Dar es Salaam,
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga, leo amezindua Kikosi Kazi cha Uzalishaji (Manufacturing Working Group) chini ya Chemba ya Wafanyabiashara wa Marekani Tanzania (AMCHAM Tanzania), ikiwa ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza uzalishaji, uwekezaji na mauzo ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Uzinduzi huo uliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Mbwasi, ambaye aliwasilisha ujumbe wa Serikali na kusisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazoathiri ushindani wa bidhaa za Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bw. Mbwasi amesema kuanzishwa kwa Kikosi Kazi hicho kunalenga kuwaleta pamoja wazalishaji, wawekezaji na Serikali, ili kujadili kwa utaratibu changamoto zinazokabili sekta ya uzalishaji na kuibua suluhisho zinazoweza kuongeza uzalishaji, uwekezaji, ajira na mauzo ya nje.
Amesema Serikali inahimiza wazalishaji wa Tanzania kutumia kikamilifu fursa ya soko la Marekani kupitia African Growth and Opportunity Act (AGOA), hususan katika kipindi kilichosalia cha mpango huo, kwa kuongeza idadi ya bidhaa na makampuni ya Tanzania yanayofikia soko hilo.
“Tunaendelea kuhimiza wazalishaji kutumia fursa zilizopo katika masoko ya kimataifa, ikiwemo soko la Marekani kupitia AGOA, ili kuongeza mauzo ya nje na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini,” amesema Bw. Mbwasi.
Ameongeza kuwa takwimu za mwaka 2025 zinaonesha kuwa shughuli za uzalishaji zimeendelea kukua ambapo amesema Serikali ina dhamira ya kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wazalishaji na wawekezaji, ikiwemo kuboresha miundombinu, sera na mifumo ya biashara, pamoja na kushughulikia changamoto zinazoweza kupunguza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Kikosi Kazi hicho kuwa jukwaa la mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Serikali na sekta binafsi, ambapo changamoto zitawasilishwa kwa ushahidi, kupatiwa taasisi zinazohusika na kufuatiliwa hadi kupata ufumbuzi.
Katika uzinduzi huo, wawakilishi wa sekta binafsi waliwasilisha changamoto mbalimbali zinazokabili wazalishaji, zikiwemo gharama na upatikanaji wa nishati, bidhaa bandia na biashara isiyo rasmi, masuala ya kodi, ushuru na tozo, upatikanaji wa ardhi ya viwanda, changamoto katika mnyororo wa thamani wa nguo, pamba na malighafi, pamoja na upatikanaji wa masoko ya nje.
Kwa upande wake, Serikali imewahimiza wadau kuwasilisha mapendekezo yenye ushahidi, vipaumbele na suluhisho mahsusi, ili kurahisisha hatua za Serikali katika kushughulikia changamoto hizo.
Kikosi Kazi cha AMCHAM Manufacturing Working Group kinajumuisha wawakilishi wa wazalishaji, wawekezaji na wadau mbalimbali wa sekta ya uzalishaji, kwa lengo la kuimarisha ushindani wa viwanda vya Tanzania na kukuza uwekezaji pamoja na biashara kati ya Tanzania na Marekani.
Uzinduzi huo unatarajiwa kuwa mwanzo wa ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Serikali na sekta binafsi, hususan katika kuongeza uzalishaji wa ndani, thamani ya bidhaa, ajira na mauzo ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

















0 comments:
Post a Comment