Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara akipokea tuzo kutoka kwa Katibu Mkuu wa International Youth Fellowship Bw. Lee Hunmok jana wakati wa ufungaji wa kambi ya kimataifa ya vijana Jijini Dar es Salaam. Tuzo hiyo ilitolewa kwa Wizara kama ishara ya kutambua mchango wake katika kuhakikisha kuwa maendeleo ya vijana yanastawi kikamilifu.
Na Concilia Niyibitanga
Maendeleo ya vijana ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa letu, na ni muhimu vijana wakatambua hilo kwa kutimiza wajibu wao kwa jamii inayowazunguka.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akifunga kambi ya kimataifa ya vijana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyokaa kwa muda wa siku saba kwa lengo la kuzungumzia mstakabari wa maendeleo ya vijana hususan kuwajengea vijana fikra chanya kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Mukangara alisema kuwa vijana wanatakiwa kuwa na moyo wa kujituma, kujitolea na kufanya kazi kwa bidii ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya ujana.
‘Fanyeni kazi kwa bidii, kwa kujitolea, kwa kuzingatia muda na kujitegemea ili kutimiza ndoto zenu za kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kiafya’. Alisema Dkt. Mukangara
Aidha, amewaasa vijana kuachana na fikra za kulalamika, kudai haki bila wajibu na kunyosheana vidole na badala yake kijana mwenyewe ajiulize amefanya nini kutatua kero inayomzunguka.
Vijana kataeni vitendo vya uchochezi, chuki na kejeri kwa viongozi kwani kufanya hivyo kunaweza kuwaingiza katika misuguano isiyo na tija na mkumbuke kuwa maendeleo ya vijana hayawezi kushamiri na kustawi pasipo na amani, lindeni amani kwa nguvu zenu zote na kusimamia sheria wakati wote’ Alisema Dkt. Mukangara.
Alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa vijana na kupitia Wizara yake imeweka mipango ambayo inatoa vipaumbele kwa maendeleo ya vijana.
Naye Katibu Mkuu wa International Youth Fellowship (IYF), Bw.Lee Hunmok aliwataka vijana kuwatumikia wenzao na kuwa mabalozi kwa vijana ambao hawakupata fursa ya kuingia kambini.
Bw. Vitus Faustin Mzale ni kijana aliyeshiriki kambi hiyo kutoka mkoani Kagera alisema kuwa ameweza kujifunza mambo mbalimbali kambini hapo na amewataka waandaaji kushirikiana na Serikali ili kuwapa vijana mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Bi Mariza Vargas kijana kutoka Peru alisema kuwa amefungua moyo wake kwa ajili ya kujitolea na ameweza kujua namna ya kufanikisha malengo yake ya kujiletea maendeleo kama kijana.
Kambi hiyo ya kimataifa iliyoandaliwa na International Youth Fellowship ilishirikisha nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Korea, Malawi, Peru na China.
0 comments:
Post a Comment