Mameneja wa mikoa na vituo wa Wakala wa
Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kubadilisha mitazamo ya
watumishi na wanaopewa huduma na Wakala ili kuufanya kuwa mfano wa kuigwa na
Taasisi zingine za Umma.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Moses R. Mabamba alipokuwa akizungumza na mameneja wa Mikoa na vituo katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Wakala mjini Dodoma ambapo
amewaagiza mameneja hao kufanya kazi kwa bidii ili kutoa huduma bora kwa
Serikali na jamii kwa ujumla ambazo zitaifanya TEMESA iweze kuwa na uwezo wa
kutekeleza majukumu yake mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maslahi bora ya
watumishi.
“Tufanye kazi tuzalishe,
tulete hela tuwalipe watumishi, mfanyakazi ni rasilimali ya thamani kwenye Taasisi
na ndiye ambaye anaifanya biashara yako ifanyike, tunahitaji kujenga taswira
yetu nzuri ili kuwapa imani wateja wetu.” Ameongeza Mabamba.
Katika hatua nyingine, Kaimu
Mtendaji Mkuu amewapa miezi mitatu watumishi wazembe ambao hawataki kufanya
kazi kubadilika na amewapa miezi mitatu kuanzia sasa watumishi hao kubadilika
ama la sivyo watafikiwa na kuchukuliwa hatua stahiki.
“Lakini wale walioshindikana
kabisa mtanipa na mimi huwa sio muumini wa watu ambao hawataki kufanya kazi,
ukiuliza mtu yoyote upande wangu mbaya huwa ni huo na napenda kuutekeleza kwa
haraka sana, kwa hiyo wale watoboa mitumbwi tuwape muda kwanza wajibadilishe,
tuwape miezi mitatu.’’ Amesema Mabamba.
Aidha, Mabamba amewaagiza
mameneja hao kufikiria kibiashara kwakuwa maeneo mengi ya Wakala huo
yanashawishi kufanyika kwa biashara kutoka vyanzo vingine na kuongeza kuwa
faida kubwa ambayo TEMESA inayo ni kuwa na maeneo maeneo ya thamani yenye
kushawishi ufanyikaji wa biashara.
0 comments:
Post a Comment