Dar es salaam - Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imepata viongozi wapya wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) ambao wataongoza kwa miaka mitano kufuatia uchaguzi uliofanyika katika Ofisi za BRELA makao makuu na kusimamiwa na Mkuu wa Uchaguzi ambaye ni Katibu wa TUGHE - Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo uliofanyika leo tarehe 23 Februari 2025, wanachama wa TUGHE, tawi la BRELA walipiga kura kumchagua Mwenyekiti wa tawi na Katibu wake, Mwenyekiti wa Kamati ya wanawake na Katibu wake, Mwakilishi wa vijana na walemavu pamoja na wajumbe.
Uchaguzi ulikuwa na ushindani mkali katika nafasi ya uenyekiti wa tawi ukiwakutanisha wagombea wawili wenye ushawishi mkubwa ambao ni Bw. Andrew Malesi kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu na Bw. Francise Philimbi kutoka Kurugenzi ya Leseni za Viwanda.
Aidha, kufuatia ushindani huo na hesabu ya kura zilizopigwa na wanachama wote, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Sara Rwezahula alimtangaza Bw. Francise Philimbi kuwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti kwa kupata kura 31 kati ya kura 51 zilizopigwa huku Bw. Andrew Malesi akipata kura 20 kati ya kura 51 zilizopigwa na wanachama wote.
Wengine walioibuka washindi katika uchaguzi huo ni Bi. Yvone Masele alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya wanawake kwa kupata kura 26 kati ya 30 zilizopigwa, Bi. Mgeni Shaban aliyeshinda nafasi ya Katibu wa Kamati ya wanawake kwa kupata kura 25 za ndio, kura 2 za hapana na moja iliharibika.
Kwa upande wa mwakilishi wa vijana, Bw. Ismail Masoud alishinda kwa kupata kura 48 za ndio huku kura 2 zikiwa za hapana na kwa upande wa mwakilishi wa walemavu Bi. Sophia Mtunzi alishinda kwa kupata kura 50 za ndio huku moja ikiwa ni hapana.
Awali akizungumza baada ya kutangaza washindi hao, Bi. Rwezahula alitoa rai kwa matawi mengine ya TUGHE ambayo yanaendelea na uchaguzi wa viongozi kuiga mfano wa tawi la BRELA kwa namna walivyoendesha uchaguzi kuanzia maandalizi mpaka mchakato wa kutangaza washindi.
Kwa upande wake Mwenyekiti ambaye amechaguliwa kwa mara nyingine Bw. Francise Philimbi ameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wengine waliochaguliwa pamoja na wajumbe wa tawi katika kuendeza yale mafanikio waliyoyapata kwa miaka mitano iliyopita.
“Chama chetu kilikuwa na wanachama 40 na tumeweza kuhakikisha tunaongeza wanachama mpaka kufikia 105 ambao wametupa imani kwa mara nyingine tena, lakini tumeweza kuweka mahusiano mazuri baina ya mwajiri na watumishi kwakuwa tumekuwa tukiunga mkono dira na maono ya taasisi.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya wanawake tawi la TUGHE BRELA, Bi. Yvone Masele alisema kwa miaka mitano iliyopita wameweza kufanya mambo mengi na kushirikiana pamoja akiahidi mazuri zaidi kwa kushirikiana kwenye changamoto za wanawake ili kupata muafaka wa pamoja katika kuzitatua na kusonga mbele.
Uchaguzi huo uliofanyika ulilenga kuwapata viongozi wapya ambao wataongoza tawi hilo kwa miaka mitano mingine na kuwa kiunganishi kati ya wafanyakazi na Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) ili kutatua changamoto za wafanyakazi na kuimarisha mahusiano mazuri baina ya mwajiri na watumishi.










0 comments:
Post a Comment