Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya I. Samamba,
amewaelekeza wachimbaji wadogo, wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi nchini
kuchukua hatua za haraka kujiandaa na kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajiwa
kunyesha kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huu, ikiwemo kuongeza kasi ya
ukaguzi wa maeneo ya uchimbaji (maduara), mabwawa ya kuhifadhia tope sumu na
kuimarisha mipango ya dharura.
Eng. Samamba ametoa maelekezo hayo leo, Septemba 28, 2026,
wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wakati akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo
wa madini kuhusu maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua hizo, akisema
tahadhari hiyo inazingatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
kuhusu uwezekano wa mvua kubwa kuliko wastani katika kipindi hicho.
Amesema mvua hizo zinaweza kuathiri shughuli za uchimbaji na
kusababisha madhara kwa watu, mazingira, miundombinu na uzalishaji iwapo hatua
stahiki za tahadhari hazitachukuliwa mapema.
“Wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi wanapaswa
kuboresha taratibu za usalama ili ziakisi hali ya mvua kubwa, kuongeza ukaguzi
wa maduara na mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, pamoja na kuhakikisha kila mgodi
una mpango wa dharura unaoeleweka na kutekelezeka,” amesema.
Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo
katika maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa Taifa, hivyo maandalizi hayo
ni muhimu ili shughuli za uchimbaji ziendelee kwa usalama na tija.
Eng. Samamba amesema miongoni mwa hatari zinazoweza
kujitokeza wakati wa mvua kubwa ni kuporomoka kwa maduara na kuta za migodi
kutokana na miamba kulainika na kupoteza uimara, mafuriko ndani ya migodi,
kudhoofika kwa mihimili inayoshikilia miamba, pamoja na kufurika au kudhoofika
kwa mabwawa ya kuhifadhia tope sumu.
Amesema pia mazingira yasiyo safi na maji yaliyotuama
yanaweza kuongeza hatari za kiafya kwa wachimbaji na jamii zinazozunguka maeneo
ya migodi.
Kwa mujibu wa Eng. Samamba, wamiliki, mameneja na wakaguzi
wa migodi wanapaswa kuhakikisha hakuna mchimbaji anayeingia au kuendelea
kufanya kazi chini ya ardhi wakati wa mvua kubwa au mara baada ya mvua kukatika
iwapo hali ya eneo husika si salama.
Aidha, amewaagiza kuhakikisha maduara yanakaguliwa kila siku
kabla ya kazi kuanza na sehemu zote dhaifu kuimarishwa kwa kutumia mihimili
imara ya miti au chuma kulingana na mahitaji ya kiusalama.
Amesema mifereji inayozunguka midomo ya maduara na maeneo ya
kazi inapaswa kujengwa na kusafishwa mara kwa mara, huku matuta, kingo, mawe na
vifusi vikitumika katika maeneo yanayohitaji ulinzi ili kuzuia maji ya juu ya
ardhi kuingia kwenye migodi.
“Kila mgodi unapaswa kuwa na pampu za kuvuta maji pamoja na
mafuta ya kutosha ili kuwezesha kuchukua hatua za haraka endapo maji yatajaa
kwenye mashimo,” amesema.
Kuhusu mabwawa ya kuhifadhia tope sumu (TSF), Eng. Samamba
amewataka waendeshaji wa migodi kuhakikisha mabwawa hayo yana nafasi na uimara
wa kutosha kupokea ongezeko la maji wakati wa mvua, huku ukaguzi wa kingo,
mifereji, kiwango cha maji, dalili za kuvuja na mmomonyoko ukifanyika kwa
wakati.
Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuzuia madhara kwa
binadamu, wanyama, mimea na mazingira.
Eng. Samamba pia amesisitiza kuzingatiwa kwa taratibu za
usalama wakati wa ulipuaji, akielekeza kuhakikisha watu wote wanatoka katika
eneo la tukio na kufika umbali salama kabla ya ulipuaji, na kurejea baada ya
muda uliowekwa kwa mujibu wa taratibu za usalama.
Amesema zamu za wachimbaji zinapaswa kusimamiwa kwa
kuzingatia uwezo wa watendaji ili kuzuia uchovu unaoweza kuongeza uwezekano wa
kutokea kwa ajali.
Aidha, amewaelekeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kusimamia
utekelezaji wa maelekezo hayo pamoja na Kanuni za Madini (Usalama, Afya na
Utunzaji wa Mazingira) za mwaka 2010, na kuchukua hatua stahiki pale ukiukwaji
unapobainika.
Amesema ukaguzi wa mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, maeneo
ya kuhifadhi miamba taka na miundombinu mingine ya migodi unapaswa kuongezwa
kabla na wakati wa mvua, huku kasoro zinazoweza kuhatarisha usalama
zikishughulikiwa mara moja.
Amesisitiza kuwa kila mgodi unapaswa kuwa na mpango wa
dharura unaoeleweka kwa watendaji, unaoainisha namna ya kutoa taarifa, kuokoa
watu, kusimamisha shughuli pale inapobidi na kuwasiliana na mamlaka husika.
Aidha, amewataka viongozi wa vyama vya wachimbaji wa madini
kutumia mitandao yao kutoa elimu kwa wanachama na kuwataka wachimbaji
kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuzitumia katika kupanga shughuli
zao za kila siku.
“Kaeni na wachimbaji, wasikilizeni hoja zao na mzitatue kwa
kushirikiana. Tusifanye kazi kwa maelekezo pekee, bali kwa ushirikiano,”
amesema.
Amesema usalama haupaswi kuchukuliwa kuwa gharama
inayopunguza uzalishaji, kwa kuwa ajali inaweza kusababisha kusimama kwa
shughuli za uchimbaji, kuharibu miundombinu, kuathiri mazingira na jamii na
kusababisha kupoteza maisha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wakaguzi wa Migodi
Tanzania, Shija Mussa, amesema wachimbaji wadogo wanakabiliwa na changamoto ya
maji kujaa kwenye mashimo wakati wa uchimbaji na kuiomba Serikali kusaidia
upatikanaji wa mitambo mikubwa ya kunyonya maji (heavy-duty pumps) pamoja na
vifaa vingine vya dharura.
Amesema mitambo hiyo inapaswa kuwekwa katika maeneo ya
kimkakati ili iweze kutumika kwa haraka wakati wa dharura.
Awali, Mkurugenzi wa Leseni kutoka Tume ya Madini, Eng.
Aziza Swedi, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng.
Ramadhani Lwamo, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwapa wachimbaji wadogo elimu
na uzoefu kuhusu namna ya kuchukua tahadhari dhidi ya athari za mvua kubwa.
Amesema Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini
imeamua kuchukua hatua mapema baada ya kutolewa kwa tahadhari ya mvua, ambapo
wataalamu wanawasilisha mada kuhusu usalama wa migodi, mabwawa ya kuhifadhia
tope sumu, maeneo ya kuhifadhi miamba taka, udhibiti wa mafuriko na mipango ya
dharura.
Eng. Swedi amesema mafanikio ya mafunzo hayo yataonekana
kupitia utekelezaji wa vitendo katika maeneo ya uchimbaji, akiwataka washiriki
kurejea katika maeneo yao ya kazi, kufanya tathmini, kubaini maeneo hatarishi
na kurekebisha kasoro kabla ya madhara kutokea.



.jpeg)
.jpeg)



.jpeg)



0 comments:
Post a Comment