Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akihutubia
wakati wa uzinduzi wa Jengo la Viongozi Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 16 Januari 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali imejizatiti kuhakikisha Sekta ya Uchukuzi
inaimarika ili kuliweka Taifa kwenye nafasi nzuri ya ushindani wa kibiashara,
kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kukuza mchango wa sekta hiyo katika pato
la Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa
Jengo la Viongozi Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere Jijini Dar es Salaam. Amesema pamoja na ujenzi wa jengo hilo, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga
kikamilifu kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kisekta kama
ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, Mpango wa Miaka
Mitano wa Maendeleo ya Taifa na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi
(2025).
Makamu wa Rais amesisitiza kwamba, Serikali
itaendelea kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali katika Viwanja vya Ndege,
huduma za usafiri wa barabara, usafiri majini na usafiri kwa njia ya reli.
Halikadhalika amesema, Serikali itaendelea na uboreshaji wa huduma za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL)
kwa lengo kuboresha usafiri wa ndani,
kuunganisha Tanzania na nchi nyingine, kupunguza gharama za usafirishaji na
kuimarisha uchumi wa Tanzania na biashara za kimataifa.
Vilevile, Makamu wa Rais amesema ili kuboresha huduma za usafiri na
usafirishaji, Serikali imedhamiria kuunganisha huduma za Sekta ya Uchukuzi,
kama vile uunganishaji wa huduma za Viwanja vya Ndege, usafiri wa barabara, maji na reli. Mathalan,
mradi wa kimkakati unaoendelea wa ujenzi wa barabara za Mwendokasi (BRT) kati
ya eneo la Posta na Gongo la Mboto utaunganishwa na Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere ili kurahisisha huduma za usafiri katika jiji la
Dar es Salaam.
Hali
kadhalika, hatua za utekelezaji zinaendelea ili kuhakikisha huduma za reli
zinaunganishwa na viwanja vya Ndege vya kimataifa, hususan Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato
na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro.
Aidha, Makamu wa Rais amesema Jitihada hizo kubwa zinazofanywa na
Serikali zinalenga kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji ili kuchochea
ukuaji wa uchumi kitaifa na kikanda. Ameongeza kwamba, hiyo inatokana na fursa
na faida za kijiografia za Tanzania, ambayo ni lango kuu la biashara la nchi
zaidi ya nane zilizopo Kusini, Mashariki
na Kati ya Bara la Afrika, na kiunganishi cha Bara la Afrika na nchi za
Mashariki ya Kati na Mbali.
Makamu wa Rais amesema, dhamira ya Serikali ni
kuendeleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo, ujenzi wa
reli ya kisasa kwa vipande na maeneo
yote yaliyobaki kuelekea Tabora, Mwanza na Kigoma hadi Musongati (Burundi),
uboreshwaji wa Bandari ya Dar es Salaam na Bandari nyingine za kimkakati za Tanga,
Mtwara, Kisiwa Mgao, Mbamba Bay, Kigoma na Bagamoyo, uboreshaji wa reli ya
TAZARA, ujenzi na ukarabati wa barabara za lami zinazounganisha Tanzania na
nchi za jirani.
Pia, Makamu wa Rais amesema uwekezaji
wa Serikali katika Sekta ya Uchukuzi umeleta manufaa makubwa. Mathalan,
mchango wa Sekta ya Uchukuzi katika Pato
la Taifa uliongezeka kutoka 7.2% (2023) hadi 7.5% (2024). Kasi ya ukuaji wa
Sekta ya Uchukuzi iliongezeka kutoka 4.1% (2023) hadi 4.2% (2024) na katika
kipindi cha hivi karibuni ilikua kwa
wastani wa 5.4%.
Makamu wa Rais
ametoa rai kwa kwa Watanzania wote kutambua wajibu wa kuilinda na kuitunza
miundombinu inayoendelea kuwekezwa na Serikali kwa manufaa ya kizazi cha sasa
na kijacho.
Kwa upande wake
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema Wizara itaendelea kuhakikisha
miradi ya Viwanja vya Ndege nchini inaendelea kutekelezwa ili kuongeza huduma
ya usafiri wa Anga na hivyo kufungua na kuchochea shughuli mbalimbali za
kiuchumi nchini.
Amesema Serikali
katika kuhakikisha inaendelea kuimarisha shughuli utalii, biashara na
kilimo,Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania inaendelea na hatua
za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ya viwanja vipya vya Serengeti, Kagera
na Njombe na mara baada ya kukamilika itatafuta fedha kwaajili ya utekelezaji
wa miradi hiyo.
Awali akitoa
taarifa ya mradi wa Jengo la Viongozi Mashuhuri, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege, Abdul Mombokaleo amesema mradi huo ni sehemu ya utakelezaji
wa mpango mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kuhusu uimarishaji wa
Miundombinu na huduma za Viwanja vya Ndege.
Jengo la Viongozi
Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es
Salaam, limejengwa mahsusi kwaajili ya kuhudumia wageni na Viongozi mashuhuri
wa ndani na nje ya nchi. Jengo hilo ni hatua muhimu katika kuimarisha taswira
ya Taifa na kuongeza hadhi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
katika ngazi ya kimataifa..jpg)
0 comments:
Post a Comment