Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi imetangaza ratiba ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura kwenye mikoa ya Ruvuma, Njombe, Songwe na Rukwa ambapo zoezi hilo
litafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 12 hadi 18 Januari, 2025.
Hayo
yameanishwa kwenye hotuba ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji
wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jacobs Mwambegele iliyosomwa kwa niaba yake kwenye
mikutano ya Tume na wadau wa uchaguzi iliyofanyika leo tarehe 31
Desemba, 2024 kwenye mikoa ya Ruvuma,
Njombe, Songwe na Rukwa.
Mhe.
Mwambegele ambaye aliwakilishwa na wakurugenzi mbalimbali wa Tume kwenye
mikutano hiyo, amesema mikoa hiyo
itafanya uboreshaji kwenye mzunguko wa tisa na kwamba tayari Tume imekamilisha
uboreshaji kwenye mikoa 19 ambayo ilijumuisha mizunguko nane kati ya mizunguko
13 ambayo imepangwa kukabilisha zoezi hilo nchini.
“Leo tupo
hapa Songwe na wenzetu wapo kwenye mikoa ya Njombe, Rukwa na Ruvuma ikiwa ni
maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mkoa huu wa Songwe, Njombe, Rukwa na
mkoani Ruvuma kwenye Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Mbinga, Mbinga Mji, Wilaya
ya Songea na Manispaa ya Songea, zoezi litakalofanyika kwa muda wa siku saba kuanzia
tarehe 12 Januari, 2025 na kukamilika tarehe 18 Januari, 2025 na ambapo vituo
vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,”
imesema sehemu ya hotuba hiyo.
Ameitaja
mikoa ambayo tayari imekamisha zoezi hilo kuwa ni Kigoma, Tabora, Katavi,
Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida.
“Mikoa
mingine ni mikoa ya Zanzibar ambayo ni Mjini Magharibi, Kusini Unguja,
Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Arusha na Kilimanjaro. Kwa
sasa mikoa miwili ya Mbeya na Iringa inatarajia kukamilisha zoezi hilo tarehe
02 Januari, 2025,” imesema sehemu ya hotuba hiyo.
Mada ya
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani iliyowasilishwa kwa niaba yake
kwenye mikutano hiyo imeanisha kwamba kwenye mikoa hiyo jumla ya wapiga kura wapya
475,743 wanatarajiwa kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mada hiyo
imeanisha kuwa uboreshaji wa Daftari utakapokamilika, mikoa hiyo inatarajiwa
kuwa na jumla ya wapiga kura 3,091,485 ikilinganishwa na idadi ya wapiga
kura 2,615,742 waliokuwemo kwenye Daftari mwaka 2020.
“Idadi hii
inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa
za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20,
lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha,” imesema sehemu ya
mada hiyo.
Mada hiyo
imeanishwa kuwa kutakuwa na vituo 3,785 ikiwa ni ongezeko la vituo 233 kutoka
vituo 3,552 vilivyokuwepo mwaka 2020.