Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe.Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa wito kwa jamii na wazazi kushiriki kikamilifu katika malezi na ulinzi wa watoto, ili kuzuia ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 01, 2026 jijini Dodoma kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani, yatakayofanyika Aprili 12, 2026 Jijini Dar Es Salaam yakiwa na Kaulimbiu isemayo “Malezi na Ulinzi wa Mtoto, Wajibu wetu Sote”.
Amesema ushiriki wa pamoja ni muhimu ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye maadili mema huku akisisitiza jukumu la malezi si la wazazi pekee, bali ni la jamii nzima.
Aidha, Waziri Gwajima ameeleza kuwa changamoto kama umasikini, migogoro ya kifamilia, na ukatili dhidi ya watoto zimekuwa zikichangia watoto wengi kukimbilia mitaani.
Ameibainisha pia mafanikio ya juhudi za Serikali katika kuwaokoa watoto wa mitaani kuwa zaidi ya watoto 5,000 wameunganishwa na familia zao tangu kuanza kwa kampeni ya kuwaokoa watoto wa mitaani mwaka 2025.
Vilevile, Serikali imeanzisha mifumo mbalimbali, ikiwemo madawati ya ustawi wa jamii katika vituo vya usafiri na makao ya watoto, ili kuhakikisha watoto waliookolewa wanapata huduma muhimu kama elimu, afya, na malezi bora.
Waziri Gwajima ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa za ukatili dhidi ya watoto na kuhakikisha wanapata malezi bora. Amesisitiza kuwa watoto wa mitaani wanapaswa kulindwa na kupewa fursa sawa za maendeleo, akihitimisha kwa kusema kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha hakuna mtoto anayelazimika kuishi au kufanya kazi mitaani.
Waziri Gwajima ametumia nafasi hiyo pia kuwashukuru wadau wote wanaoshirikiana na Serikali katika kuhakikisha malezi ya watoto yanaimarishwa hususani shirika SoS Village na Railway Children.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Dodoma, mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kukabiliana na changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, akieleza hatua mbalimbali zilizofikiwa na mkoa wa Dodoma.
Shekimweri amesema mwaka 2024 hadi 2026 Serikali ya mkoa imewaunganisha watoto 293 na familia zao.











0 comments:
Post a Comment