Nafasi Ya Matangazo

June 20, 2012


Tukiamua kubishana,tunaweza kufanya hivyo. Lakini endapo mwisho wa ubishi huo tutaamua kukubaliana,basi sina shaka kwamba sote tutakubaliana kwamba; miongoni mwa mitandao inayotembelewa na yenye ushawishi mkubwa na wa aina yake miongoni mwa watanzania wengi,mtandao wa Jamii Forums au kwa kifupi JF hauwezi kukosa katika orodha hiyo.
Lakini tofauti na mitandao mingine ambayo kimsingi imekuwa ikiendeshwa na mtu au watu wachache tu, JF ni mtandao unaondeshwa na watu wengi.Wengi wakiwa watanzania wenyewe. Pengine hiki ndicho kinachoufanya mtandao wa Jamii Forums kuwa na “upekee” kama nilivyogusia hapo juu.
Uendeshwaji huu wa jumla unafanyika kwa uhuru wa kila mtu kujiunga na kuanzisha mjadala,kuchangia au kuupanua zaidi. Kimsingi,hivyo ndivyo mtandao wa Jamii Forums unavyochanja mbuga hivi leo. Wewe na mimi sote tunaweza kujiunga na kuendeleza mijadala. Ndani ya Jamii Forums kuna watu wa kila aina.Kuna watanzania.Kuna viongozi/wanasiasa,wanataaluma mbalimbali na pia kuna wenzangu na mie,watu wa kawaida wenye mapenzi na tekinolojia,habari,maarifa na wenye kutafuta mahali pa kutolea maoni yao huku wakiwa na imani kubwa kwamba kuna mtu atasoma ,kusikia na kuyafanyia kazi.
Ulianzaje? Nini malengo yake?Ni kweli kwamba mtandao huu unamilikiwa na chama fulani cha kisiasa? Mtandao huu una malengo gani?
Ili kupata majibu kwa maswali lukuki niliyokuwa nayo(na bila shaka uliyonayo wewe msomaji) nilimtafuta Maxence Melo Mubyazi(pichani), ambaye ni mwanzilishi-mwenza wa Jamii Forums na mtu ambaye mpaka hivi leo anabakia kuwa mhimili wa Jamii Forums ili kupata baadhi ya majibu kwa maswali yangu. Haya hapa ni mahojiano yangu naye;

BC: Kawaida mtu anapoanzisha kitu cha mtandaoni huwa ana malengo fulani ingawa inaweza ikatokea kwamba hapo baadae malengo yakabadilika au kujinyambulisha kidogo ili kwenda na wakati na hali halisi. Kwa upande wenu, mlikuwa na malengo gani kimsingi mlipoanzisha Jamii Forums? Je, bado malengo ni yale yale au yamebadilika?

MM: Malengo yetu tangu mwanzo ni yale yale na hayajabadilika na wala hatudhanii yatabadilika karibuni; kutoa uhuru wa kujieleza kwa njia mbadala. Ni wazi kuwa hili linaendelea japo linakuwa ndani ya sheria (http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/18042-jamiiforums-rules.html ) tulizojiwekea tangu mapema 2006.

BC: Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama wa Jamii Forums kwamba nyie Moderators wakati mwingine mmekuwa mkionyesha utashi binafsi. Mmewahi kulalamikiwa kwamba huwa mnatoa thread fulani kwa sababu zenu binafsi. Unasemaje kuhusu tuhuma kama hizi na labda unaweza kutusaidia kuelewa ni kitu au sababu gani zinaweza kusababisha “thread” fulani kuondolewa?

MM: Kama nilivyotangulia kusema tangu mwanzo; moderators wa JF wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria za uendeshaji JF; ufafanuzi juu ya thread (topic) gani huondolewa na kwa vigezo gani upo wazi http://www.jamiiforums.com/habari-na-hoja-mchanganyiko/69153-topic-gani-hufungwa-au-kufutwa-kabisa-jf.html na tuliutoa baada ya malalamiko ya wengi. Kila kitu kiko wazi, wengi wa wanaolalamika huwa hawapendi kuumiza vichwa, wale wanaowasiliana nasi huwa tunawapa ufafanuzi. Kuna kipindi tuliweka ‘automated notifications’ pindi thread inapohamishwa au kufutwa, tulichoambulia ilikuwa ni kazi bure, watu hawasomi hizo notifications!
Kila binadamu ana mapungufu, lakini hatuwezi kusema kuwa tutafanya kazi kwa hisia tu. Kuna moderation tools, moderator akifanya makosa yanaonekana kwa wote kuwa aliyefanya kosa ni moderator gani hivyo wote tunawajibika kurekebisha kosa la mmoja. Nyakati nyingine huwa tunalazimika kuomba radhi kutokana na makosa yanayoweza kutokea tokana na utendaji wa mmoja wetu.
Tuseme ukweli, uhuru bila mipaka wakati mwingine ni fujo. Huwezi kuruhusu mijadala ambayo inachochea umwagikaji damu, inachochea vurugu ama inajenga utengano miongoni mwa watanzania bila kufikiria athari za mbeleni kwa taifa letu.
Tunaijua hulka ya mwanadamu; wakati mwingine akishaweka kitu flani kichwani mwake basi kukibadili inakuwa kazi kubwa. Mtu anayeanzisha mjadala wa uchokonozi wa kidini ama kikabila ama kuanzisha mjadala ambao hana ushahidi ili mradi anataka kuchangamsha jamvi tu anakuwa anajua wazi anachofanya si kizuri lakini anafanya hivyo akiwa kajiandaa kuwashambulia viranja wa jukwaa (moderators).

BC: Bila shaka hili ntakalokuuliza na nyie wenyewe mmeshalisikia sana. Inasemekana kwamba Jamii Forums ni kama vile mkono wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) cha mtandaoni. Mnazungumziaje tuhuma kama hizi ?Ukweli uko wapi?

MM: Tuhuma hizi zilikuwepo kuelekea uchaguzi 2010; well, mara zote huwezi kukwepa tuhuma maana tuhuma ni tuhuma na anayetuhumu mara nyingine hana sababu za kutuhumu.
Ukweli ni kuwa hata hao CHADEMA wanatulalamikia kuwa tunatumiwa na CCM; lakini cha kujiuliza, ni kweli tuhuma hizi wanapozitoa wanakuwa na ushahidi wa wazi?
CCM:
Baada ya uchaguzi walitoa tuhuma zinazoelekeana na hili, tulitoa ufafanuzi (http://www.fikrapevu.com/habari/political-paranoia-tanzanias-ruling-party-in-fear-of-online-social-media) na kwa bahati walituelewa na kuongeza jeshi lao ndani ya JF.
Siamini kama Mwigulu, Nape, Dr. Kigwangalla, Hussein Bashe n.k ambao ni wanachama hai (achilia mbali Salva Rweyemamu, AG Werema n.k) ndani ya JF ni CHADEMA. Hawa ni wenye uthubutu toka CCM.
CHADEMA:
Kinachoipa CHADEMA credit kwenye social networks nyingi (si JF pekee) ni uharaka wa wao kujibu hoja wanapoona imelengwa kwao. Wengi wamejisajili kwa majina yao halisi na wanakuwa ‘active’ kwenye ‘hot issues’. Dr. Slaa, Zitto, Mnyika na Dr. Kitila Mkumbo ni baadhi watu toka CHADEMA ambao wako active JF. Lakini, kukubali kwao kukosolewa na kujibu pale wanapoweza ndiko kunakowafanya wengi wajikute wanakishabikia chama chao. Nina wasiwasi kuwa hata hao wanaowashabikia hawana kadi za CHADEMA.
Kifupi:
‘Trending’ ya siasa ndani ya Tanzania ndiyo inapelekea mijadala kuonekana kui-favor CHADEMA. Lakini ukiangalia kwa sasa hali inavyoelekea mwaka 2012 CHADEMA inaweza kupita kwenye wakati mgumu kuliko wakati wowote; hata hivyo ni endapo hawataweza kuling’amua hili na kulifanyia kazi. JF as JF haitozuia mjadala endapo ya CUF yatawakuta CHADEMA, ndo uhuru wa kujieleza huo, na kama kutakuwa na ‘facts’ basi huwezi kuzuia mjadala.

