Nafasi Ya Matangazo

December 03, 2011



WAZIRI wa Maji, Profesa Mark Mwandosya ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali ya Apollo, nchini India, amesema hajawahi kulazwa hospitalini kwa muda wa miaka 34 akiwa katika utumishi wa umma.
Profesa Mwandosya, aliyasema hayo Jumamosi, tarehe 03.12. 2011 akiongea katika mkutano na Watendaji Wakuu, baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Maji pamoja na Waandishi wa habari kwa mara ya kwanza baada ya kurejea nchini akitokea India alikokuwa anatibiwa.
Katika mkutano huo, Profesa Mwandosya alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake kwani hali yake inaendelea vizuri. Aliongeza kuwa fimbo aliyonayo ataitumia kwa muda mfupi wakati viungo vyake vinatengemaa.
“Baada ya kutangaziwa tanzia nakiri kuwa anayezungumza ni mimi mwenyewe wala siyo mzimu wangu, nimerudi nyumbani salama baada ya kutibiwa kwa miezi mitano na nusu” Alisema, Profesa. Mwandosya.
Profesa Mwandosya alimshukuru Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilali, Rais wa Zanzibar Ali Mohammed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sherif Hammad, Spika wa Bunge Anna Makinda, Mawaziri wote, Wabunge wote na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahimu Lipumba, kwa kumjulia hali kwa njia ya simu pamoja na mtandao na wengine kumtembelea.
“Nimeona niitumie fursa hii kuwashukuru nyie wadau wa sekta ya maji kwa kuendelea kufanya kazi wakati mimi nilikuwa sipo. Sekta ya maji inaendelea vizuri,” alisisitiza.
Profesa Mwandosya aliongeza kuwa kitu kilimchompa nguvu ni upendo na ubinadamu alionyeshwa na Watanzania.
“Hili nakiri sikulitegemea nilidhani ningepata lawama kwa kutotimiza adhima ya huduma ya maji kwa baadhi ya wananchi, lakini ajabu nilioneshwa upendo, ubinadamu na mshikamano na wananchi wa kawaida kutoka mikoa mbalimbali kwa njia ya simu na mtandao. Hii ilinipa faraja” alisema huku akisisitiza tusipoteze upendo, ubinadamu na mshikamano huo.
Aliwashukuru waandishi wa habari kwa kuwajulisha wananchi jinsi alivyokuwa anaendelea akiwa nchini India, Viongozi wa dini kwa sala maalum za kumwombea na wananchi wote kwa kumjulia hali na kumwombea. Aidha, alitoa shukrani zake za pekee kwa wapiga kura wake wa jimbo la Rungwe Mashariki na kuwapongeza kwa kupata Halmashauri mpya ya Busokelo.
Profesa Mwandosya aliruhusiwa na Daktari wake kutoka katika Hospitali ya Apollo nchini India siku ya Jumatatu tarehe 28 Novemba, ambapo aliondoka nchini India Jumanne saa nne asubuhi tarehe 29 na aliwasili nchini siku ya Alhamisi Desemba Mosi , mwaka huu kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates.
Posted by MROKI On Saturday, December 03, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo