Nafasi Ya Matangazo

May 08, 2010


Dodoma

TIMU ya vijana ya taifa ya umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Herous, jana ilishindwa kuonyesha uwezo wake na kukubali kutoka sare ya bila kufungana na timu ya mkoa wa Singida katika mchezo wa kuwania kombe la taifa, ‘Kili Taifa Cup' uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani hapa.


Katika mchezo huo uliokuwa wa kasi katika dakika zote za mchezo, Ngorongoro Herous walionekana kucheza kwa nguvu zaidi na kuhimili mashabulizi yaliyokuwa yanafanywa na wapinzani wao ambao pia wengi walikuwa katika timu hiyo ya taifa.

Thomas Ulimwengu wa Ngorongoro Herous ndiye aliyekuwa wa kwanza kufanya shambulio katika lango la Singida katika dakika ya 10 lakini akiwa anakaribia kwenda kufunga aligongana na kipa wa Singida, Noley Luca na hivyo mwamauzi Abbas Omary kutolikubali goli alilokuwa amefunga mshambuliaji huyo na kuzua tafrani katika benchi la yosso hao.

Dakika tano baadaye, Ngorongoro Herous tena ilifanya shambulio la hatari kupitia kwa Abuu Ubwa lakini kipa wa Singida, Luca alifanikiwa kuuwahi mpira huo na kuudaka wakati dakika ya 17 Rajab Mohammed naye alipiga shuti kali katika lango la yosso hao ambalo liliokolewa na kipa wao, Faraji Kabali.

Kwa mara nyingine kipa wa Singida, Luca aliokoa shambulizi na kuinyima Ngorongoro Herous nafasi ya kupata bao kupitia kwa Rajab Isihaka kwa kudaka kiufundi shuti lililomlenga katika lango lake.

Kipindi cha pili Singida iliamka zaidi na kufanya mashambulizi kadhaa katika lango la Ngorongoro Herous ambapo dakika 50, Kiula Grayson, alipiga shuti zuri kwa wapinzani wao lakini liliokolewa na hivyo kupoteza nafasi hiyo.

Naye Rajab Mohammed alionekana kuwasumbua mabeki wa Ngorongoro lakini nafasi zote alizokuwa anapata alishindwa kuwapenya na hivyo mipira yake kupotea kirahisi na timu yake kuondoka ikijutia nafasi ilizopoteza.

Mkoani Mtwara timu ya Lindi ilianza vizuri mashindano haya kwa kuifunga Ruvuma 3-1 wakati mjini Tanga wenyeji walitoka sare ya 0-0 dhidi ya Morogoro mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani.

Leo ni mapumziko katika vituo vyote sita na mechi zinatarajiwa kuendelea kesho ambapo mkoani hapa Dodoma, Ngorongoro Herous itacheza na Dodoma huku Kigoma wakiikaribisha Singida.


MTWARA
Mtwara TIMU ya soka ya Mkoa wa Lindi imeanza vizuri Michuano ya Kili Taifa Cup iliyoanza jana kwenye viwanja mbalimbali kwa kuwabamiza wenzao wa mkoa wa Ruvuma "Ruvuma worrious" mabao 3-1 katika mpambano uliofanyika kwenye Uwanja wa Umoja mjini Mtwara.

Katika mpambano huo Lindi walianza kuandika bao dakika ya kwanza ya mchezo kupitia kwa Andrew Christopher baada ya kupata pasi ya mbali huku walinzi wa Ruvuma wakidhani mfungaji ameotea.

Wakati Lindi wakiendelea kufurahia bao lao Ruvuma walisawazisha kupitia kwa Edward Ajilo baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona.

Hekaheka ziliendelea kwa timu kushambuliana kwa zamu hata hivyo walikuwa Lindi tena waliofumania nyavu za wapinzani wao pale Ally Mohamed'Gaucho' alipopachika bao la pili dakika ya 30 baada ya kuwazidi mbio walinzi wa Ruvuma wakiongozwa na Patric Betwel na kufanya hadi mapumziko Lindi watoke kifua mbele kwa mabao 2-1.


Kipindi cha pili kilianza kwa vijana wa Lindi kuzidisha mashambulizi langoni mwa wapinzani wao na kufanikiwa kupata bao la la tatu katika dakika ya 70 kupitia Amani George kufuatia piga nikupige langoni mwa Ruvuma.

Ruvuma nao walijitahidi kutaka kusawazisha dakika 20 za mwisho lakini wakajikuta hadi mwisho wakichapwa mabao 3-1.

Mara baada ya mpira kumalizika kocha wa Lindi John William alisema anashukuru kupata ushindi huo kwani imempa faraja ya kufanya vizuri zaidi katika michezo ijayo hasa kwakua katika michuano iliyopita walianza kwa kupoteza.

Naye Peter Mhina wa Ruvuma alisema kipigo walichokipata kilitokana na uchovu uliotokana na barabara mbovu na kuahidi kushinda katika mchezo ujao dhidi ya Mtwara.

ARUSHA

MARA imeanza vyema kampeni ya kuwania Kombe la soka la taifa, Kili Taifa Cup baada ya kuilaza Kilimanjaro, mabao 3-2 katika mchezo wa ufunguzi wa kituo cha hapa, uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa.

Shukrani kwao, Noel Makunja, Mwita Kamaronge na Furumence Tungaraza wafungaji wa mabao ya washindi katika mchezo wa jana- wakati mabao ya kufutia machozi ya Kilimanjaro yalitiwa kimiani na Ben Rafael na Victor Ndozero.

Kilimanjaro walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 34, baada ya Ndozero kuuwahi mpira uliorudi na kufumua shuti kali lililogonga mwamba wa juu ndani kabla ya kutua kwenye mikono ya kipa Msafiri Shaibu, lakini mwamuzi Peter Mujaya aliyehamishia makazi yake Mwanza kutoka Pwani, akasema mpira uwekwe kati.

Makunja aliisawazishia Mara dakika mbili baadaye kutokana na shambulizi lao kali la kushitukiza, kabla ya Ndozero kuifungia Kilimanjaro bao la pli dakika ya 43.

Hadi mapumziko, Kilimanjaro walikuwa mbele kwa mabao 2-1- na kipindi cha pili, Mara ilianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika tatu tangu kuanza ngwe hiyo, kabla ya Tungaraza kufunga la ushindi dakika ya 56, akitumia udhaifu wa mabeki wa Kilimanjaro kudhani ameotea.

Katika mchezo huo, wachezaji wawili wa Mara walitolewa nje kwa nyekundu kwa kucheza rafu, hao ni Ismail Fundi aliyempiga kiwiko Amro Guya akilipa kisasi cha kukwatuliwa na dakika ya 88, kipa Emanuel Mseja naye alipewa adhabu hiyo, baada ya kumkwatua Philipo Alando wakati anakwenda kufunga.

Wakati huo, tayari Kilimanjaro walikuwa wamekwishakamilisha idadi ya wachezaji wa kubadilisha, hivyo Ndozero akavaa glavu na kumalizia mchezo.
Posted by MROKI On Saturday, May 08, 2010 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo