Nafasi Ya Matangazo

September 29, 2026

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moris Budotela akimsomea majibu Meneja Uhusiano kwa Umma Hifadhi ya Ngorongoro Hamisi Dambaya wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya inayofanyika katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali (CEO Forum 2026) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) jijini Arusha.
Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Glory Mtui akichukua sampuli ya damu wakati wa kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali (CEO Forum 2026) kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa wa Mikutano (AICC) jijini Arusha.
**********
Na. Mwandishi Maalum - Arusha
Viongozi na watendaji wakuu wa taasisi za umma nchini wanufaika na huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali (CEO Forum 2026).
 
Huduma hizo zinatolewa katika kambi maalumu inaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) ambapo washiriki wa kikao kazi hicho wanafanyiwa uchunguzi wa utendaji kazi wa moyo, vipimo vya figo, wingi wa mafuta kwenye damu na wingi wa sukari kwenye damu sambamba na kupewa elimu ya kujua namba zao.
 
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI-ALMC) Farida Abdallah alisema kambi huduma za uchunguzi wa afya kwa viongozi hao ni za muhimu kwani wakiwa na afya bora wataweza kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuleta maendeleo ya nchi.
 
“Tumepata fursa ya kuwahudumia wenyeviti wa bodi, wakurugenzi wa taasisi, mashirika ya umma na mashirika ya kiserikali nchini, viongozi hao wameendelea kufika katika kitengo cha uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwaajili ya kujua namba zao”, alisema Dkt. Farida.
 
Dkt. Farida alisema sambamba na uchunguzi wa afya ya moyo wataalamu wa JKCI wameendelea kutoa elimu ya lishe bora kwa viongozi hao ili waweze kufahamu viashiria vya magonjwa ya moyo na namna ya kukabiliana na magonjwa hayo.
 
Kwa upande wake Meneja Uhusiano kwa Umma wa Hifadhi ya Ngorongoro Hamisi Dambaya alisema amefurahishwa na huduma aliyoipata kutoka kwa wataalamu wa JKCI kwani uchunguzi aliofanyiwa umemsaidia kupata taarifa sahihi kuhusu afya yake.
 
“Nimefanyiwa uchunguzi wa afya na kuhudumiwa vizuri, kikubwa nimefanyiwa vipimo vya moyo na kupata elimu ya kutosha kuhusu magonjwa hayo.  Watanzania wana kila sababu ya kufika katika Taasisi hii na kuchunguza afya zao”, alisema Dambaya.
 
Kambi hiyo inaendelea kutoa huduma za uchunguzi na elimu ya afya kwa washiriki wa mkutano wa CEO Forum 2026 ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kinga na utambuzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza.
Posted by MROKI On Tuesday, September 29, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo