Nafasi Ya Matangazo

June 17, 2026

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limehimiza ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi, taasisi mbalimbali na wananchi katika juhudi za kulinda na kuhifadhi mazingira nchini. 

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha rasilimali za asili zinaendelea kutumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho huku zikihifadhiwa kwa uendelevu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Mawasiliano wa NEMC, Martha Kawishe, amesema kuwa mafanikio ya uhifadhi wa mazingira yanategemea ushiriki wa wadau wote. 

Amesema changamoto za mazingira, ikiwemo uchafuzi wa mazingira, utupaji holela wa taka na shughuli zinazoweza kuharibu ikolojia, zinahitaji juhudi za pamoja ili kudhibitiwa kwa ufanisi.

Kawishe amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini vitendo au shughuli zinazohatarisha mazingira katika maeneo yao. 

Amesema ushirikiano huo utasaidia mamlaka kuchukua hatua kwa wakati na kuzuia madhara yanayoweza kuathiri afya za wananchi, uchumi na mazingira kwa ujumla. 

Aidha, NEMC itaendelea kutoa elimu kwa umma na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira nchini.

Katika hatua nyingine, Kawishe amesema NEMC imekuwa ikipokea taarifa kuhusu baadhi ya watu wasio waaminifu wanaojitambulisha kwa uongo kuwa wakaguzi wa mazingira kutoka NEMC kwa lengo la kuwalaghai wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji. 

Amesema watu hao wamekuwa wakijaribu kutumia jina la taasisi hiyo kufanya ukaguzi usio rasmi au kudai fedha kinyume na taratibu zilizowekwa.

Kutokana na hali hiyo, amewashauri wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kuwa makini wanapokutana na watu wanaodai kuwa maafisa wa NEMC. 

Amesema kabla ya kuruhusu ukaguzi wowote, ni muhimu kuomba kuonyeshwa kitambulisho cha kazi, kitambulisho maalumu cha ukaguzi wa mazingira pamoja na nyaraka rasmi zinazompa mhusika mamlaka ya kufanya ukaguzi huo. 

NEMC imeeleza kuwa tahadhari hiyo itasaidia kudhibiti vitendo vya udanganyifu na kulinda maslahi ya wananchi pamoja na wawekezaji nchini.

Posted by MROKI On Wednesday, June 17, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo