Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Mary Chatanda, amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, ni muumini mzuri wa kutumia meza ya mazungumzo kujadili na kufikia muafaka wa masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Chatanda ameyasema hayo, kufuatia kumalizika kwa mazungumzo baina ya Rais Dk. Samia na viongozi wa vyama 18 vya siasa, Julai 30, 2026, Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
Chatanda amesema, mazungumzo ya pamoja baina ya serikali na viongozi wa vyama vya siasa ni muhimu katika kuimarisha umoja na mshikamano.
"Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni muumini mkubwa wa meza ya mazungumzo. Katika meza hiyo, mengi yanajadiliwa kuliko kutumia mitandao ya kijamii kulalamika. Kimsingi, serikali imepokea ushauri kutoka kwa viongozi wa vyama vya siasa, na hapa kama taifa tunapata mawazo chanya ya kujenga na hivyo tunaimarisha umoja na mshikamano wetu," amesema.
Katika hatua nyingine, Chatanda amesema, Rais Dk. Samia amejipambanua kuwa kinara wa kusikiliza hoja kutoka kwa wadau mbalimbali hata wenye itikadi tofauti za kisiasa ili tu kufikia azma ya kujenga taifa letu.
"Linapokuja suala la ujenzi wa taifa, Rais wetu Dk. Samia anasikilizia kila mtu kwani anaamini taifa hujengwa kwa mawazo jumuishi," amesisitiza.
Aidha, katika mazungumzo hayo na viongozi wa vyama vya siasa, Rais Dk. Samia alieleza namna serikali inavyohimiza maridhiano ya kisiasa ili kufanikisha mipango mingi ya kimaendeleo.
Sambamba na hilo, Rais alieleza mchakato ya maridhiano visiwani Zanzibar huku aliwajulisha viongozi hao maandalizi ya mchakato wa maridhiano kuelekea mapitio ya katiba.
Kwa upande wa viongozi wa vyama vya siasa, walitumia mkutano huo kushauri masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ambayo serikali inapaswa kufanyia kazi ili kukuza maendeleo na ustawi wa wananchi.











0 comments:
Post a Comment