohitaji kutoka kwa Timu hii ni:-
(a) Uzoefu wa nchi ambazo
zimefanya vibaya katika kusimamia sekta zao za mafuta na gesi asilia. Lengo ni
kuhakikisha hatufanyi makosa waliyofanya wengine.
(b) Uzoefu wa nchi ambazo
zimefanya vizuri katika kusimamia sekta hii. Lengo ni kuzingatia yale yote
yaliyothibitika kwa wengine kuwa ni ya manufaa.
Mambo ya msingi kwa upande wa Serikali
ni kuhakikisha:-
(a) Tunakuwa
na mikataba bora inayolinda maslahi ya taifa lakini bila kukosa mvuto kwa
wawekezaji. Hivyo tunahitaji kujenga uwezo mkubwa kwenye eneo hili.
(b) Tunahimiza
wajasiriamali wetu wajiandae kutoa huduma kwa makampuni makubwa ya gesi ili
kupata manufaa zaidi kutokana na gesi.
(c) Tunaandaa
watalaam na mafundi wanaoweza kuajiriwa na makampuni ya gesi.
(d) Tuna
mfumo thabiti wa kusimamia matumizi ya mapato yakatakayotokana na gesi ili
yasiyumbishe uchumi mkuu wa nchi bali yawe msingi wa uwekezaji katika kubadili
mfumo wa uchumi wetu na maendeleo endelevu.
(e) Tuna
mfumo thabiti na uwezo wa usimamizi na udhibiti.
Pamoja na hayo ni muhimu wananchi
waelewe kuwa hatutakuwa matajiri mara moja. Hatutarajii mapato katika miaka
michache ijayo. Isitoshe lazima tufikirie vizazi vijavyo. Sisi tulio hai leo ni
wadhamini wa kile ambacho vizazi vijavyo vitarithi kutoka kwetu. Hivyo itabidi
tufikiri vya kutosha na kuamua kiasi gani cha mapato tutakayopata kitumike leo
na kiasi gani kitumike kujenga msingi wa maisha bora ya vizazi vijavyo hasa
ikizingatiwa kuwa kuna siku gesi hiyo itakwisha.
Nawashukuru washirika wa maendeleo waliotoa wajumbe kushiriki kwenye timu hii.
Pia nawashukuru wajumbe wenyewe kwa ushirikiano mzuri waliouonyesha wakati wa
zoezi hili.
Aidha nawashukuru watanzania walioshiriki na kutoa maoni yao hata kufanikisha
zoezi hili.
Kwa pamoja tuhakikishe Tanzania inakuwa mfano bora wa matumizi sahihi ya
rasilimali hii kwa faida na maendeleo yetu na vizazi vijavyo.
0 comments:
Post a Comment