BC: Watu wengi ambao nimewahi kuongea nao kuhusu au kuiongelea Jamii Forums nikiwa nao,wamekuwa wakihoji kuhusu chanzo cha habari zenu. Ninavyojua mimi ni kwamba chanzo chenu kikubwa ni wanachama wenyewe (JF Members). Ninachotaka kuhoji mimi ni jinsi au utaratibu mnaoutumia katika kuhakiki authenticity au ukweli wa habari zinazochapwa au kutokea katika Jamii Forums. Mnafanyaje?

MM: Well,Maswali ya ‘Chanzo chenu cha habari’ huwa tunakumbana nayo sana. Lakini ni pale mtu anaposhindwa kuelewa JF ni nini. JF si gazeti, si redio na wala kituo cha televisheni. JF ni social network; moderators wapo kusimamia sheria za kujadiliana bila kuziathiri, pale inapokuja habari ambayo mwanzishaji tunamtilia walakini huwa tunajitahidi kuwasiliana na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo tuna ushirikiano nao na pengine kutuma waandishi wetu kuweza kutafiti ukweli wa habari husika. Mara nyingi zinakuwa si habari bali ni ‘news tips’.
Kwa kutambua hilo, tuliamua kuwa na kitengo maalumu kinacho-deal na habari ambapo habari zilizohaririwa toka kwetu zinapatikana www.FikraPevu.com hapa ukituuliza chanzo cha habari tutakupatia kila aina ya ushahidi na waandishi wetu wapo makini wanapofuatilia jambo flani.
Kuwazuia watu ati wanapoandika JF kwanza kila ‘comment’ au hoja mama (thread) ithibitishwe kabla ya kwenda hewani itakuwa ni ukiritimba ambao utapelekea mambo mengine kuwa magumu kufanyika. Wanachama wa JF wengi ni waungwana (japo si wote), wanatambua umuhimu wa jukwaa lao na wanahakikisha wanalilinda. Vifaa (tools) kwa ajili ya kuwasaidia moderators kujua kuwa kuna kitu hakipo sawa vimewekwa (Report Abuse) na wanachama wetu huvitumia kutujulisha pindi panapokuwa na kitu ambacho si cha kawaida ili kiweze kuwa ‘reviewed’ haraka kabla hakijasababisha madhara kwa Jamii yetu.

BC: Baadhi ya habari zinazoandikwa kwenye Jamii Forums (hususani zile za kimataifa) huonekana kama zimenyofolewa kutoka katika vyombo vya habari vya nchi za nje. Hii huwa na picha na maelezo wakati mwingine. Hamuoni kama kwa kufanya hivyo na hususani pale source ya habari hizo inapokuwa haijawekwa wazi ni ukiukwaji wa masuala ya hakimiliki? Mnakabiliana vipi na changamoto hizo?

MM: Kama nilivyoongea hapo awali; wanachama wa JF wapo makini; mtu anapoanzisha mjadala ambao unaonekana wazi si wake ameunyofoa sehemu basi humlazimisha aweke chanzo cha habari. Mara nyingi mataifa ya nje wako makini kwenye hili, wanapogundua unatumia habari zao bila ku-credit source (kuonyesha chanzo) basi hukupiga DMCA. Moderators wa JF wanajitahidi kufuatilia endapo mtu anaweka habari bila kuweka chanzo kuhakikisha inaonyeshwa wazi kuwa habari hii ina chanzo na chanzo chake ni kipi.
Hili hufanyika kwa vyanzo vyote; iwe ni online au offline (radio, magazeti au televisheni); mhusika LAZIMA awafahamishe wasomaji chanzo cha habari yake; kama ni hoja yake ni wachache watakaomhoji juu ya chanzo cha habari husika.
BC: Baadhi ya wanasiasa wenye majina makubwa nchini, aidha wakitumia majina yao halisi au wakitumia majina ya kujipandikizia, wamekuwa wakitumia mtandao wenu katika kujadili hoja mbalimbali na wengine hata kuelezea sera zao. Una ushauri gani?

MM: Mazingira ya nchi yetu ndiyo yanapelekea watu kutumia majina ya bandia. Wanaotumia majina yao halisi ni wengi kwa sasa, lakini kuna hoja inawawia vigumu kushiriki pale wanapohitaji kufanya hivyo.
JamiiForums ni mkusanyiko wa mijadala mbalimbali (zaidi ya siasa); ni vigumu kwa Zitto/Slaa/Kigwangalla kuingia Jukwaa la Mapenzi na kushiriki mjadala flani ambao huenda angetamani kushiriki. Kuna perception flani ilishajengeka juu yake, kwa mantiki hii anaweza kujikuta analazimika kutumia jina la kivuli kuweza kuwasilisha hoja na kutoa maoni yake kama mwananchi.
Mara zote tunawasisitiza watu ‘kuwa wao’ (to be genuine) na kuepuka kuandika uzushi, hii inasaidia watu kuweza kushiriki mijadala bila kuingiza chumvi sana au kuandika bila kufikiria (japo si wote). Watu wa propaganda huwezi kuwazuia, haswa wanapoingia Jukwaa la Siasa!
Kifupi; muhimu kwetu ni hoja ya mtu na si jina la mtu.
Bahati mbaya sana sheria za JF hazijui cheo cha mtu wala jina lake; anapovuka mipaka bila kujali yeye ni nani atafungiwa kwa muda na endapo ataendelea kukiuka sheria atafungiwa moja kwa moja!
Lakini, kwa kutambua kuwa wengine wanahitaji kushiriki mijadala isiyokaa kishabiki; ndani ya JF kuna Jukwaa maalum kwa wale wanaojadili hoja tu bila kuingiza vioja. Jukwaa hili tumeliita ‘Great Thinkers’. Jukwaa hili halina moderator, wanaojadili huko wanajadili ‘issues’ zaidi na tunajitahidi kabla ya kumpa mtu fursa ya kuwa mdau huko kuzipitia baadhi ya jumbe alizokwisha weka ndani ya JF, kama ni mwanasiasa mwenye jina na ndio kwanza kajisajili, tunawasiliana naye na akitaka msaada tupo tayari kumfuata kumwelekeza namna ya kutumia jukwaa hili. Kimsingi, ukilitembelea utathibitisha kuwa wanaojadili issues huko ni kweli ni ‘Great Thinkers’.

BC: Ni kiasi gani cha muda ambao mnautumia kwa siku katika kuhakikisha kwamba JF inakwenda katika mtiririko mnaoutaka. Hapa nazungumzia mambo kama kuhakikisha ipo hewani, ku-approve members wapya, kuhakiki kinachoandikwa au kuwekwa mtandaoni na mambo mengine kwa ujumla?
MM: Mpaka sasa tuna moderators 22, wapo maeneo tofauti ya Dunia na hivyo JF inakuwa monitored masaa 24. Labda niseme MIMI huwa natumia masaa takribani 18-20 kwa siku nikiwa online.

BC: Kumekuwa na changamoto kwamba vyombo vingi vya habari vya mtandaoni kama vile JF na hata hii bongocelebrity.com ni vyombo vya kimjini mjini…hususani Dar-es-salaam yaani tunawafikia zaidi watu waliopo mjini ambao kimsingi ndio wenye uelewa zaidi na uwezo wa kuingia mtandaoni kwa maana ya kuwa na access na mtandao. Mnaziongelea vipi changamoto hizi na mipango ikoje kuwafikia wengi na wengi zaidi?

