Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mary Chatanda, amesema katika zama hizi za kutafuta fursa za kiuchumi duniani, sera ya kutofungamana upande wowote, inafaa zaidi kutumiwa.
Chatanda ameyasema hayo Juni 16, Jijini Dodoma, alipokuwa akitoa maoni yake kutokana na mwelekeo wa serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuifungua nchi kimataifa na mkakati wa kuhimiza diplomasia ya kiuchumi.
"Hii ya kusema mimi rafiki yangu huyu, yule adui yangu, sio nzuri, hii ya kusema nampenda huyu namchukia yule, kisa ana ugomvi na nchi mshirika wako haifai. Tanzania chini ya Rais Dk. Samia tumejitanabaisha kuwa hatufungamani na upande wowote.
Kutofungamana pande wowote kutatupa uwanja mpana wa kushirikiana na mataifa mengi duniani na kufaidi fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazoweza kuleta tija kwa wananchi na Taifa letu," amesema Chatanda.
Sambamba na hilo, Chatanda amesema wakati mwingine nchi inanunua ugomvi usiowahusu kisa tu mataifa mawili yamegombana na hivyo nchi kumchukia nchi aliyegombama na rafiki mshirika wake.
"Tanzania tumekataa kujiingizia katika ugomvi usiotuhusu, sisi tunakwenda na yeyote ilimradi tunaona ana dhamira ya dhati ya kushirikiana na sisi katika kuchochea maendeleo. Ndiyo maana binafsi, nasimamia na Rais wetu kwa msimamo huu wa kutofungamana upande wowote," amesisitiza Chatanda.
Aidha, Chatanda amesema tunahitaji kushirikiana na mataifa mengi duniani na kila Taifa lina upekee wake katika nyanja mbalimbali kama kilimo, nishati, teknolojia, madini, elimu, afya, hivyo Tanzania inajiweka pazuri katika kuwa na washirika wengi wa maendeleo.
Ikumbukwe kuwa, Rais Dk. Samia alipokuwa ziarani nchini Urusi, katika mahojiano yake na mwandishi wa habari, aliulizwa Tanzania inawezaje kuhusiana na mataifa tofauti katika kipindi ambacho mazingira ya uchumi wa dunia yamebadikika.
Akijibu swali hilo, Rais Dk. Samia amesema "Tanzania inafuata misingi ya kutofungamana na upande wowote. Kwahiyo, adui wa rafiki yetu si adui wetu, na rafiki wa adui yetu si adui wetu".
Kimsingi, Tanzania inaendelea kusimamia sera ya diplomasia ya kiuchumi yenye mkazo wa kushirikiana na mataifa mengine ulimwenguni huku mashirikiano hayo yakiwa na wajibu wa kuleta manufaa kijamii na kiuchumi kwa pande zote.





.jpeg)



0 comments:
Post a Comment