Na Mwandishi Wetu- Dar es
Salaam. Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa
Pamoja (PBPA) leo tarehe 30 Januari, 2026 umepokea ugeni wa wanafunzi 30 wa
Kitengo cha Petroleum Engineering kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na
Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), chini ya Chama cha wahandisi wa mafuta
(Society of Petroleum Engineers -SPE),waliotembelea Wakala huo kwa lengo la
kujifunza kwa vitendo kuhusu utendaji kazi wa PBPA na namna Mfumo wa Uagizaji
Mafuta kwa Pamoja (BPS) unavyotekelezwa nchini.
Akizungumza wakati wa ziara
hiyo, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Lojistiki za Mafuta PBPA, Mhandisi Sophia
Kidimwa, alisema kuwa wanafunzi hao wamepata fursa ya kuelewa mchakato mzima wa
upatikanaji wa mafuta nchini kuanzia hatua za uagizaji hadi usimamizi wa
lojistiki za kupokea mafuta.
“Tumepokea ugeni wa wanafunzi
wa mwaka wa nne kutoka UDSM na DMI waliokuja kujifunza kuhusu taratibu zote za
upatikanaji wa mafuta hapa Tanzania, jinsi mafuta yanavyoingia nchini, mchakato
mzima wa uletaji wake pamoja na lojistiki za kupokea mafuta na manufaa ya Mfumo
wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS),” alisema Sophia.
Aliongeza kuwa PBPA imekuwa
ikipokea wageni kutoka taasisi mbalimbali zinazopenda kujifunza kuhusu mfumo wa
BPS kutokana na mafanikio na manufaa yake kwa Taifa.
“Kama taasisi, tumekuwa
tukitoa uelewa huo kwa wageni wetu na wamekuwa wakionyesha kuridhika.
Tunaendelea kuwakaribisha wadau wote wanaopenda kujifunza kuhusu Mfumo wa
Uagizaji Mafuta kwa Pamoja,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mhandisi
kutoka Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Prudence Laurean, alisema
wanafunzi hao walipitishwa katika mifumo yote ya PBPA kuanzia hatua za uagizaji
wa mafuta hadi mafuta yanapofika kwenye maghala ya kuhifadhia, ikiwemo matumizi
ya Mfumo wa SCADA katika ufuatiliaji wa mafuta wakati wa kushushwa kutoka melini
kwenda kwenye maghala ya Serikali na binafsi.
“Mafunzo haya ni muhimu sana
kwa wanafunzi kwani yanawajengea uelewa wa kina kuhusu kazi za PBPA na faida
zitakazowasaidia kitaaluma hapo baadaye,” aliongeza.
Akizungumza kwa niaba ya
wanafunzi, Sifrina John, mwanafunzi wa mwaka wa nne Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, alisema ziara hiyo imelenga kuwaunganisha wanafunzi na uhalisia wa kazi
katika sekta ya mafuta nchini.
“Lengo letu ni kuunganisha
yale tunayojifunza darasani na mazingira halisi ya kazi katika sekta ya mafuta,
na kuelewa kwa vitendo jinsi PBPA inavyofanya kazi katika uagizaji na usimamizi
wa ugavi wa mafuta nchini,” alisema Sifrina.
Aliongeza kuwa wanafunzi
wamefurahishwa na mafunzo waliyoyapata na namna PBPA inavyosimamia ugavi wa
mafuta pamoja na mchango wake katika uchumi wa Taifa.
“Tumepata uelewa wa kina
kuhusu mchakato wa uagizaji wa mafuta, usimamizi wa ugavi na mchango wa PBPA
katika uchumi wa nchi. Mafunzo haya yametujenga kwa kiasi kikubwa kwa
kuunganisha nadharia na vitendo,” alisisitiza.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa
juhudi za PBPA katika kuimarisha ushirikiano na wadau kutoka taasisi mbalimbali
nchini sambamba na kukuza uelewa wa vijana kuhusu mifumo ya kimkakati
inayosimamia sekta ya mafuta na mchango wake katika uchumi wa Taifa.
Posted by MROKI
On Friday, January 30, 2026
No comments
0 comments:
Post a Comment