Nafasi Ya Matangazo

February 18, 2010

Marehemu William Samike.
Na Mwandishi Wetu, Singida.

Aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya wa Kilwa, Singida na Sengerema, William Samike wa Samike (73) amefariki dunia kwa shinikizo la damu. Marehemu Samike alizikwa mkoani Singida jana (Februari 18)

Akizungumza na gazeti hili Mtoto wa Marehemu, Jeremiah Samike alisema kuwa baba yake alifariki dunia Jumatatu wiki hii baada ya kuanguka ghafla nyumbani kwake na kupoteza fahamu Februari 14, mwaka huu saa moja jioni ambapo alikimbizwa Hospitalini na kugundulika kuvia kwa damu katika ubongo ambapo madaktari na wauguzi walifanya jitihada za kuokoa maisha lakini bila mafanikio marehemu aliaga dunia.

Alisema kuwa mara baada ya kuanguka mke wa marehemu, Bibi Loyce Samike kwa kushirikiana na baadhi ya wanafamilia walimkimbiza Hospitali ya Mkoa wa Singida alikolazwa hadi mauti yalipomkuta Jumatatu saa 9 Alasiri.

Kabla ya kukubwa na tatizo hilo mwaka 2007 marehemu alipata tatizo la kibofu cha mkojo jitihada mbalimbali za matibabu zilifanyika kutibu tatizo hilo katika hospitali za Singida, Aga Khan, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Tumaini Dar es Salaam. Jitihada hizo zilizaa matunda na kurudisha afya yake kama kawaida.

Aidha mtoto wake huyo alisema kuwa marehemu aliyejulikana kwa jina maarufu la Samike wa Samike mwaka 1952- 1956 alisoma elimu ya Msingi katika shule ya Msingi Kijima Wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza. Mwaka 1957 -1958 elimu ya kati (middle school) katika shule ya Kazilankanda, Ukerewe na mwaka 1959 -1962 alipata elimu ya Sekondari Luwure Uganda.

Mwaka 1964 Marehemu alipata mafunzo ya Siasa na Uchumi katika Chuo cha Kivukoni, Dar es Salaam, mwaka 1967 alipata mafunzo ya Elimu ya Jamii katika Chuo cha Tengeru, Arusha na alipata mafunzo ya jeshi katika kambi ya Ruvu (Ruvu National Service mwaka 1969-1970.

Aliendelea kusema kuwa alipata mafunzo ya Kilimo katika Chuo cha Ukiriguru Mwanza mwaka 1970 na mwaka huo huo alijiunga na mafunzo ya Siasa na Uongozi katika Chuo cha Kivukoni.

Marehemu aliwahi kufanya kazi mbalimbali za Ualimu huko Ukerewe mwaka 1963, Karani wa kodi na mahakama kati ya mwaka 1963 na 1964 huko Busongo Kwimba mkoani Mwanza. Bwana Maendeleo Msaidizi (Community Development Assistant) kati ya mwaka 1964-1969 katika kata za Kahangara, Ishingisha na Mantare za Kwimba.

Vile vile marehemu aliwahi kuwa katibu Tarafa za Nanjilinji, Kivinje na Kipatimu za wilayani Kilwa mkoa wa Lindi kati ya mwaka 1969-1981.

Aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya na Katibu wa CCM 1981-1990. Wilaya alizofanyia kazi ni Kilwa, Singida na Sengerema. Marehemu alistaafu mwaka 1992 na baadaye kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Bomani, Singida, Mshauri katika Idara ya Magereza na Elimu, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Mwenge, Mjumbe wa Baraza la Ardhi wilaya. Hadi anaaga dunia alikuwa mkulima stadi katika shamba lake lililopo Kijiji cha Mudida Singida na mfugaji.

Marehemu ameacha mke Bibi Loyce Gwandasa Samike na watoto 12 ambao ni Samwel, Jeremiah, Christina, Mahona, Sundi, Angelina, Msafiri, Leah, Minza, Esther, Lochiba na Elizabeth na wajukuu 28.
Posted by MROKI On Thursday, February 18, 2010 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo