Nafasi Ya Matangazo

April 12, 2026






Na Mwandishi wetu, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepatiwa mafunzo maalum kuhusu Sheria, Kanuni na Miongozo ya Sekta ya Madini, kwa lengo la kuongeza uelewa hususan juu ya tofauti kati ya Haki ya Ardhi na Haki ya Madini.

Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Tanzanite, Makao Makuu ya Tume ya Madini, jijini Dodoma.

Akizungumza katika semina hiyo, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa umiliki wa haki ya madini na haki ya ardhi ni mambo mawili tofauti kisheria, na kwamba mwenye leseni ya madini haruhusiwi kuanza shughuli za uchimbaji bila kufikia makubaliano na mmiliki wa ardhi husika.

Amefafanua kuwa, kwa mujibu wa Sheria, leseni ya madini inaweza kutolewa katika eneo lolote, lakini utekelezaji wake unahitaji ridhaa au makubaliano na mwenye haki ya ardhi. Hata hivyo, iwapo makubaliano hayatapatikana, Waziri ana mamlaka ya kuruhusu shughuli za uchimbaji kuendelea kwa kuzingatia sheria.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yameongeza uelewa na kuwajengea wabunge uwezo wa kusimamia vyema sekta hiyo.

Wasilisho kuhusu haki ya madini na haki ya ardhi limetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Madini, Dkt. Arnold Gisase, ambaye ameeleza kuwa mtu anaweza kumiliki haki ya madini bila kuwa mmiliki wa ardhi, na kwamba umiliki wa ardhi pekee haumruhusu mtu kufanya shughuli za madini bila leseni husika.

Dkt. Gisase pia amebainisha changamoto zinazojitokeza, ikiwemo uelewa mdogo wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao, kutokuelewa taratibu za uthamini na fidia, ucheleweshaji wa malipo ya fidia, pamoja na baadhi ya wamiliki wa ardhi kudai kuwa sehemu ya umiliki wa leseni za madini.

Naye, Mwanasheria kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Method Akilimali, amesisitiza kuwa fidia kwa mmiliki wa ardhi lazima ilipwe kabla ya kuanza kwa shughuli za utafiti au uchimbaji.

Ameongeza kuwa sheria inamtaka mmiliki wa leseni kurejesha eneo katika hali yake ya awali baada ya shughuli za madini kukamilika. Aidha, ameeleza kuwa ardhi yote nchini ni mali ya umma chini ya usimamizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mdhamini.

Amesema pia fidia inapaswa kulipwa ndani ya miezi sita; kuchelewa hulazimu kulipwa riba, na endapo itazidi miaka miwili tangu uthamini kufanyika, tathmini hiyo hupoteza uhalali.

Akizungumzia muundo wa leseni, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema zipo aina kuu tatu za leseni ambazo ni leseni ya utafiti, uchimbaji mdogo na uchimbaji mkubwa ambapo kwa leseni ya uchimbaji mdogo Mtanzania pekee mwenye umri wa kuanzia miaka 18 ndiyo anaruhusiwa kuomba.

Mhandisi Lwamo amesema leseni kubwa na ya kati inaruhusiwa kuombwa na mtu yoyote na kwa sasa kuna mfumo wa kuomba leseni bila kufika ofisi za madini.

Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wabunge kuelewa kwa kina masuala ya kisheria na kiutendaji katika sekta ya madini ili kuboresha usimamizi na maamuzi yenye tija kwa maendeleo ya taifa.
Posted by MROKI On Sunday, April 12, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo