Nafasi Ya Matangazo

June 11, 2026




Dodoma
Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Marvel Gold ya Australia, Timothy Strong, jijini Dodoma ambapo amepokea taarifa kuhusu maendeleo ya hatua za awali za mradi wa mgodi wa dhahabu unaoendelezwa katika Wilaya ya Hanang’, Mkoa wa Manyara.

Akizungumza katika kikao hicho, Strong amesema kuwa kampuni hiyo inaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi yaliyowezesha kufanikisha uwekezaji huo.

Ameeleza kuwa baada ya kukamilisha hatua ya awali ya utafiti kwa kutumia teknolojia ya ndege nyuki (drones), kampuni imeingia katika hatua ya pili ya uchorongaji, huku awamu ya kwanza ya shughuli hizo ikitarajiwa kukamilika mwishoni mwa Julai 2026.

“Shabaha yetu ni kuanza mara moja shughuli za uchimbaji pindi ambapo taratibu zote zitakapokamilika kwa mafanikio,” amesema Strong.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira bora na kuvutia uwekezaji unaochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Waziri Mavunde ameipongeza Kampuni ya Marvel Gold kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo mpya wa dhahabu katika Mkoa wa Manyara, akieleza kuwa kukamilika kwake kutachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Wilaya ya Hanang’, Mkoa wa Manyara na Tanzania kwa ujumla.

“Ni matarajio yetu kwamba mradi huu utakuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Hanang’ na Mkoa wa Manyara, sambamba na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa. Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania,” amesema Waziri Mavunde.
Posted by MROKI On Thursday, June 11, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo