Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali inatarajia kujenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia mkopo wa shilingi trilioni 1.2, badala ya kufanya ukarabati wa majengo yaliyopo sasa.
Dkt. Samizi ametoa ufafanuzi huo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Sumbawanga, Mhe. Aeshi Hillary, aliyehoji kuhusu matumizi ya mkopo huo uliotengwa kwa ajili ya hospitali hiyo.
Amesema uamuzi wa kujenga hospitali mpya unatokana na hali ya majengo ya sasa kuwa yamechoka na kusambaa katika maeneo mbalimbali, hali inayopunguza ufanisi wa utoaji huduma na kushindwa kukidhi viwango vinavyohitajika kwa hospitali ya taifa.
Ameeleza kuwa kupitia mkopo huo, Serikali itatekeleza ujenzi wa hospitali ya kisasa pamoja na usimikaji wa mitambo ya tiba ya kisasa, hatua itakayoongeza ubora wa huduma za afya na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Aidha, amebainisha kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa majengo mapya ya hospitali yenye jumla ya vitanda 1,301 pamoja na vitanda 100 vya watoto wachanga (bay cots), ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, pamoja na uwekaji wa Mfumo wa Kisasa wa Taarifa za Afya (Health Information System – HIS).
Pia, mradi huo unaendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa katika kuimarisha huduma za afya za ubingwa na ubingwa bobezi, sambamba na kuimarisha mafunzo na utafiti katika sekta ya afya.
Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuchukua takribani miaka nane, huku huduma za kila siku katika hospitali hiyo zikiendelea kutolewa bila kusitishwa.
Aidha, mradi huo ni hatua muhimu ya Serikali katika kuboresha miundombinu ya afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ndani ya nchi bila kulazimika kusafiri nje kwa matibabu.










0 comments:
Post a Comment