Nafasi Ya Matangazo

September 13, 2026






Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Babati ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Remidius Mwema amefunga machinjio ya kuku katika Soko Kuu la Babati kwa muda wa siku 14, baada ya kubaini hali isiyoridhisha ya usafi katika eneo hilo.
Mwema ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya usafi katika soko hilo, akiwa ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Usalama Wilaya ya Babati.

Ameagiza ndani ya kipindi hicho eneo la machinjio lifanyiwe usafi na marekebisho ya kina, ikiwemo kuwekwa mfumo mzuri wa maji, ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama kwa wafanyabiashara na wananchi. Amesisitiza kuwa usafi unatakiwa kuzingatiwa kila siku, bila kusubiri viongozi kufika kukagua.

"Usafi sio mpaka Mkuu wa Wilaya afike, usafi uzingatiwe siku zote," amesema Mwema.

Wakati machinjio hayo yakifungwa kwa siku 14 ( tangu tarehe 11 Sept,2026) kwa ajili ya marekebisho,shughuli za uchinjaji wa kuku zitaendelea katika Soko la Silent.

Katika hatua nyingine  Mhe.Mwema  ameagiza uchafu katika kizimba cha Soko Kuu la Halmashauri ya Mji wa Babati kuondolewa ndani ya saa 24 na kwamba wakati wote taka hizo kuondolewa kwa wakati, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia usafi kwa ajili ya afya za wafanyabiashara na wateja na kwamba usafi unatakiwa kuwa hulka ya kila mmoja. 

Aidha, amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El-Niño zinazotarajiwa, kama ilivyoelezwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa kuhakikisha maeneo ya biashara na mazingira kwa ujumla yanakuwa safi.

Mhe. Mwema anaendelea na utekelezaji wa majukumu mbalimbali Wilayani Babati ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Wilaya hiyo inakuwa safi muda wote.
Posted by MROKI On Sunday, September 13, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo