Nafasi Ya Matangazo

April 04, 2025









Serikali itaanza kutekekeza Programu ya kuendeleza miji iliyochakaa katika majiji sita ya Arusha, Dar es salaam, Dodoma, Mwanza Mbeya na Tanga.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.  Deogratius Ndejembi Aprili 04, 2025 katika mkutano wa hadhara na wananchi wa mtaa wa Makangira, Kata ya Msasani wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam wakati akitambulisha program hiyo.

Waziri Ndejembi amesema, kwa kuzingatia matakwa Sera ya Taifa ya mwaka 1995 Toleo la mwaka 2023 iliyozinduliwa  hivi karibuni na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Programu hiyo maalum ya uendelezaji upya maeneo chakavu katika miji inalenga kukabiliana na changamoto za ukosefu wa huduma za msingi, miundombinu, makazi duni au chakavu, ukosefu wa mifumo ya maji taka na uwepo wa changamoto ya taka ngumu zinapelekea uchafuzi wa mazingira. 

"Wizara imetambua jumla ya maeneo 111 katika mikoa 24 ambapo kwa kuanzia Programu hiyo itatekelezwa katika majiji ya Arusha, Dar es salaam, Dodoma, Mwanza Mbeya na Tanga". Amesema

Akizungumzia utekelezaji wa programu hiyo katika eneo la Makangira, Msasani jijini Dar es Salaam Mhe. Ndejembi amesema, wakati wa utekelezaji wa programu hiyo hakuna mwananchi hata mmoja atahamishwa katika eneo analoishi pale mradi utakapoanza isipokuwa kwa wachache.

Kwa mujibu wa Mhe. Ndejembi, Serikali itawapangishia nyumba wakazi wa maeneo husika wakati mradi ukiendelea kutekelezwa na baada ya kukamilika watarejea katika maeneo yao.

Amebainisha kuwa, program hiyo ina faida nyingi ikiwemo upatikanaji wa ardhi iliyopangwa kwa matumizi mbalimbali, upatikanaji wa nyumba hususani za makazi na biashara pamoja na kutatua changamoto ya makazi duni katika maeneo ya miji nchini.

Faida nyingine ni pamoja na uboreshaji  madhari ya miji sambamba na kuongeza usalama wa milki za wananchi katika maeneo husika kwa kupatiwa hati za sehemu ya jengo na kuwawezesha  kiuchumi kwa kugeuza ardhi mfu kuwa na thamani.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Saad Mtambule amesema, program ya kuendeleza miji iliyochakaa katika eneo la Makangira itakuwa suluhisho la changamoto ya mafuriko, magonjwa ya mlipuko, migogoro ya ardhi pamoja na kusaidia kuongeza thamani ya ardhi katika eneo hilo kwa kuweka miundombinu ya maji na barabara hatua aliyoieleza kuwa, itaboresha  makazi ya wananchi wa eneo la Makangira jijini Dar es salaam.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Songoro Mnyonge ameeleza kuwa, ujio wa program katika manispaa yake umekuja muda mwafaka ambapo manispaa hiyo mwaka 2013 ilipitisha Mpango wa Kuboresha  Makazi ili kupata nyumba bora za wananchi wa manispaa hiyo.
Posted by MROKI On Friday, April 04, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo