Nafasi Ya Matangazo

February 23, 2026

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Leonard Akwilapo.
*********
Na Mwandishi Wetu
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekanusha malalamiko ya Taasisi ya Al-Malid kuhusiana na umiliki wa kiwanja Na 8 Kitalu A kilichopo Nzuguni jijini Dodoma.

Akizungumza jijini Dodoma leo tarehe 23 Februari 2026, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Leonard Akwilapo amesema, malalamiko ya taasisi hiyo yalishughulikiwa kikamilifu na walalamikaji kujibiwa kwa maandishi kupitia barua yenye kumbukumbu namba BA 97/171/01L/28 ya tarehe 9/01/2026.

Kwa mujibu wa Dkt Akwilapo, kumbukumbu za umiliki zinaonesha Al-Malid iliwahi kumilikishwa kiwanja namba 1 Kitalu H Ihumwa jijini Dodoma wakati wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) tarehe 21 Machi 2009 kikiwa na ukubwa wa mita za mraba 181,700 kwa matumizi  ya taasisi.
Hata hivyo, amesema taasisi ya Al-Mallid ilikiuza kiwanja hicho kwa Kampuni ya Elishadai Centre for Academic Limited kupitia mkataba uliosainiwa tarehe 25 Julai 2009, na Wizara ilipatiwa nakala ya mauziano hayo.

Ameongeza kuwa, taasisi ya Al-Mallid ilianza kulalamika kuhusu kiwanja hicho tajwa mnamo mwaka 2019 na wataalamu wa Wizara waliomba kuoneshwa eneo linalolalamikiwa ambapo taasisi hiyo ilionesha maeneo tofauti kwa nyakati tofauti, ambayo ufuatiliaji uliofanyika ulibaini kuwa, maeneo hayo yana miliki halali za Taasisi nyingine na wao Al-Mallid hawakuwa na nyaraka zozote za kuthibitisha umiliki wao kwenye maeneo hayo.

Kupitia kumbukumbu za Wizara eneo lenye Kiwanja Na. 1 Kitalu ’H’, ni eneo ambalo taasisi ya Al- Mallid ililiuza kwa Kampuni ya Elishadai Centre for Academic Limited. Aidha, Wizara imekuwa ikiwafahamisha ukweli wa suala hili mara zote ambazo walifika kupata huduma.

Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameutaarifu umma kuwa upatikanaji na umiliki wa ardhi unasimamiwa kwa mujibu wa Sheria za Ardhi pamoja na kanuni zake. Sheria na Kanuni zimewekwa makusudi ili kuondoa migogoro kama hii na vilevile kuimarisha usimamizi bora wa rasilimali ardhi.

Amesisitiza kuwa, ni umuhimu kuzingatia Kanuni na Taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sharia ili kuondoa mgongano isiyo ya lazima katika jamii.

Tarehe 18 Februari 2026 Taasisi ya kiislamu ya Al-Mallid ya mkoani Dodoma iliilalamikia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa madai ya kusababisha sintofahamu ya umiliki wa kiwamja namba 8 Kitalu A Nzuguni C,  malalamiko ambayo yalisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Posted by MROKI On Monday, February 23, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo