Nafasi Ya Matangazo

August 29, 2011

MBUNGE wa jimbo la Mvomero, mkoani Morogoro, Amos Makala ameingilia kati mgogoro wa ardhi uliopo katika Kitongoji cha Kinyenze , Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali , Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro baina ya wananchi na mwekezaji wa Kigeni aliyeuziwa shamba kijijini hapo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki Kijijini hapo Makala aliyeambatana na Ofisa Ardhi wa Wilaya hiyo, Majaliwa Jaffari amewataka idara ya ardhi kuchukua hatua za haraka na dharula kutatua mgogoro huo kabla ya kuibuka kwa machafuko ya uvunjifu wa amani.

“Nimejionea mwenyewe baada ya kusikia kiliochenu juu ya mwekezaji huyu, watu wa ardhi tafadhalini sana lishughulikieni suala hili haraka sana na mkae pamoja mgogoro huu umalizike upesi iwezekanavyo”, alisema Makala.

Aidha Makala amemwomba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero kutumia mamlaka waliyonayo kufika kijijini hapo wafungue uzio huo uliowekwa na mweklezaji huyo haraka ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali, watoto kwenda shule na watu kuvuna mazao yao yanayoibiwa na walinzi wa kampuni ya Tanbreed Poultry Limited ambayo imemega mashamba yao.

“Nivyema sasa Viongozi wa Mkoa na Wilaya kufika hapa wakiwa na dola na kukata uzio huu, ili wananchi muendelee na shughuli zenu za kijamii, si haki kufunga barabara mnayoitumia kwenda katika makazi yenu na mashambani”,alisema Mbunge Makala.

Makala pia aliwapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa moyo wa uvumilivu waliouonesha katika kipindi kirefu tangu kuibuka kwa mgogoro huo bila kupatiwa ufumbuzi kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu licha ya kuandikiwa barua tangu mwezi Aprili mwaka huu mgogoro huo ulipoanza kushika kasi.

“Wananchi mmefanya jambo jema sana la kuheshimu mamlaka za kisheria kwa kuwa watulivu kipindi chote lakini vinginevyo hapa machafuko yangetokea maana wananchi mpo wengi kuliko hao askari wao wanaolinda hilo shamba”, alisema Makala.

Pia alisema kwa maelezo aliyoyasikia kutoka kwa baadhi ya wazee wa kijiji hicho Ally Kidunda na Said Ahmad na viongozi wa Kijiji yaliyotolewa kwaa nyakati tofauti Mwekezaji huyo ndiye mvamizi wa eneo lao na si wananchi maana hata kijiji hakimtambui kwa maana hajawahi kufika kwao.

Nae Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Mvomero, Majaliwa Jaffari alisema watalishughulikia suala hilo haraka na hasa baada ya kufika eneo la tukio na kukiri kuna mapungufu katika ramani waliyonayo.

Agosti 23, mwaka huu wananchi hao waliitaka serikali kuingilia kati mgogoro huo haraka kabla ya machafuko kutokea wakati wakiwa katika mkutano wa hadhara uliokuwa uhudhuriwe na Mkurugenzi wa Wilaya na Maofisa wa Ardhi.
Posted by MROKI On Monday, August 29, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo