WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba amezindua shule mpya ya sekondari ya Sinya ambayo ni ya bweni iliyojengwa katika kijiji cha Leremeta, wilayani Longido, Arusha kwa gharama ya sh. bilioni 1.23.
Akizungumza na wakazi wa kata ya Sinya na viongozi mbalimbali waliofika kushuhudia uzinduzi huo leo (Jumatatu, Februari 23, 2026), Waziri Mkuu ameelekeza suala la ujenzi wa uzio wa shule lifanyiwe kazi haraka kutokana uwepo wa wanyama wakali.
“Nimeridhishwa na ujenzi wa hii shule; taarifa nilizonazo zinaonesha ujenzi wake umezingatia thamani halisi ya fedha kwa ubora. Ombi la kuwekwa uzio hapa shuleni ni jambo la maana kwa sababu kuna wanyama wakali. Mkurugenzi angalia ndani ya mapato ya Halmashauri mnaweza kupata kiasi gani ili kazi hiyo ifanywe kwa haraka. Mkuu wa Mkoa simamia jambo hili ili liwe moja ya kipaumbele.”
“Nyumba za walimu kama alivyoomba Mkuu wa shule, Naibu Waziri wa TAMISEMI kaa nao muangalie uwezekano. Na mabweni yaliyoombwa ni muhimu yajengwe,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi, Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Andrew Emmanuel alisema shule hiyo ina wanafunzi 387 wa kidato cha kwanza hadi cha tatu na walimu 12 ambao kati yao tisa ni wa kiume na watatu ni wa kike.
Alisema bweni la wanafunzi wa kike limekamilika na linatumika na akaomba mabweni zaidi na nyumba za walimu kwani iliyopo ni moja inayoweza kutumika kwa familia mbili. Alisema nguvu ya wananchi ya sh. milioni 34 ilitumika kununua meza 140 na vitanda 80.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amekagua ujenzi wa mradi wa majisafi wa Sinya–Namanga ambao pia unatekelezwa katika kijiji cha Sinya, wilayani Longido, mkoani Arusha kwa gharama ya sh. bilioni 13.5.
Akitoa maelezo mafupi, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema kupatikana kwa maji kwenye eneo hilo kulitoka na uwepo wa mitambo ya kupimia maji chini ya ardhi iliyonunuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo iligawanywa kwenye kanda tofauti.
“Wananchi wa huku walikuwa wanategemea chanzo cha mto Simba ambacho hakitoshelezi lakini utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) ulibaini eneo la Ildonyo (Sinya) linafaa kuwa na kisima chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 2.4 kwa siku.”
Alisema uzalishaji wa sasa ni wastani wa lita milioni 1.7 kwa siku wakati mahitaji ni lita milioni 3.8 na kwamba mradi ukikamilika utaweza kuongeza uzalishaji hadi lita milioni 4.1 kwa siku, hivyo kuboresha huduma ya maji safi kwa wananchi na mifugo.



.jpeg)

.jpeg)






0 comments:
Post a Comment