Nafasi Ya Matangazo

January 04, 2026

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Jumla ya Wapiga Kura 20,851 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura watashiriki katika uchaguzi wa kuchagua madiwani katika Kata ya Kirua Vunjo Magharibi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro na Kata ya Mindu iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoa wa Morogoro.
 
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele leo Januari 04, 2026 wakati akisoma risala maalum kuhusu uchaguzi katika Kata hizo utakao fanyika Januari 05,2026 na kusema kuwa jumla ya vituo 55 vya Kupigia Kura vitatumika.
 
Aidha, amesema jumla ya wagombea watano (5) kutoka katika vyama vya siasa vinne (4) wanawania nafasi wazi za udiwani katika maeneo hayo na kuvipongeza vyama vya siasa na wagombea waliojitokeza kushiriki katika uchaguzi huo.
 
“Natumia fursa hii kuvikumbusha Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi kesho Januari 05,2026 kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya zoezi la kupiga, kuhesabu na kujumlishia kura. Wasimamizi wa uchaguzi katika Majimbo na Kata husika, wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha mawakala wa vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi,”alisema Jaji Mwambegele.
 
Amesema, mawakala hao, wanawajibika katika kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao. Hivyo, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu za Uchaguzi na maelekezo ya Tume katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni.
 
Jaji Mwambegele amesema vituo vitafunguliwa saa 01:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Ifikapo muda wa kufunga kituo saa 10:00 kamili jioni, kama wapiga kura bado wapo kwenye mistari, mlinzi wa kituo atasimama nyuma ya mtu wa mwisho na zoezi la upigaji kura litaendelea hadi wapiga kura walio kwenye mstari watakapomalizika.
 
“Baada ya kumaliza kupiga kura, mpiga kura anatakiwa kuondoka eneo la kituo cha kupigia kura; na Mpiga kura awapo kituoni, anatakiwa kufuata maelekezo yote atakayopewa na karani mwongozaji wapiga kura,”alisema Jaji Mwambegele.
 
Kwa mpiga kura ambaye ameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na taarifa zake zipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililopo katika kituo husika, lakini amepoteza kadi yake au kadi yake imeharibika, ataruhusiwa kupiga Kura kwa kutumia moja wapo ya vitambulisho cha Taifa NIDA, Leseni ya udereva au Pasi ya kusafiria (Passport).
Posted by MROKI On Sunday, January 04, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo