Nafasi Ya Matangazo

October 26, 2026


Na M
wandishi Maalum
Makocha na mabondia wa ngumi za kulipwa nchini wametaka uchunguzi wa afya kupewa kipaumbele kwa wanamichezo hao ili kubaini mapema magonjwa yanayoweza kuhatarisha maisha yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kambi maalumu ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo wa ngumi za kulipwa Tanzania inayofanyika katika viwanja vya Mafia Boxing Sports Promotion vilivyopo Magomeni jijini Dar es Salaam wamesema huduma hizo ni muhimu katika kuwasaidia mabondia kufahamu hali za afya zao.
Bondia wa zamani wa ngumi za kulipwa nchini Said Yazidu alisema uchunguzi wa afya ni muhimu kwa mabondia kwa sababu kufanya mazoezi mara kwa mara hakumaanishi kuwa wanamichezo hawana changamoto za kiafya.
“Ni jambo zuri sana kwa wachezaji kufahamu afya zao kwa sababu mchezaji anaweza kufanya mazoezi kila siku kumbe ana matatizo ya kiafya ambayo hayajui, naomba zoezi hili lisiwe la muda tu bali liwe endelevu na ikiwezekana lifikishwe katika mikoa mingine ili mabondia wote wapimwe moyo”, alisema Yazidu.
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Frank Shagembe aliwahimiza mabondia ambao hawajapata nafasi ya kupima afya zao kujitokeza kwa wingi wanapopata fursa hiyo akieleza kuwa uchunguzi wa afya unaweza kusaidia kubaini matatizo ambayo hayawezi kutambuliwa kwa kutegemea hali ya mwili pekee.
Kwa upande wake kocha na refa wa ngumi za kulipwa Tanzania Kondo Nassoro alisema amefurahishwa na mwitikio wa mabondia waliojitokeza kufanya uchunguzi wa afya na kuwasisitiza mabondia  umuhimu wa kupima afya zao kabla ya kushiriki katika mchezo huo unaohitaji maandalizi na uangalizi wa karibu wa kiafya.
“Ni muhimu kabla mabondia hawajaingia ulingoni kupima vipimo vya moyo, wamekuwa wakishiriki katika michezo bila kupima afya zao hivo JKCI imetupa elimu ambayo tutaifanyia kazi kuwalinda wanamichezo wetu”, alisema Nassoro.
Posted by MROKI On Monday, October 26, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo