Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa kwenye picha na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Perseus Mining Limited Bw. Rick Menell mara baada ya mazungumzo yao, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 06 Mei, 2026. Perseus Mining Limited ni mwekezaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Nyanzaga, Wilayani Sengerema, Mkoani Mwanza kupitia Kampuni ya Sotta Minining Corporation Limited, inayomilikiwa kwa ubia na Serikali ya Tanzania.
***********
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo
amekutana na kuzungumza na uongozi wa Kampuni ya Perseus Mining Limited, Ikulu
Chamwino, mkoani Dodoma.
Ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Bw. Rick Menell,
aliyeambatana na Mjumbe wa Bodi ya Kampuni ya Sotta Mining Corporation Limited,
Prof. Raphael Chibunda, katika mazungumzo yaliyolenga kujadili maendeleo ya Mgodi
wa Dhahabu wa Nyanzaga uliopo wilayani Sengerema, mkoani Mwanza.
Mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 523 (zaidi ya shilingi trilioni moja)
tayari umeingia katika hatua kamili ya ujenzi, na unatarajiwa kuanza uzalishaji katika
kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2027, ukiwa ni mgodi mkubwa wa kwanza mpya
wa dhahabu kuanzishwa nchini takribani miaka 20 iliyopita.
Mgodi wa Dhahabu wa Nyanzaga unatekelezwa na Kampuni ya Sotta Mining Corporation
Limited, ambayo ni ubia baina ya Kampuni ya Perseus Mining Limited yenye umiliki wa
asilimia 80, na Serikali ya Tanzania inayomiliki asilimia 20 ya hisa.
Hadi mwezi Februari, 2026, makadirio ya akiba ya madini katika eneo la mradi yalikuwa
wakia milioni 4.0, sawa na ongezeko la asilimia 73 kutoka wakia milioni 2.3 za awali, na
hivyo kuongeza makisio ya uhai wa mgodi huo hadi kufikia miaka 16.
Mradi huo unatarajiwa kuzalisha wastani wa wakia 200,000 za dhahabu kwa mwaka, na
kufikia kilele cha uzalishaji wa wakia 250,000 mwaka 2028.
Kazi za maandalizi ya mgodi zinaendelea, sambamba na ujenzi wa kambi ya kudumu ya
wafanyakazi, inayotarajiwa kukamilika katikati ya mwaka 2026, huku ujenzi wa nyumba za wananchi wa maeneo yaliyopitiwa na mradi zikiwa katika hatua za mwisho kukamilika,
chini ya mpango wa uhamaji na fidia.
Rais Dkt. Samia amepongeza uwekezaji huo mkubwa, akisema unaonesha kuimarika kwa
sekta ya madini na nafasi yake katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesisitiza kuwa mradi huo unapaswa kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa
Watanzania, hususan jamii zinazozunguka eneo la mgodi, kupitia ajira, usambazaji wa
bidhaa na huduma mgodini, pamoja na utekelezaji wa miradi ya kijamii.
Aidha, amesema Serikali inataka kuona ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa
thamani wa mradi huo, ili uwekezaji mkubwa unaofanyika katika sekta ya madini ufungue
fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji
nchini ili kuvutia mitaji zaidi katika sekta ya madini na maeneo mengine ya kimkakati,
huku akizielekeza taasisi zinazohusika na uwekezaji kushughulikia kwa haraka
changamoto zinazowakabili wawekezaji nchini.
Kwa upande wao, wawakilishi wa kampuni ya Perseus Mining Limited wameipongeza
Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji, wakiahidi
kushirikiana na Serikali katika kuleta mabadiliko makubwa ya miundombinu na teknolojia
katika mnyororo wa uzalishaji wa dhahabu nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde kwenye picha na Ujumbe wa Kampuni ya Perseus Mining Limited na Sotta Minining Corporation Limited mara baada ya mazungumzo yao, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 6 Mei, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde kwenye picha na Ujumbe wa Kampuni ya Perseus Mining Limited na Sotta Minining Corporation Limited mara baada ya mazungumzo yao, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 6 Mei, 2026.Perseus Mining Limited ni mwekezaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Nyanzaga, Wilayani Sengerema, Mkoani Mwanza kupitia Kampuni ya Sotta Minining Corporation Limited, inayomilikiwa kwa ubia na Serikali ya Tanzania.






0 comments:
Post a Comment