Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kupitia programu ya Polisi Jamii limeendelea kuonesha mshikamano na jamii baada ya kuwatembelea wakina mama waliojifungua, watoto na wagonjwa mbalimbali katika kituo cha afya cha Tnduma kilichopo Wilaya ya Momba, ambapo walikabidhi mahitaji mbalimbali na kuwasaidia kulipia gharama ndogo za matibabu. Hatua hiyo imelenga kuimarisha mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi pamoja na kuhamasisha ushirikiano katika kudumisha amani, usalama na malezi bora ya watoto.
Akiongoza ziara hiyo Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi Maria Kway, tarehe 04 Agosti 2026, alisema kuwa malezi bora ndiyo msingi wa kujenga taifa lenye maadili na usalama, hivyo aliwataka wakina mama kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi, uangalizi unaostahili na kulindwa dhidi ya aina zote za ukatili, ikiwemo unyanyasaji wa kimwili, kisaikolojia na kijinsia.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu na kulinda ustawi wa jamii.
Mwisho wananchi wamehimizwa kutumia elimu hiyo kwa kuwalea watoto katika mazingira salama, kuripoti matukio ya ukatili na uhalifu kwa wakati kwenye vyombo vya dola, pamoja na kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kudumisha amani, usalama na maendeleo ya jamii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.











0 comments:
Post a Comment