Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), ameipongeza kampuni ya Simba Beverages Limited kwa uwekezaji wa takribani Shilingi bilioni 28 katika sekta ya viwanda nchini, akieleza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uchumi kupitia uzalishaji wa bidhaa nchini, kuongeza ajira na kupanua wigo wa mapato ya Serikali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho kilichopo katika eneo la viwanda la Zegereni, Kibaha, mkoani Pwani, Waziri Kapinga amesema,Serikali inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ya kufungua viwanda vipya nchini na kuvutia uwekezaji wa viwanda vipya ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.
Amesema sekta ya vinywaji baridi ni miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi wa viwanda kutokana na mchango wake katika uzalishaji, ajira na uwekezaji, pamoja na kuunganisha shughuli nyingine za kiuchumi zikiwemo kilimo, usindikaji na usambazaji wa bidhaa. Amesisitiza kuwa maendeleo ya sekta hiyo yanapaswa kwenda sambamba na matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini ili kuongeza thamani ya rasilimali za ndani na kunufaisha wazalishaji wa Kitanzania.
Waziri Kapinga ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku akiwataka wawekezaji kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinazingatia sheria, kanuni na viwango vya ubora na usalama. Amesisitiza pia umuhimu wa kulinda wafanyakazi na kuboresha mazingira ya kazi ili kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Fadhili Nkurlu, amesema idadi ya viwanda katika Mkoa wa Pwani imeongezeka kutoka viwanda 387 katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi kufikia viwanda 768 kufikia Septemba 2026. Alieleza kuwa viwanda hivyo vinajumuisha viwanda vikubwa 33, vya kati 33, vidogo 248 na vidogo zaidi 454.
Ameongeza kuwa viwanda vikubwa na vya kati 38 vilikuwa katika hatua za ujenzi ila sasa vimekamilika, vikiwemo viwanda vikubwa 27 na vya kati 11, huku viwanda vingine 99 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi na maandalizi. Aidha, alisema viwanda 35 vilivyopo katika maeneo ya uwekezaji mkoani humo vimechangia kuzalisha ajira za moja kwa moja 2,357 na ajira nyingine zisizo rasmi 6,062 zinazotokana na shughuli za kiuchumi zinazohusiana na viwanda hivyo.
Mhe. Nkurlu amesema Mkoa wa Pwani unaendelea kuweka kipaumbele katika kuvutia uwekezaji wa viwanda vipya, kuongeza ajira kwa vijana, kuhamasisha matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini na kusimamia ubora na usalama wa bidhaa zinazozalishwa. Ameeleza kuwa uwekezaji wa Simba Beverages Limited ni sehemu ya juhudi za kujenga uchumi imara na wenye ushindani kupitia sekta ya viwanda.
Kwa upande wake, Afisa mkuu wa fedha Surya Murthy, Afisa Mkuu wa Fedha (CFO) wa Simba Beverages Limited, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na viongozi wa Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Kibaha kwa ushirikiano wao katika kuwezesha uwekezaji huo. Ameeleza kuwa uzinduzi wa kiwanda hicho ni hatua muhimu katika kuendeleza shughuli za uzalishaji nchini, kuongeza thamani ya bidhaa na kuimarisha minyororo ya ugavi, huku kampuni ikiendelea kutekeleza dhamira yake kupitia kaulimbiu ya “Imezaliwa Tanzania, Inatumikia Afrika.”
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa katika hafla hiyo, Simba Beverages Limited imewekeza katika uzalishaji wa vinywaji baridi vyenye gesi pamoja na vifungashio vya plastiki. Mitambo ya kiwanda hicho ina uwezo wa kuzalisha chupa 12,000 za vinywaji baridi kwa saa, huku kampuni ikitarajia kuzalisha ajira za moja kwa moja 100 na ajira nyingine 200 zisizo za moja kwa moja kadri shughuli zake zitakavyopanuka.
Aidha, kampuni hiyo imeeleza kuwa inatumia zaidi ya asilimia 90 ya malighafi zinazopatikana nchini, hatua inayochangia kuimarisha mnyororo wa thamani wa uzalishaji wa ndani. Kampuni pia inalenga kuongeza mauzo yake hadi Sh bilioni 15.4 ifikapo mwaka 2027 na Sh bilioni 33 ifikapo mwaka 2030, kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa katika uzinduzi huo.
Uwekezaji wa Simba Beverages Limited unaonesha nafasi ya sekta binafsi katika kuendeleza viwanda nchini, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi unaotegemea uzalishaji wa bidhaa na matumizi ya rasilimali zinazopatikana ndani ya nchi. Serikali inaendelea kuhimiza wawekezaji kutumia malighafi za ndani, kuongeza thamani ya bidhaa, kuhamisha teknolojia na kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya sekta ya viwanda.















0 comments:
Post a Comment