Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Serikali imejipanga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha madini ya kimkakati na shughuli za uongezaji thamani barani Afrika, huku akizitaka taasisi za sekta hiyo kutumia fursa zilizopo kuhakikisha nchi inahudumia masoko ya kikanda na kimataifa.
Mhe. Mavunde ameyasema hayo Juni 19, 2026, baada ya kufanya ziara katika Kituo cha African Minerals and Geoscience Centre (AMGC) kilichopo Kunduchi jijini Dar es Salaam, ambapo alipata fursa ya kutembelea maabara, kitengo cha ukataji, utengenezaji na usafishaji wa vito pamoja na kuzungumza na viongozi pamoja na watumishi wa kituo hicho.
“Tumedhamiria kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha madini ya kimkakati barani Afrika. Tunayo nafasi kubwa kutokana na eneo letu la kijiografia na miundombinu iliyopo, hivyo ni lazima tutumie fursa hii kuhakikisha tunazihudumia nchi zote zinazotuzunguka na kuifanya Tanzania kuwa lango la huduma za madini katika ukanda huu,” amesema Waziri Mavunde.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini inaendelea kutekeleza programu ya *Mining for a Brighter Tomorrow*, inayolenga kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kiuchumi kupitia sekta ya madini.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, programu hiyo itahusisha utoaji wa mafunzo ya kitaalamu katika vituo mbalimbali vya sekta ya madini ikiwemo AMGC, ambapo wanufaika watapatiwa maarifa pamoja na teknolojia na mashine ndogo zitakazowawezesha kujiajiri na kuongeza kipato chao.
“Tutawaleta vijana, kina mama na watu wenye ulemavu hapa AMGC wapatiwe mafunzo maalum, na baada ya hapo waweze kupata vifaa na mashine ndogo zitakazowawezesha kujiajiri na kuboresha maisha yao kupitia shughuli za madini,” ameeleza.
Katika ziara hiyo, Waziri Mavunde amesema amevutiwa na kiwango cha utaalamu kilichopo AMGC, hususan katika ukataji na utengenezajishaji wa madini ya vito, akisema dhana iliyokuwa imejengeka kuwa Tanzania haina wataalamu wa kutosha katika eneo hilo siyo sahihi.
“Kwa muda mrefu tuliaminishwa kwamba hatuna wataalamu wa kutosha katika ukataji wa madini ya vito, lakini leo nimeshangazwa kukutana na wataalamu wazawa wenye uwezo mkubwa wa kukata na kutengeneza vito kwa viwango vya kimataifa. Huu ni uthibitisho kwamba tuna rasilimali watu wenye uwezo wa kuipeleka Tanzania mbele zaidi,” amesema.
Aidha, Waziri Mavunde amesema hiyo ilikuwa ziara yake ya kwanza katika kituo hicho na kuahidi kukitangaza kimataifa ili kuvutia wawekezaji, wataalamu na wadau mbalimbali wa sekta ya madini kutoka ndani na nje ya Afrika.
“Niwahakikishie kwamba tutakitangaza kituo cha AMGC kimataifa ili Tanzania iwe kitovu cha uongezaji thamani wa madini barani Afrika. Pia nitarudi tena hapa kukutana na watumishi wote, kusikiliza changamoto zao na kujadiliana namna bora ya kukiendeleza kituo hiki,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa AMGC, Ibrahim Shaddad, amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi, ambapo kwa sasa kina watumishi wa kudumu 17 na watumishi wa mikataba ya muda mfupi 12, hali inayokifanya kushindwa kutekeleza kikamilifu baadhi ya majukumu yake.
Aidha, Shaddad amemuomba Waziri wa Madini kusaidia katika upatikanaji wa fedha za uendeshaji wa kituo hicho, hususan kupitia nchi wanachama ambazo kwa mujibu wa sheria zinapaswa kuchangia gharama za uendeshaji, lakini baadhi yake zimekuwa zikichelewesha au kutotekeleza wajibu huo.
Shaddad amesema ucheleweshaji wa michango kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama umeendelea kuathiri shughuli za kila siku za AMGC na kusababisha upungufu wa fedha za uendeshaji.
Ametaja Tanzania, Kenya, Angola na Sudan kuwa miongoni mwa nchi zinazowasilisha michango yao kwa wakati, huku baadhi ya nchi nyingine ikiwemo Msumbiji, Ethiopia, Comoro, Sudan Kusini na Uganda zikikabiliwa na changamoto ya kutowasilisha michango hiyo kwa wakati.
AMGC ni taasisi ya kikanda inayojihusisha na tafiti za jiolojia, huduma za maabara, mafunzo na maendeleo ya teknolojia za madini kwa nchi wanachama wa Afrika, na imeendelea kuwa moja ya taasisi muhimu katika kuendeleza sekta ya madini na kuongeza thamani ya rasilimali za madini barani Afrika. Uh















0 comments:
Post a Comment