Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza
Novemba 04, 2026 kuwa siku ya uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino,
Mkoa wa Dodoma, pamoja na Madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ramadhani Kailima, imesema uchaguzi huo
unafanyika kufuatia kuwepo kwa nafasi wazi za uongozi katika maeneo ya
uchaguzi.
“Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea
taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu
kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Chamwino, Halmashauri ya
Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma,” ilisema taarifa hiyo.
Nafasi hiyo imetokea baada ya Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe.
Deogratius John Ndejembi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uteuzi wake ulifanyika tarehe 26 Agosti, 2026
na kuthibitishwa na Bunge tarehe 28 Agosti, 2026.
Aidha, Kailima kupitia taarifa hiyo amesema
Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa
Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343 ilipokea taarifa kutoka kwa Waziri
mwenye dhamana juu ya uwepo wa nafasi wazi za madiwani 11 kwa Tanzania bara.
“Tumepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye
dhamana ya Serikali za Mitaa kuhusu uwepo wa nafasi wazi za madiwani 11 kwa
Tanzania Bara. Nafasi hizo wazi zilitokana na vifo vya madiwani nane (08) kwa
nyakati tofauti na madiwani watatu (03) kujiuzulu,”taarifa ilisema.
Tume imesema kuwa fomu za uteuzi kwa wagombea wa Ubunge Chamwino na Udiwani katika kata 11 zitatolewa kuanzia tarehe 7 hadi 13 Oktoba 2026, huku zoezi la uteuzi wa wagombea likifanyika tarehe 13 Oktoba 2026.







0 comments:
Post a Comment