Siku
ya Familia Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Mei na nchi
wanachama wa Umoja wa Mataifa. Maadhimisho hayo yanatokana na tamko la
Baraza la Umoja wa Mataifa Na. 47/257 la tarehe 20 Septemba, 1993,
linaloidhinisha kuwa na Siku maalum kwa ajili ya familia. Tanzania ni
moja ya wanachama wa Umoja wa Mataifa hivyo huungana na nchi nyingine
kila mwaka kuadhimisha siku hii. Mwaka huu maadhimisho haya yatafanyika
kimkoa.
Madhumuni
ya Siku ya Familia Duniani ni kuhamasisha, kuhimiza, kuelimisha na
kutanabahisha jamii kuhusu umuhimu wa familia katika jamii kwa nia ya
kuchukua hatua zinazopasa ili kuziimarisha na kuziendeleza.
Kauli
mbiu ya Siku ya Familia mwaka huu ni: “UWAJIBIKAJI SAWA KATIKA
MAJUKUMU: MSINGI WA FAMILIA BORA”. Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha,
kuhimiza, kuelimisha familia na jamii kugawa muda wa kazi za kiuchumi na
kuacha muda wa kutosha kutekeleza majukumu ya familia, hasa ya kulea na
kukaa na watoto/familia hivyo kujenga umoja, uadilifu na upendo kwa
familia. Ushindani uliopo katika soko huria ni changamoto kwa wazazi wa
kizazi cha sasa kutopata muda wa kutosha kuwa na familia.
Aidha,
majukumu yanaongezeka siku hadi siku ambayo husababisha wazazi/walezi
kufanya kazi siku zote za wiki na hata usiku, hatimaye kupunguza muda wa
kukaa na familia hasa watoto wao na hivyo kusababisha kutokuwepo kwa
uwiano wa kazi na majukumu ya malezi.
Pamoja
na kwamba tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kukidhi mahitaji ya
familia, inabidi kuwianisha muda wa kufanya kazi na kukaa na familia ili
watoto wapate malezi stahiki.
Familia
nyingi za Kitanzania zinakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja
na kuwepo kwa mila na desturi zenye kuleta madhara, umaskini
uliokithiri, mawasiliano na miundo mbinu mibovu ambapo husababisha hali
ya maisha ya watu kuwa duni na tegemezi na hatimaye kutumia muda mwingi
wa kufanya kazi bila ya kujali madhara yatakayotokea kwa familia.
Madhara haya ni pamoja na watoto kuwa na tabia mbaya kama kuacha shule,
kukimbilia mitaani, kutokuwa na maadili na kuiga tamaduni zisizokubalika
katika jamii yetu.
Ni
wazi kuwa changamoto hizi zinaweza kushughulikiwa vyema kuanzia ngazi
ya familia na ngazi mbalimbali za uongozi. Kwa kuwa maadhimisho ya mwaka
huu yatafanyika kimkoa, napenda kuwaasa watanzania wenzangu kutenga
muda wa kutosha kukaa na familia zao ili kujadili, kushauriana na
kutekeleza masuala muhimu ya kuendeleza familia zao; kwani familia ndiyo
kitovu cha maendeleo.
Aidha
viongozi katika ngazi mbalimbali wahamasishe na kuhimiza watumishi wote
kuona njia bora za kugawa muda wa kazi na muda wa kushughulikia familia
zao ili kujenga maadili na maendeleo ya familia. Natoa wito kwa
wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kuadhimisha siku hii kwa kuwa
kila mmoja wetu ana familia na ni sehemu ya familia ndani ya jamii.
Ni
matumaini yangu kwamba kupitia maadhimisho haya familia zitakumbushwa
wajibu na mchango wao katika maendeleo ya familia zao, jamii na Taifa
kwa ujumla .
Nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Familia Duniani.
Asanteni,
Anna T. Maembe
KAIMU KATIBU MKUU
0 comments:
Post a Comment