Nafasi Ya Matangazo

June 25, 2026

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Chemba amesema michezo ya watu wenye ulemavu imeiletea heshima kubwa Tanzania kimataifa katika nyanja ya michezo.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu ameeleza hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Yumna Mmanga aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inasimamia michezo ya watu wenye ulemavu iweze kushinda medali ambapo Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika michezo ya watu wenye ulemavu ili kuitangaza zaidi Tanzania.
“Ni kweli timu zetu zimekuwa zikishiriki mashindano mbalimbali ya watu wenye ulemavu, na kweli hazijafanikiwa kuleta medali, lakini kwa kweli wameiletea sifa kubwa nchi yetu,” amesema Waziri Mkuu.
“Kama Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka, timu yetu ya Tembo Warriors ilishiriki Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Uturuki, na tena haikushiriki kinyonge, ilishiriki kama timu iliyojiandaa na ilionesha mchezo mzuri sana, kadhalika ikashiriki michuano ya AAFCON ya wenye ulemavu mwaka 2024 nchini Misri, pamoja na michuano ya CECAFA ya wenye ulemavu ya mwaka huu nchini Burundi, ambako ilifika fainali, siyo jambo dogo,” ameongeza Dkt. Mwigulu.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutengeneza mazingira ya kuhakikisha timu mbalimbali zinatwaa medali, ikiwemo kutengeneza miundombinu ya michezo ya watu wenye ulemavu na kusajili timu na wachezaji wa michezo ya watu wenye ulemavu.
“Pamoja na kwamba kwenye yale mashindano timu zetu hazikupata medali nyingi, lakini bado wachezaji wa timu zile waliweza kuonekana duniani na kusajiliwa na timu mbalimbali, Serikali itaendelea kuwekeza katika michezo hiyo ili kuhakikisha timu zetu zinapata mafanikio zaidi,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Posted by MROKI On Thursday, June 25, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo