WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekagua ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani unaotekelezwa katika eneo la Bondeni City kwenye Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa gharama ya sh. bilioni 14.3.
Akizungumza na wafanyakazi na wananchi waliofika eneo hilo leo (Jumanne, Februari 24, 2026), Waziri Mkuu amesema ameona jinsi stendi iliyopangiliwa na amefurahishwa kuona kwamba wamebakiza eneo la akiba kwa ajili ya ujenzi wowote utakaohitajika kwenye awamu ya pili.
“Nimeona kuna eneo la akiba mmelibakiza. Pia kuna matoleo ya BRT ambayo mmesema ni maandalizi ya kuweka miundombinu ya mabasi yaendayo haraka. Maeneo mengine ya Zanzibar na Dar es Salaam yatakapofanyika mashindano haya ya AFCON, nayo tuwe kwenye standard hizohizo. Tuongee na sekta binafsi ili tupate fedha za mabadiliko ya tabianchi ili hapa Arusha tuwe na mabasi yanayotumia gesi,” amesema.
Amesema yakipatikana mabasi hayo, na stendi ikakamilika, kutakuwa na magari ya kubeba wageni watakaokuwa wamefika kushuhudia michuano ya AFCON.
Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Arusha, Paul Makonda amesema ziara za Waziri Mkuu zinawapa faraja na matumaini wananchi wengi wakiwemo wa Jiji la Arusha.
“Ziara yako sisi wananchi wa Arusha Mjini inatupa matumaini ya kuelekea nchi ya ahadi ambayo tumeahidi katika Ilani yetu; ujenzi wa uwanja unatokana na kazi njema inayofanywa na Chama cha Mapinduzi, kwa miradi hii hatuacha kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,” amesema.
“Tunaomba utuwekee alama za nyayo zako kila utakapopita katika hii miradi, iweze kukamilika kwa wakati ili wananchi wa Jiji la Arusha waweze kunufaika nayo. Wafanyabiashara wote watapata nafasi sawa katika stendi hii ili waweze kupata kipato na tunaamini kupitia stendi hii mji wetu wa Arusha utapumua.”
Mapema, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo alimweleza Waziri Mkuu kuwa mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika Mei 30, 2026 hadi sasa umefikia asilimia 49. Alisema mradi huo una lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kupunguza msongamano katikati ya Jiji na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji hilo.
Alisema itakapokamilika, stendi hiyo itakuwa na jengo kuu la kituo cha mabasi (ghorofa moja) na sehemu mbili za kusubiri abiria, maduka 23 ya biashara, maeneo mawili kwa wauza vyakula, vyoo vya kisasa pande zote mbili na nyumba ya walinzi. Vingine ni nyumba ya umeme (power house), tanki la maji, vituo vitano vya ukaguzi na ulinzi, vituo 20 vya kukusanyia taka na eneo maalum la dharura.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko la Kilombero unaotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha ili kuboresha huduma za biashara na miundombinu ya soko hilo.
Akizungumza na wananchi waliofika sokoni hapo leo (Jumanne, Februari 24, 2026), Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaeleza mafanikio yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika nyanja mbalimbali.
Amesema Rais Samia ameweza kukwamua miradi mikubwa ya maji ambayo awali ilikaa kwa muda mrefu bila kukamilika kama vile ya Mwanga-Same-Korogwe. Pia amenunua mitambo na vifaa kwenye sekta za maji na afya.
“Zamani tulikuwa na mitambo miwili au mitatu ya kuchimba visima lakini sasa hivi kila mkoa una mitambo yake. Pia kuna mitambo mitano ya kupima maji chini ya ardhi, kila kanda imepata mtambo wake. Na jana tu, nilishuhudia kule kata ya Sinya, wilaya ya Longido wamepata maji chini ya ardhi umbali wa mita 300 (sawa na viwanja vitatu vya mpira). Wamechimba maji na sasa yanaenda hadi Namanga.”
“Kwenye sekta ya afya, Mheshimiwa Rais wetu amenunua vifaa vya kisasa kwenye hospitali zetu. Amenunua mashine 32 za CT-scan sasa hivi kila hospitali za mkoa na rufaa zina vifaa vya kisasa, zamani zilikuwa kwenye hospitali chache sana. Amejenga hospitali mpya za wilaya 119, vituo vya afya 649 na zahanati 2,800.”
Kwa mujibu wa taarifa ya ujenzi wa soko hilo, hadi kukamilika linatarajiwa kugharimu sh. bilioni 9.5 na hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 43 ambapo kutakuwa na jengo la soko kuu lenye ghorofa mbili zenye vizimba 518, vibanda 70, majengo mawili ya vyoo kila moja likiwa na matundu 19 na vyumba viwili vya kubadilishia nguo.
Pia, kutakuwa na vyumba vya kulelea watoto, vyumba viwili vya ofisi, vyumba viwili vya kuabudia, maeneo 54 ya maegesho, sehemu saba za kukusanya taka na stendi ya kushusha/kupakia abiria.










0 comments:
Post a Comment