DODOMA — Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeonesha namna sekta ya misitu na nyuki inavyoweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira, kipato na ukuaji wa uchumi kupitia mnyororo wa thamani wa mazao yake.
Hayo yamebainika katika Maonesho ya Nane Nane 2026 yanayoendelea Dodoma, baada ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT, Brigedia Jenerali Shija Lupi, kutembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii na kujionea ubunifu unaofanywa na TFS katika kuibua fursa hizo.
Brigedia Jenerali Lupi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Nane Nane Kitaifa upande wa JKT, alielezwa kuhusu safari ya mazao ya misitu na nyuki kutoka uzalishaji, uchakataji, uongezaji thamani hadi kufikia masoko ya ndani na nje.
Amesema ubunifu huo unaonesha kuwa rasilimali za misitu zinaweza kutumika zaidi ya uhifadhi, bali pia kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
“Nimeona mnyororo mzima wa thamani unaoonesha namna mazao ya misitu na nyuki yanavyoweza kuongeza ajira, kipato na kuchangia uhifadhi wa mazingira,” amesema.
Katika banda hilo, Brigedia Jenerali Lupi pia alishuhudia huduma ya tiba nyuki (Apitherapy), inayotumia bidhaa za nyuki pamoja na kudungishwa na nyuki chini ya uangalizi wa wataalamu.
Alielezwa kuwa tiba hiyo imekuwa ikitumika kusaidia kupunguza baadhi ya maumivu ya viungo na changamoto nyingine zinazohusishwa na afya, huku wataalamu wakisisitiza matumizi sahihi na salama ya huduma hiyo.













0 comments:
Post a Comment