MM: JF imeenda step kubwa zaidi, si ya ki-mjini mjini tena. Kama utakumbuka, mwanzoni (2006-2008) JF ilikuwa na wachangiaji wengi toka ng’ambo. Kwa kifupi asilimia kama 75 hivi ya waliokuwa wanatembelea JF (enzi hizo JamboForums.com) ilikuwa ni toka ng’ambo.
Maisha yamebadilika Tanzania, kwa leo hii zaidi ya 70% ya wanaotembelea JamiiForums ni toka Tanzania! JamiiForums kwa kutambua umuhimu wa kuwawezesha walio vijijini kuipata, tuliweka ‘mobile detection tools’ ili mtu anapoitembelea kwa simu ya mkononi (hata ya kichina) yenye uwezo wa kutumia mtandao aipate ndani ya sekunde 3. Kwa survey tuliyoifanya, watumiaji wa simu za mikononi kwenye mitandao wameongezeka na inaelekea kufikia 2014 asilimia hamsini (50%) ya watumiaji wa mtandao inaweza kuwa ni kutoka simu za mikononi.
Kuna changamoto, lakini hii haikwepeki kuwa ukuaji wa teknolojia utasaidia watanzania wa vijijini kuzipata tovuti nyingi toka simu za mikononi. Kumbuka, karibia 50% ya watanzania wana simu za mikononi (kwa mujibu wa TCRA).

BC: Kama moderator,mwanzilishi na mmiliki wa JF nina uhakika kwamba unaona na kusikia mengi ambayo yanaakisi kwa kiasi kikubwa, fikra za wananchi, maoni, mwelekeo na utashi wao kwa vyama vya kisiasa na siasa zenyewe. Kwa kutumia mwangaza huo huo, unadhani ni mambo gani matano ambayo yanawakera zaidi wananchi na ambayo ni rahisi tu kupatiwa ufumbuzi lakini kwa makusudi tu yanapewa nafasi ya nyuma?

MM: Well, mimi si mmiliki; ni mwanzilishi tu. Wamiliki ni watanzania wanaoitumia JF.
Kujibu swali lako kwa uzuri nitoe ufafanuzi (mfupi nikiwa limited kwa mambo matano tu) ifuatavyo:
  1. Watanzania wenye kuwa na uanachama wa vyama vya siasa ni wachache; vyama vinatakiwa kuelewa kuwa watanzania shida yao kubwa si siasa, maisha mazuri ndicho kilio chao. Maisha ya watanzania wengi ni duni, wanaishi bila kujua kesho itakuwaje! Pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho linazidi kuwa kubwa, ni hatari tunakoelekea.
  2. Miundombinu iboreshwe, ukitembelea vijiji vingi hawana hata maji walau ya visima na vyanzo vya maji vimeharibiwa (achilia mbali mijini); jitihada za serikali kwenye kuboresha barabara zinaonekana lakini haziendani na kasi ya ongezeko la idadi ya watanzania.
  3. Siasa za majitaka watanzania kwa sasa hawazioni za maana, bado zinatumiwa na vyama vyote na kwa mtizamo wangu zitavimaliza vyama vyenyewe! Kuna Tanzania zaidi ya vyama tunavyoviona sasa.
  4. Mfumo wa elimu uangaliwe upya; wanaohitimu serikali iangalie wapo wapi na wanafanya nini. Iweke namna ambayo kila chuo kitaweza ku-track wahitimu wake na kujua wafanyalo; tunakoelekea bomu la watanzania kukosa ajira litakuwa kubwa. Kuna baadhi ya wanasiasa wameanza ku-capitalize kwenye hili kuelekea uchaguzi 2015!
  5. Kuna umuhimu wa kuwa na wawekezaji lakini wengi wa wanaokuja Tanzania ni wakwapuaji. Wapinzani hata kama wamelipigia kelele hili bado hawajafanya vile walivyotarajiwa! Tanzania imekuwa shamba la bibi na kwa sasa wageni wanazidi kujazana na inaelekea ni wazi tunakoelekea hili litakuwa tatizo kubwa.
BC: Mbali na tovuti au blogs, watanzania wengi siku hizi wanatumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Twitter katika kupashana habari nk. Pamoja na hayo, wataalamu mbalimbali wa mawasiliano ya kimtandao wanasema Tanzania tupo nyuma katika kuitumia mitandao hiyo katika kupashana habari na kupeana ujuzi ambao/ambazo zinaweza kusaidia katika kuleta maendeleo au mabadiliko ya kijamii. Tunaambiwa sisi tumebakia “kupiga umbea” tu katika mitandao hiyo badala ya kuitumia kama ambavyo wenzetu wa nchi mbalimbali ulimwenguni wanavyoitumia. Nini maoni yako na ushauri katika hili?

MM: Kifupi: Ni vigumu njia inayotumiwa na Congo/Kenya kuwasiliana kufanya kazi Tanzania. Namaanisha kuwa, si kama mitandao ya FaceBook au Twitter ni mibaya kwa watanzania, tunachogundua kwa sasa ni kuwa wasomi wa Tanzania wengi ni waoga na wabinafsi; tusitarajie wale tunaowaona wakipongezana, wakisifiana Facebook na twitter siku moja waamue kuanza kukosoana kirahisi.
Isipokuwa twitter au facebook au JamiiForums vitakavyoleta mabadiliko muhimu, bado watanzania watakuja na namna mbadala; mitandao hii itatumika kupashana habari na huenda ikachukua hatamu baada ya wananchi ‘wa kawaida’ kuja na namna mbadala.
Tumetoka mbali, taratibu tutafika. Kusema watanzania ‘wanapiga umbea’ kwenye twitter ni kuwaonea, ikiwa ni facebook hapo naweza kukubaliana na wanachosema. Aidha, sidhani kama malengo ya mitandao hii ni kuleta ukombozi/mapinduzi bali upashanaji habari. Hili linaelekea kufanikiwa kwa Tanzania, tutaulizana miaka 5 ijayo juu ya kauli yangu hii.
BC: Kuna tofauti gani kubwa kati ya mtandao wa Jamii Forums na mitandao mingine mingi hapa nchini au hata nje ya nchi ambayo inaandika au kudurusu habari na matukio kutoka Tanzania?

MM: JF unaweza kuitofautisha na mitandao kulingana na mtandao unaoilinganisha nao. Tofauti sidhani kama ni kubwa bali kinachoitofautisha JF na kwingineko ni kuwa hoja/mijadala inakuwa monitored na kumfanya mwingine adhanie huenda ni chombo cha habari!
Zaidi, JF ni tovuti ya kwanza kwa Tanzania kuwa na mobile apps zake; tunazo apps kwa ajili ya watumiaji wa iPad/iPhone, BlackBerry na Android.
BC: Kama nilivyogusia huko juu, kupitia JF unaona, unasikia mengi nk. Una ushauri gani kwa vijana wa kitanzania ambao ndio watakaoshika dola miaka ijayo?
MM: Wasome!
Mtu anayejisomea vitabu vingi (si vya udaku tu) ana hazina kubwa kichwani. Kwa vijana ambao wanaitembelea JF, nashauri kwa umakini mkubwa wawe wasomaji zaidi, wajaribu kuuliza ili waeleweshwe juu ya jambo flani. JF inaweza kuwa hazina kubwa kwao endapo watafuatilia mijadala inayoendelea na iliyopita. Jukwaa la Great Thinkers ndani ya JF lina mijadala ambayo inamfanya mtu atumie bongo zake anapochangia (http://www.jamiiforums.com/great-thinkers/ )
Wajibidishe na washirikiane; kufanya mambo kivyakovyako ina gharama kubwa. Tukiungana ni rahisi kufanikiwa hata bila kuwezeshwa na serikali ama wahisani.
Wajiamini!
Vijana tunaweza, tusisubiri kuwezeshwa. Mtaji wa kwanza kwetu ni akili kichwani; pesa ni ziada tu!
BC: Asante sana Max kwa muda wako. Kila la kheri katika kazi zako
MM: Asante Jeff.Kazi njema na wewe pia.
Posted by MROKI On Wednesday, June 20, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo