Nafasi Ya Matangazo

August 08, 2026

Na: Mwandishi Wetu
Mpango wa serikali wa kutoa mikopo isiyo na riba ya asilimia kumi kwa wanawake, vijana na wenye mahitaji maalum, imeonyesha kuzaa matunda kwa wananchi wa Mbalizi mkoani Mbeya.

Hii ni kutokana wa wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo ya kujikwamua kiuchumi na kubadili hali za maisha yao.

Matokeo chanya hayo yameonekana katika ziara ya Wajumbe wa Baraza la Utekelezaji la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Mary Chatanda, Agosti 6, 2026.

Akiwa katika ziara hiyo, Chatanda ametembelea kikundi cha wauzaji wa nafaka ambacho kimenufaika na mkopo wa shilingi milioni 56. Kikundi hicho kimefanikiwa kurejesha robotatu ya mkopo huo. Kutokana na uaminifu huo, Chatamda ameeleza wakimaliza mkopo huo, wakopeshwe tena kwa kuwa wamefanya vizuri katika marejesho ya mkopo wao.

"Mmefanya vizuri kukopa ili mjikwamue kiuchumi, na kwa kuwa mmefanikiwa kurejesha robotatu ya mkopo wenu, nitoe wito kwa uongozi wa Halmashauri kuwakopesha tena pindi mtakapomaliza mkopo wenu wote, na mimi nawachangia 1,200,000 ili mlipe pango kwa kipindi cha mwaka mzima," amesema Chatanda.

Vilevile, ujumbe wa UWT Taifa, ulitembelea kikundi cha mamalishe cha stendi ya Mbalizi ambacho kimekopeshwa milioni 50. Kikundi hicho kimeendelea kurejesha vizuri mkopo wao na kufanikisha kuzalisha biashara nyingine.

Halikadhalika, wamewatembelea wanawake wauzaji wa matunda katika stendi hiyo, ambapo Chatanda aliwapa elimu ya ujasiriamali na kuwachangia 300,000 ili iongeze mtaji katika biashara yao.





 

Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments

Na Mwandishi wa OTR
Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara na Maendeleo (TDB), Bw. Admassu Tadesse, kuhusu namna benki hiyo inavyoweza kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha ufanisi wa uwekezaji wa Serikali.

Mazungumzo hayo yana umuhimu wa kipekee kwa Tanzania kwa kuzingatia kwamba Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, inamiliki asilimia 8.3 ya hisa katika TDB na hivyo kuwa miongoni mwa wanahisa wa benki hiyo ya maendeleo ya kikanda.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam yalijikita katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo namna TDB inavyoweza kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Tanzania na kuimarisha ufanisi wa uwekezaji wa Serikali.

Bw. Mchechu alisema ushirikiano kati ya Tanzania na TDB ni muhimu katika kuendeleza uwekezaji, biashara na upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya miradi yenye mchango katika maendeleo ya uchumi.

Alisema TDB, kama taasisi ya fedha ya maendeleo ya kikanda, ina nafasi muhimu katika kusaidia Tanzania kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali na kuongeza thamani ya uwekezaji wa umma unaosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, wenye thamani ya Sh92.3 trilioni.

Bw. Mchechu alisema Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kuboresha utendaji wa taasisi za umma, huku akisisitiza uwajibikaji, ufanisi, uongozi wenye ufanisi na matumizi bora ya rasilimali za umma.

Alisema mageuzi hayo yanaenda sambamba na juhudi za kuhakikisha taasisi na kampuni zinazomilikiwa na Serikali zinafanya kazi kwa ufanisi zaidi, zinatimiza malengo ya kuanzishwa kwake na kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Bw. Tadesse alisema TDB iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kusaidia juhudi za maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji.

Alisema benki hiyo imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kutoa masuluhisho mbalimbali ya kifedha, ikiwemo ufadhili wa kibiashara, fedha za masharti nafuu na mifumo ya ufadhili mseto, kwa ajili ya kusaidia miradi yenye mchango katika maendeleo.

Bw. Tadesse alisema TDB inaiona Tanzania kama nchi yenye fursa kubwa za uwekezaji na ambayo inaendelea kuchukua hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wake.

Alisema benki hiyo inalenga kuelekeza mtaji katika nchi na miradi ambayo inaweza kuleta matokeo ya kiuchumi, kijamii na kifedha, huku ikisaidia kuongeza uzalishaji, biashara na uwekezaji.

Alisema benki hiyo imekuwa ikishirikiana na washirika mbalimbali wa maendeleo katika kuandaa mifumo ya ufadhili inayoweza kusaidia miradi yenye umuhimu wa maendeleo, hasa katika maeneo ambayo bado hayajafikia kiwango cha kuvutia mitaji ya kibiashara kwa kiwango kikubwa.

Mshauri wa TDB, Bw. Anthony Mwithiga, alisema benki hiyo imeendelea kujenga mifumo mbalimbali ya ufadhili inayolenga kuziba mapengo ya mitaji na kusaidia miradi yenye umuhimu wa kiuchumi na kijamii.

Bw. Mwithiga alisema TDB inaweza kutumia uzoefu wake katika kuunganisha vyanzo mbalimbali vya fedha, ikiwemo mitaji ya kibiashara, fedha za masharti nafuu na rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo, kulingana na mahitaji na aina ya mradi.
Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments

 

Na WMA- Dodoma

Wakala wa Vipimo (WMA) umetakiwa kupanua mpango wa kuanzisha klabu za vipimo shuleni hadi katika shule za sekondari, ili kuongeza wigo wa elimu ya vipimo na kuhakikisha uelewa wa matumizi sahihi ya vipimo unafika hadi ngazi ya kaya.

Wito huo umetolewa na Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Patroba Chaulo, ambaye amepongeza WMA kwa kuanzisha klabu hizo katika shule za msingi, akisema matumizi ya wanafunzi kama mabalozi wa elimu ya vipimo ni mkakati wenye tija kubwa kwa jamii.

Amesema mpango huo unatoa fursa ya kutumia mfumo wa elimu wa “mtoto kwa mtoto” (child-to-child), ambapo wanafunzi huweza kufikisha elimu na ujumbe kwa wenzao kwa urahisi zaidi, na hatimaye kuwafikishia wazazi na familia zao.

Kwa mujibu wa Chaulo, njia hiyo inaweza kuwa na ufanisi mkubwa kwa sababu wanafunzi wana nafasi kubwa ya kushirikiana na kuwasiliana na wenzao kwa lugha rahisi na inayoeleweka, jambo linalorahisisha uenezaji wa elimu ya vipimo.

“Mtoto anaweza kumwelewesha mtoto mwenzake kwa urahisi zaidi kuliko mtu mzima anapojaribu kumwelewesha mwanafunzi. Hii inafanya mfumo wa child-to-child kuwa fursa muhimu katika kueneza elimu ya vipimo,” amesema.

Ameeleza kuwa umuhimu wa mpango huo hauishii shuleni pekee, bali unaweza kusaidia elimu ya vipimo kufika hadi ngazi ya kaya, kwa kuwa wanafunzi wanaotoka katika klabu hizo wanaishi katika familia na jamii mbalimbali.

Amesema kupitia wanafunzi hao, WMA inaweza kuwa na mtandao mpana wa mabalozi ambao utasaidia kufikisha ujumbe kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi katika maeneo ambayo ni vigumu kwa Wakala kufika moja kwa moja.

“WMA haiwezi kufika katika kila nyumba, lakini wanafunzi hawa wanatoka katika kaya mbalimbali. Hivyo, wanakuwa kiungo muhimu cha kufikisha elimu hii kutoka shuleni hadi katika familia na jamii kwa ujumla,” amesisitiza.

Chaulo amesema elimu hiyo ni muhimu katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya vipimo sahihi na vilivyothibitishwa, hususan katika shughuli za kila siku zinazohusisha biashara na miamala mbalimbali.

Amesema jamii yenye uelewa kuhusu vipimo inaweza kutambua umuhimu wa kuhakikisha bidhaa zinapimwa kwa vipimo sahihi na kulinda haki za watumiaji pamoja na wafanyabiashara.


Kwa msingi huo, amependekeza WMA kuendelea kuimarisha klabu hizo katika shule za msingi na kuzitanua hadi shule za sekondari ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kujenga kizazi chenye uelewa mpana kuhusu viwango na vipimo.

Ameongeza kuwa uwekezaji katika elimu ya vipimo kupitia shule ni hatua muhimu ya kujenga utamaduni wa matumizi sahihi ya vipimo nchini, huku wanafunzi wakitumiwa kama sehemu ya suluhisho la kufikisha elimu hiyo katika jamii.

Mpango huo pia unatarajiwa kuongeza uelewa wa Watanzania kuhusu umuhimu wa kuwa na viwango na vipimo sahihi na vilivyothibitishwa (standards in measurements) katika maisha ya kila siku, hususan katika shughuli zinazohusisha biashara, ununuzi na uuzaji wa bidhaa.
Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments

August 07, 2026


Na Neema Chalila Mbuja
WIZARA ya Maliasili na Utalii imevunja rekodi ya kupokea  wageni zaidi ya 17,000  kwa siku kwenye  Maonesho ya mwaka huu ya Wakulima, Wafugaji  na Wavuvi maarufu  lama NANE NANE yanayoendelea kitaifa kwenye Viwanja vya John Malecela, Nzuguni Jijini Dodoma.

Makundi makubwa ya wananchi, wanafunzi na wadau mbalimbali wa uhifadhi na wanyamapori wamefurika kwenye banda l Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kuona wanyama aina mbalimbali waliopo kwenye bustani ya wanyamapori kwa lengo la kutangaza utalii wa ndani. 

Idadi hiyo inafanya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kuvunja  rekodi ya kutembelewa na wananchi wengi ambapo Bi. Amina Saleh  mmoja wa wananchi waliotembelea bustani ya wanyama anasema wamefurahishwa sana na ujio wa wanyamapori hao kwani hajawahi kuwaona wanyama ana kwa ana zaidi ya kwenye picha.

Tembo Mary aliyekuwa kwenye bustani hiyo ya Maonesho ya wanyamapori amekuwa kivutio kwa wanafunzi wengi na wananchi kwa ujumla kutokana na historia yake na usikivu alionao ambapo mwanafunzi Collins Msemwa wa Kato Victoria Academy anasema kuwa ziara hiyo ya shule imehamasisha wanafunzi wengi kupenda wanyamapori na kujifunza kwa kina tabia za wanyamapori hao.

Mamlaka ya Usimamizi wa  Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo ndiyo msimamizi wa wanyamapori imefanikiwa kuleta wanyama Kama  Tembo, Simba, Nyumbu, Pofu, Ngiri maarufu Kama Kasongoyeye, Duma, Chatu, ndege Karani, Mbuni, ndege Korongo (Crane) ambaye ni alama ya nchi ya Uganda, na ndege Mwali (White Perican bird) mbalimbali waliopo kwenye bustani ya NANE NANE.






Posted by MROKI On Friday, August 07, 2026 No comments
Muonekano wa eneo utakapotekelezwa Mradi wa Bwawa la Farkwa, ujezi unatarajiwa kuanza Oktoba, 2026, katika Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.
Na Adelina Johnbosco – MAELEZO
Tatizo la uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dodoma linaelekea kupata ufumbuzi wa kudumu kufuatia ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Farkwa utakaoanza kujengwa Oktoba mwaka huu.

Bwawa hilo litakalojengwa wilayani Chemba, kata ya Farkwa mkoani Dodoma litakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 128 kwa siku na kuhifadhi lita bilioni 390 na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 22.

Bwawa hili litahudumia hasa wilaya za Chemba, Bahi, Chamwino na maeneo mengine ndani na maeneo ya karibu na mkoa wa Dodoma, lengo ni kutokomeza kabisa upungufu wa maji ndani ya mkoa huo.

Ujenzi wa bwawa la Farkwa utatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya Shilingi bilioni 163.43 hadi kukamilika kwake.

Aidha, jumla ya Shilingi bilioni 8.5 zimelipwa kama fidia kwa wananchi kutoka katika vijiji viwili vya Mombose na Bubutole waliopisha ujenzi.

“Tuliambiwa tunahamishwa na kulipwa, mwaka 2017 tathmini ilifanyika katika maeneo yetu, ila ukiwa bado hujapokea kitu mkononi unaona kama haiwezekani, lakini mwaka 2019 tukalipwa fidia zetu, tukaanza maisha mapya na yenye matumaini zaidi katika kijiji cha Sankwaleto kwenye makazi mapya” Bi. Rahma Petro, mkazi wa Farkwa

Hadi hapa, tayari inaonekana Dodoma yenye ukijani wakati wote, iwe mvua iwe jua, hakuna tena ukame katika mkoa huu pale mradi huu utakapokuwa umekamilika, yale yaliyokuwa yanasubiriwa kufanyika wakati wa kipindi cha mvua pekee yatafanyika pia kipindi cha kiangazi.

“Tumeajiandaa kwa vingi kwa kweli, kijamii na kiuchumi, tutalima kilimo cha umwagiliaji, tutafuga samaki na mengine mengi, ni furaha tupu. Hii ilikuwa ni hadithi ya muda mrefu ambayo tumezaliwa tukaikuta kutoka kwa wazee wetu, hakika leo inatimia” Bw. Suleiman Gawa, mkazi wa Farkwa

Akiwa katika eneo utakapotekelezwa mradi huo, hivi karibuni, Bw. David Manyama, Mhaidrojiolojia ambaye ni mtaalam wa maji chini ya ardhi kutoka Wizara ya Maji, amebainisha uwepo wa maji ya akiba kwa watumiaji kutokana na wingi wa lita za maji utaokaozalishwa na bwawa hilo.

“Mradi huu unaanza mwezi Oktoba, 2026, maandalizi yako tayari na baada ya kukamilika kwa mradi, si kwamba utaondoa kero ya maji tu bali hata kuchochea miradi mbali mbali ya kiuchumi kama vile kilimo cha umwagiliaji kisichosubiri msimu, ufugaji wa samaki na itakuwa ongezeko la maji katika hifadhi ya pori la akiba Swagaswaga Chemba, wanyama hifadhini watapata maji ya kunywa ya kutosha tofauti na hali ilivyo kwa sasa” Bw. David Manyama, Mhaidrojiolojia

Mradi huu mwisho wake ni kuleta maji, lakini suala la ajira wakati na baada ya mradi ni vitu vinavotegemewa pakubwa. Mwenyekiti wa kijiji chenye makazi mapya cha Sankwaleto, akaongea kuhusu wazawa kupata fursa mbalimbali kutokana na mradi huo.

“Kama kiongozi tumeshashirikishwa na kuhakikishiwa kwamba, sisi wazawa tutapewa kipaumbele katika fursa mbalimbali zinazotokana na huu mradi ikiwemo ajira wakati na baada ya ujenzi, hivyo nawasihi vijana na wakazi wenzangu wa hapa kuwa tayari, tusikubali kukaa kinyonge katika kuchangamkia fursa katika hizi” Bw. Khalifa Salum, mwenyekiti wa kijiji chenye makazi mapya Sankwaleto

Si nyumba na umiliki wa ardhi pekee kwenye maeneo ya makazi mapya waliohamia wananchi waliopisha mradi, bali shule na zahanati vimejengwa kwa ajili ya kuwahudumia.

“Kijiji cha Sankwaleto kimejengwa shule ya msingi na imeshaanza kazi, kuna nyumba za walimu na wanafunzi wote waliokuwa wakisoma kule kwenye vijiji vya zamani wako kwenye shule mpya wanaendelea na masomo, hakuna kilichosimama, pia zahanati inayowahudumia wananchi, kwa kweli tunashukuru sana” – Bi. Agnes Msote, Diwani wa kata ya Farkwa

Kukamilika kwa Bwawa la Farkwa kunatarajiwa kuimarisha usalama wa maji katika jiji la Dodoma na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo.

Juhudi hizo zinaendana na azma ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji nchini kwa kuzingatia usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na upatikanaji wake maeneo yote hasa katika maeneo ya vijijini pamoja na kuhakikisha juhudi za kufikisha huduma za maji katika vijiji vyote nchini linatimia ili kumtua mwanamke ndoo kichwani.
Posted by MROKI On Friday, August 07, 2026 No comments
 

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,  Agosti 7, 2026, ametembelea Banda la Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha katika Maonesho ya Wakulima Nanenane Kanda ya Mashariki 2026 yanayoendelea mkoani Morogoro na kuvutiwa na ubunifu mbalimbali unaooneshwa katika banda hilo.

Akiwa katika ziara hiyo, Dkt. Kikwete alipata fursa ya kujionea teknolojia ya kilimo mseto (Integrated Farming) inayolenga kuongeza tija kwa wakulima wenye maeneo madogo kwa kuunganisha shughuli za kilimo, ufugaji na matumizi bora ya rasilimali zilizopo.

Pia alivutiwa na ufugaji wa ng’ombe aina ya Sahiwal, ambao ni ng’ombe wenye uwezo mkubwa wa uzalishaji wa maziwa na wanaofaa kwa mazingira ya Tanzania. Katika maelezo yaliyotolewa na wataalamu wa banda hilo, Dkt. Kikwete alifurahishwa zaidi na simulizi ya kijana anayejishughulisha na ufugaji huo wa kisasa.

Halmashauri inaendelea kuwakaribisha wananchi, wadau, wawekezaji na wananchi wote kutembelea banda lake ili kujionea fursa, ubunifu wa kilimo na ufugaji, vivutio vya kipekee pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa.


Posted by MROKI On Friday, August 07, 2026 No comments


Na Mwandishi Wetu, Dodoma
DODOMA: Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatma Almas Nyangasa, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa misitu na uendelezaji wa utalii, akisema hatua hiyo inaongeza ufanisi wa uhifadhi na kuvutia watalii kutembelea vivutio vya Tanzania.

Nyangasa alitoa pongezi hizo jana alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea Viwanja vya Nzuguni, Dodoma, ambapo alipata maelezo kuhusu shughuli na huduma zinazotolewa na TFS kwa mujibu wa majukumu yake ya kisheria.

Akiwa katika banda la TFS, alijionea matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones) katika usimamizi wa misitu pamoja na teknolojia ya Virtual Reality inayowawezesha wananchi na wageni kutembelea vivutio vya utalii kwa njia ya mtandao kabla ya kufika maeneo husika.

Alisema matumizi ya teknolojia hizo ni hatua muhimu ya kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za misitu na kuongeza hamasa ya watalii kutembelea maeneo yenye vivutio mbalimbali, ikiwemo Eneo la Urithi wa Dunia la Michoro ya Miambani ya Kondoa.

Aliongeza kuwa, ubunifu unaoendelea kufanywa na TFS unapaswa kuendelezwa kwa kuwa unarahisisha utoaji wa elimu kwa wananchi na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii wa asili na urithi wa kiutamaduni.
Posted by MROKI On Friday, August 07, 2026 No comments
 


Na. OWM–TAMISEMI, Kilosa
Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa watanufaika na Shilingi Bilioni 1.2 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kisasa la chuma lenye urefu wa mita 30 katika Mto Nyameni, Kata ya Ulaya, mradi  unaotekelezwa na TARURA wenye lengo la kuboresha usafiri na usafirishaji kati ya kata za Zombo, Nyameni na Ulaya.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, Agosti 6, 2026 alipokagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo katika ziara yake ya kikazi ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Kilosa.

"Mhe. Rais anawapenda wananchi wa Zombo, Nyameni na Ulaya. Ameonesha hilo kwa kutoa Bilioni 1.2 kujenga daraja hili litakalomaliza changamoto ya usafiri na usafirishaji iliyosababishwa na kuvunjika kwa daraja la zamani," amesema Prof. Shemdoe.

Amesema ujenzi wa daraja katika barabara ya Zombo–Nyameni–Ulaya umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika Agosti 30, 2026, mara baada ya kuwasili kwa vyuma vya kukamilisha ujenzi, ambavyo vinatarajiwa kuingia nchini kwa njia ya meli.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamkama, amesema ufungaji wa vyuma hivyo utafanywa na wahandisi wa TARURA mkoa wa Morogoro wenye uzoefu wa kazi kama hiyo iliyotekelezwa Mlimba, wilaya ya Kilombero.

Ameongeza kuwa daraja hilo litakuwa na njia mbili za watembea kwa miguu pamoja na uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa zaidi ya tani 40. Pia, daraja la kamba lililopo litahamishiwa eneo jingine lenye uhitaji ili kuongeza huduma ya kuvuka mto Nyameni.

Naye, mkazi wa kata ya Ulaya, Bi. Fatuma Mwalimu Chaubwa, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa daraja hilo na kumpongeza Mbunge wa Jimbo, Mhe. Denis Londo, kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa utekelezaji wa mradi huo.

Daraja hilo linatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa kwenda sokoni, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na elimu, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji, pamoja na kuimarisha usalama wa wananchi wanaovuka mto Nyameni.




Posted by MROKI On Friday, August 07, 2026 No comments

Na WMA - DODOMA.
Wanafunzi wa Klabu ya Vipimo (Vipimo Club)  kutoka Shule ya Msingi Mtemi Mazengo ya jijini Dodoma, wamegeuka walimu kwa siku moja baada ya kumpa elimu ya vipimo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, katika banda la Wakala wa Vipimo  (WMA), kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane, Dodoma.

Leo Agosti 7, 2026, Naibu Waziri Londo alishangazwa na ufasaha wa wanafunzi hao walipomweleza umuhimu wa vipimo sahihi, kuandika kwa usahihi vifungashio katika bidhaa zilizofungashwa pamoja na madhara ya lumbesa.

“Nimefurahishwa sana. Watoto hawa ni mabalozi wazuri wa jamii. Uwekezaji wa WMA katika kizazi kijacho unaleta matokeo,” alisema.

Wanafunzi hao walikuwa katika ziara iliyoratibiwa na Wakala wa Vipimo ikiwa ni sehemu ya mpango wa elimu ya vipimo kwa vitendo.

 Mkakati wa WMA ni  kuwajengea wanafunzi uelewa wa vipimo kwa nadharia na vitendo ambapo  leo wanafunzi hao wa Klabu ya Vipimo ndiyo walikuwa wakitoa huduma zote bandani ikiwemo kuelimisha, kuonyesha matumizi ya vipimo mbalimbali na kujibu maswali ya wananchi.

Naibu Waziri Londo ameonesha kufurahishwa na namna wanafunzi hao walivyojengewa uelewa mpana katika masuala ya vipimo na umahiri wao wa kutoa elimu hiyo kwake na kwa wananchi mbalimbali waliotembelea banda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Wakala wa Vipimo,  Francis Olwero amesema WMA imejipanga kikamilifu kuendeleza klabu za vipimo za wanafunzi ili kuwajengea uelewa wa kivipimo na kurahisisha zaidi usambazaji wa elimu ya vipimo kwa taifa zima wao wakiwa kama mabalozi. 

Amesema wanafunzi hao wamedhihirisha kuwa mbinu hiyo ya kuwaandaa wanafunzi kwa kuwapatia elimu ya vipimo ina tija.

Kiongozi wa Vipimo Club kutoka Mtemi Mazengo, Glory Enock ameishukuru WMA kuanzisha klabu hiyo na kuwapa elimu ya vipimo huku akibainisha kuwa ziara yao NaneNane ililenga pia kusaidia kujenga utamaduni wa “Pima kwa Haki, Pata Faida Halali”

“Tumefundishwa, sasa tunafundisha wazazi na wafanyabiashara kutumia mizani sahihi,” alisema.

Wananchi waliotembelea banda la WMA waliipongeza na kuitaka iendelee kushirikisha shule nyingine kuanzisha Klabu za Vipimo.
Posted by MROKI On Friday, August 07, 2026 No comments

August 06, 2026

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndugu Aggrey Mwanri, akiwa ameambatana na wajumbe wengine wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, amepokelewa Makao Makuu ya CCM, jijini Dodoma, leo tarehe 6 Agosti 2026. Mapokezi hayo yaliyoandaliwa na CCM Mkoa wa Dodoma, yamehudhuriwa na wanachama, makada na viongozi mbalimbali wa CCM, akiwemo Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM (Bara), Mzee Philip Japhet Mangula.







Posted by MROKI On Thursday, August 06, 2026 No comments



Dodoma
Tume ya Madini imeendelea kuimarisha ukaguzi wa migodi nchini ili kuhakikisha shughuli zote za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia sheria, usalama wa wafanyakazi, afya kazini na utunzaji wa mazingira, hatua inayolenga kujenga sekta ya madini yenye tija na endelevu.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mjiolojia na Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini, Paschal Juma, amesema Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira chini ya Mkurugenzi wake, Mhandisi Hamisi Kamando, ina jukumu la kusimamia na kufuatilia shughuli zote za uchimbaji ili kuhakikisha zinazingatia Sheria ya Madini, kanuni, sera na miongozo mbalimbali ya sekta hiyo.

Amesema Kurugenzi hiyo hufanya ukaguzi wa usalama na afya mahali pa kazi, hufuatilia utekelezaji wa mipango ya usimamizi wa mazingira, urejeshaji wa maeneo yaliyochimbwa pamoja na mipango ya ufungaji migodi kwa kuzingatia viwango vinavyolinda mazingira na kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, amesema Kurugenzi hiyo hupitia na kuidhinisha mipango ya uchimbaji, taarifa za utendaji wa migodi na usanifu wa miundombinu ya migodi, huku ikisimamia matumizi salama ya baruti kwa mujibu wa Sheria ya Baruti, Sura ya 45, na kanuni zake.

Paschal amesema Tume ya Madini inatumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kutoa elimu kwa wananchi, wachimbaji na wadau wa sekta kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga, mbinu salama za uchimbaji, utunzaji wa mazingira pamoja na uhifadhi na matumizi salama ya baruti.

Amesisitiza kuwa elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wadau, kuimarisha uzingatiaji wa sheria na viwango vya usalama, kupunguza ajali migodini na kuendeleza sekta ya madini inayochangia ukuaji wa uchumi wa taifa kwa njia endelevu.
Posted by MROKI On Thursday, August 06, 2026 No comments

August 05, 2026






Dodoma
Kampuni ya CDICD Group Limited imeendelea kuimarisha mnyororo wa thamani katika Sekta ya Madini kwa kuchakata madini ya black granite na kuzalisha bidhaa mbalimbali za ujenzi zinazouzwa katika soko la ndani na nje ya nchi, hatua inayochochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira na kukuza mauzo ya bidhaa zenye thamani.

Akizungumza jijini Dodoma kwenye Maonesho ya Nane Nane, Meneja wa CDICD, Shija Shimba, amesema kampuni hiyo imewekeza katika kiwanda cha kisasa cha uchakataji wa black granite kinachobadilisha mawe ghafi kuwa bidhaa mbalimbali zikiwemo countertops za majiko, paving stones, slabs za ujenzi na headstones zinazotumika katika makaburi.

Amesema shughuli za uchimbaji na uchakataji zinafanyika katika kijiji cha Manyemba, wilayani Chamwino mkoani Dodoma, ambapo kampuni imejikita katika kuongeza thamani ya madini kabla ya kuyapeleka sokoni.

Kwa mujibu wa Shimba, uwekezaji huo umeiwezesha CDICD kupanua masoko yake ndani na nje ya Tanzania. Mbali na kuuza bidhaa zilizochakatwa nchini, kampuni pia husafirisha black granite blocks kwenda China na nchi nyingine kwa ajili ya uchakataji zaidi katika viwanda vya nchi hizo.

Amesema kampuni huzalisha wastani wa tani 270 za black granite kwa wiki, huku bidhaa zake zikisambazwa kupitia vituo vya mauzo vilivyopo Dodoma na Victoria, Kinondoni jijini Dar es Salaam, pamoja na mikoa mbalimbali nchini.

Shimba amesema uwekezaji huo pia umefungua fursa za ajira kwa vijana kati ya 90 na 100 wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo uendeshaji wa mitambo, udereva, uchomeleaji na shughuli nyingine za uzalishaji.

Ameongeza kuwa CDICD ilianza shughuli zake mwaka 2014 na imeendelea kupanua shughuli za uchimbaji wa black granite katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chamwino, kabla ya kuhamishia shughuli zake Manyemba, ambako inaendelea na uzalishaji na uchakataji wa madini hayo kwa sasa.
Posted by MROKI On Wednesday, August 05, 2026 No comments






Na: Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Mary Chatanda, ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Songwe kwa kufanikisha miradi mingi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi.

Chatanda ametoa pongezi hizo, Agosti 3, wilayani Songwe, katika ziara maalum ya viongozi wa UWT Taifa kukagua shughuli mbalimbali mkoani Songwe.

Amesema kuwa, serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imejikita katika kutatua kero za wananchi kupitia miradi ya maendeleo.

"Nimejionea kwa macho kazi nzuri zimefanyika Songwe, mmegusa maisha ya wananchi, fedha za mikopo ya asilimia kumi zinafika kwa vijana, wanawake na wenye mahitaji maalum, hakika Songwe mmeonyesha mfano mzuri wa kuigwa," amesema Chatanda.

Akiwa Songwe, Chatanda na wajumbe wa Jumuiya hiyo, walipata fursa ya kutembelea kikundi cha wanawake cha 'Mama ni Nguzo' kinachojishughulisha na uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu. Kikundi hiki kimenufaika na mkopo wa shilingi milioni 100.

Aidha, walitembelea kikundi cha waponda kokoto Saza ambacho kimeonyesha uaminifu wa kurejesha mkopo wote wa shilingi milioni 23 waliokopeshwa awali huku uongozi wa Halmashauri ukijipanga kuwakopesha gari aina ya fuso ili kubeba mawe na hatimaye waweze kukuza mradi wao.

Katika hatua nyingine, wajumbe hao walitembelea mradi wa ujenzi wa Soko la Madini la CPA. Cecilia Kavishe, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 99.

Sanjari na hilo, wametembelea mradi wa ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT wilaya, huku wakipongeza hatua nzuri iliyofikiwa.

Ziara hiyo ya siku tatu mkoani humo ni mahsusi kwa ajili ya kukagua uhai wa Chama, Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025-2030. 

Vilevile, kufanya mikutano ya ndani, kuongea na wanachama na wananchi kuwapongeza kwa kuendelea kuwa na imani na Chama hicho katika kuwatumikia.

Katika ziara hiyo, Chatanda ameambatana na viongozi wengine wakiwemo Ellen Bogohe (MNEC), Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa Flora Magambe na Mbunge wa Viti Maalum, Dk. Catherine Joakim.
Posted by MROKI On Wednesday, August 05, 2026 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo