Katika hatua ya kihistoria na mageuzi ya Sekta ya Madini nchini, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini leo Februari 23, 2026 imesaini Makubaliano Maalum na Benki ya CRDB yatakayorahisisha upatikanaji wa huduma za fedha kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kihistoria iliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde (Mb) ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa utashi na uongozi thabiti unaoendelea kuibadilisha Sekta ya Madini kuendelea kuwavutia wawekezaji .
Waziri Mavunde amesisitiza kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa juhudi za makusudi za Serikali kujenga mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo wa madini kwa kuimarisha uchimbaji, biashara, kuongeza ufanisi, na kuimarisha mchango wa sekta katika Pato la Taifa (GDP).
“Tunawapongeza CRDB kwa kwenda “field”, kujionea uhalisia wa shughuli za uchimbaji, na kufanya maamuzi kupata taarifa sahihi na sio zilizopikwa. Nawapongeza kwa kuwa mmeanza kuielewa Sekta ya Madini, na hili litaongeza tija ya uwekezaji wenu, maendeleo ya sekta, na mapato ya taifa,” amesisitiza Mavunde.
Mhe. Mavunde ameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazowatambua wachimbaji wadogo kisheria, na kwamba Serikali inaendelea; kutoa leseni za uchimbaji kwa wachimbaji wadogo, kufuta leseni za utafiti zisizoendelezwa na kugawa maeneo kwa wachimbaji wadogo, na kujenga mazingira ya uwezeshaji ili wachimbaji wadogo waongeze uzalishaji, tija, na mchango wao kwa uchumi.
Hatua ya Kihistoria: Mkopo wa Shilingi Bilioni 50
Waziri Mavunde ameeleza kuwa katika hatua ya kihistoria Kikundi cha Wachimbaji Wadogo cha Songwe Gold Family kitakuwa cha kwanza kupata mkopo wa shilingi bilioni 50 kwa wakati mmoja, jambo ambalo halijawahi kutokea nchini, akiitaja hatua hiyo kuwa ya uthubutu wa kipekee kutoka Benki ya CRDB.
Pia, amebainisha kuwa, Serikali iko katika hatua za mwisho za kuanzisha Mfuko wa Dhamana kwa ajili ya kukopesha wachimbaji wadogo, ili kupunguza vikwazo vya upatikanaji wa mitaji na kuongeza kasi ya urasimishaji wa shughuli za uchimbaji.
Benki CRDB Yasema ni Mfumo Bunifu, Dhamana Rafiki
Akizungumza katika hafla hiyo , Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema mpango huu ni historia kwa benki na kwa Sekta ya Madini, kwani unaweka mfumo wa kisasa na shirikishi unaoendana na uhalisia wa wachimbaji wadogo kwa kuwa wanabeba sehemu kubwa ya sekta inayokua kwa kasi kwa miaka mitano mfululizo kuliko sekta nyingine.
“Changamoto tulizoona kwa wachimbaji ni ukosefu wa mitaji, teknolojia, na ushauri wa kitaalamu. Uwezeshaji wa sekta ndiyo msingi wa mapato ya taifa. Huu ni mpango wa mkakati wa kitaifa unaojumuisha elimu ya kifedha, urasimishaji wa shughuli, na kuimarisha mchango wa sekta kwenye GDP,” amesema Nsekela.
Kwa mujibu wa Dkt. Nsekela, tayari benki imeshatoa shilingi bilioni 186 kwa Sekta ya Madini, kati ya hizo bilioni 136 kwa wachimbaji wakubwa na bilioni 50 kwa wachimbaji wadogo.
“Tofauti kubwa ya mpango huu ni aina ya dhamana, si lazima kutumia mali zisizohamishika, dhamana zitajumuisha leseni halali za uchimbaji, leseni ya biashara ya dhahabu, hifadhi ya dhahabu ya mkopaji, pamoja na mikataba maalum” amesisitiza Nsekela.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amempongeza Waziri Mavunde kwa kuhakikisha mageuzi haya yanafikiwa katika kipindi cha uongozi wake kwa kushawishi Taasisi za Fedha kuwekeza katika Sekta ya Madini na leo ni ishara ya mafanikio ya jitihada hizo.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi CRDB, Dkt. Donald Mmari, ameeleza kuwa Sekta ya Madini inachochea na kufungamanisha sekta nyingine, na kwamba ni miongoni mwa sekta za vipaumbele katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Ameongeza kuwa mpango huu utaleta mageuzi ya kimkakati na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo, Rais wa FEMATA, John Bina, amesema wachimbaji watakwenda kumshukuru Rais Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulifanikisha jambo hilo la kihistoria, akisisitiza kuwa mpango huo ulikuwa kilio cha muda mrefu cha wachimbaji wadogo na sasa unafungua ukurasa mpya wa maendeleo kwa sekta hiyo.













0 comments:
Post a Comment