Nafasi Ya Matangazo

March 30, 2025

Na: Dk. Reubeni Lumbagala, 
Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inawajibika kupokea maombi ya mikopo na kutoa mikopo kwa waombaji waliokidhi vigezo vilivyowekwa. Bodi ya Mikopo ambayo sasa imetimiza miaka ishirini tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004, inajivunia kutoa takribani shilingi Trilioni 8 kwa waombaji mbalimbali ambao sasa si waombaji tena bali ni wanufaika wa mikopo hiyo. 

Kiukweli, fedha hizi ni nyingi sana ambazo zimetolewa na serikali kwa nia njema ya kuwasaidia wanafunzi ambao kutokana na hali za kiuchumi hawawezi kugharamia gharama za elimu ya juu wenyewe, hivyo kuhitaji kuwezeshwa raslimalifedha ili kumudu kulipa ada, malazi, kununua chakula, vitabu, kuhudhuria mafunzo kwa vitendo na masuala mengineyo.

Ni muhimu kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kufahamu kuwa mikopo waliyokopeshwa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo inapaswa kurejeshwa pindi wanapohitimu masomo yao hasa baada ya kuwa na kipato ili kuwawezesha waombaji wengine kunufaika nayo. Wigo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi unaweza kuongezeka endapo wanufaika waliohitimu masomo yao watarejesha mikopo hiyo kwa wakati. Bila marejesho mazuri kutoka kwa wanufaika, waombaji wengi watakosa mikopo na mwisho watashindwa kuendelea na elimu ya juu.

Kwamba, ni muhimu kwa wanufaika wahitimu wenye kipato yaani walioajiriwa au kujiajiri wenyewe kurejesha mikopo yao kwa hiari ili kuwa na uendelevu mzuri wa utoaji mikopo kwa kuzingatia kuwa kila mwaka kuna ongezeko kubwa la waombaji wa mikopo ambao wanasifa za kukopesheka ambao kupitia marejesho ya wanufaika, Bodi ya Mikopo itaweza kuwakopesha waombaji wengi zaidi.

Waajiri wanao wajibu wa kuwasilisha taarifa za wafanyakazi wao wenye elimu ngazi ya Stashahada au Shahada ili Bodi ya Mikopo iweze kujiridhisha kama wafanyakazi hao ni wanufaika wa mikopo au la. Na endapo itathibitika kuwa mfanyakazi ni mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu, mwajiri atapaswa kukata asilimia kumi na tano ya mshahara wa mfanyakazi mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu kila mwezi na kuwasilisha makato hayo Bodi ya Mikopo hadi pale mfanyakazi mnufaika atakapomaliza deni lake lote.

Aidha, kwa waliojiajiri wenyewe kama mamalishe, babalishe, bodaboda, mafundi wa fani mbalimbali, wakulima, wafugaji, wavuvi na wengineo, wanaweza kujisajili kwenye mfumo ili kujua deni lao na kupata Namba Maalum ya Malipo (Control number) ambayo wataweza kulipa kiasi fulani cha fedha kulingana na kipato wanachoingiza ili mwisho wa siku waweze kumaliza deni lote na kuwawezesha wengine kupata mikopo kama walivyopata wao. Pia, kupitia kujisajili huko kwenye mfumo, wahitimu wanufaika watajua mwenendo wa taarifa za madeni yao.
Kimsingi, utaratibu wa kulipa deni si lazima mnufaika awe ni mfanyakazi wa sekta rasmi yaani aliyeajiriwa. Hapana. Hata aliyejiajiri mwenyewe au asiye katika ajira rasmi anaweza kuanza kulipa deni lake hadi akamaliza kulilipa deni lote. Cha muhimu ni mnufaika mhitimu awe na kipato, na kipato kinaweza kuwa ni kwa kuajiriwa au kujiajiri.

Ni hivi: Lipo kundi kubwa la wanafunzi wanaohitaji kukopeshwa ili kutimiza ndoto zao za kielimu, njia mojawapo ya kuwasaidia wanafunzi hawa ni wanufaika wahitimu kulipa kwa hiari mikopo yao ili nao waweze kukopesheka. Pengine mhitimu mnufaika anaweza kuwa ana kipato lakini hajaanza kurejesha mkopo wake, ni vyema kujifichua na kuanza kulipa kwa hiari. Kwa kufanya hivyo, mhitimu mnufaika atakuwa ameshiriki kutimiza ndoto za kielimu za vijana wengi wanaohitaji kuwezeshwa mkopo, na huu ndiyo uzalendo na moyo wa kupenda maendeleo.

Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni iliyoko Wilaya ya Pangani mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800 462.
Posted by MROKI On Sunday, March 30, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo