WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amemwagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini amsake kokote alipo mkandarasi wa kampuni ya Tunnel Sadd Ariana na kumnyang'anya hati yake ya kusafiria kwa kushindwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa bwawa katika mradi wa umwagiliaji wa Ziwa Eyasi.
“Huyu mtu amelipwa fedha na Serikali, lakini amepata wapi ujasiri wa kutufungulia kesi mahakamani wakati amekusanya vifaa tu na hajaanza kazi? Hii haikubaliki, ni dharau kwa nchi. Nimemwagiza Kamishna wa Uhamiaji, huyu mkandarasi atafutwe popote alipo, anyang'anywe pasi yake ya kusafiria, asiende kokote.”
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Machi 6, 2026) wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mazingira mjini Karatu, mkoani Arusha.
Waziri Mkuu amesema mkandarasi huyo alipaswa kujenga mradi huo wenye thamani ya sh. bilioni 21 na akalipwa malipo ya awali ya sh. bilioni tatu lakini hajafanya kazi. “Ipo michezo ya wakandarasi hasa wale wanaotaka walipwe kwenye akaunti za kwao. Nilishatoa maelekezo kwamba kuanzia sasa, fedha zilipwe katika akaunti zao kwenye benki za hapa Tanzania,” amesema.
Mapema, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa skimu za umwagiliaji katika Bonde la Eyasi, lililopo kilometa 50 kutoka mjini Karatu.
Amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi 780 ya umwagiliaji inayoendelea kujengwa nchi nzima. “Mradi huu ni kama miradi inayoendelea kujengwa kule Isimani na Msingi. Miradi hii siyo ya serikali bali ni kwa ajili ya mashamba ya Watanzania walioko vijijini. Serikali haitavumilia uzembe, wizi na udokozi katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za walipakodi.”
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi iliyowasilishwa, mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, utagharimu sh. bilioni 38.4. Hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 30 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, mwaka huu.
Kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha zaidi ya wakulima 2,500 kutoka skimu za Mang’ola Barazani, Maleckchand, Laghangareri, Mbuga Nyekundu, Jobaji na Dumbechand, zenye zaidi ya hekta 5,000.
Aidha, utekelezaji wa mradi huo utasaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa upotevu wa maji unaotokea katika mifereji ya asili, hatua itakayoongeza ufanisi wa matumizi ya maji na kuimarisha uzalishaji wa mazao katika eneo hilo.












0 comments:
Post a Comment