Nafasi Ya Matangazo

October 06, 2025

Timu ya wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ikikagua mojawapo ya kizimba ilipotembelea eneo Mwiseni kata ya Butimba, Wilayani Bunda Mkoani Mara Oktoba 6, 2025.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwiseni, Bw. Msiba Chiharata akizungumza wakati wa ziara ya timu ya wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilipotembelea eneo la kizimba Mwiseni kata ya Butimba, Wilayani Bunda Mkoani Mara Oktoba 6, 2025.
Muonekano wa mojawapo ya kizimba cha kuzuia mamba pembezoni mwa ziwa Victoria kilichojengwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika eneo la Nampangala kata ya Kisorya, Wilayani Bunda Mkoani Mara.
Mkazi wa kitongoji cha Nampangala kata ya Kisorya, Bunda mkoani Mara, Bw. Tabingwa Charles Kasao akiipongeza Serikali kwa kujenga vizimba vilivyosaidia kuepusha vifo vinavyotokana na mamba katika eneo analoishi , wakati wa ziara ya timu ya wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilipotembelea kata ya Kisorya leo Oktoba 6,2025.
Muonekano wa mojawapo ya kizimba cha kuzuia mamba pembezoni mwa ziwa Victoria kilichojengwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika eneo la Kasahunga kata ya Neruma, Wilayani Bunda Mkoani Mara.
Muonekano wa mojawapo ya kizimba cha kuzuia mamba pembezoni mwa ziwa Victoria kilichojengwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika eneo la Mwiseni kata ya Butimba, Wilayani Bunda Mkoani Mara.
*****************
Wananchi wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara wameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kwa kuwajengea vizimba vya kuzuia mamba kuwadhuru wakati wa kuchota maji ziwani na kufanya shughuli zingine pembezoni mwa Ziwa Victoria ikiwemo kufua na kuoga.

Wamesema hayo leo Oktoba 6, 2025 kwa nyakati tofauti wakati timu ya wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilipotembelea maeneo ya vizimba hivyo.

Akizungumza katika ziara hiyo,Mkazi wa Mwiseni,kata ya Butimba, Bi. Gabaseki Gervaz  amesema wamefurahi sana kupata kizimba kutokana na changamoto walizokuwa wanakutana nazo mwanzoni za kukamatwa na mamba wanapofanya shughuli zao pembezoni mwa ziwa.

"Serikali baada ya kuona tunateseka kutokana na vifo kila mwaka kwa kuuliwa na mamba ikajenga kizimba hiki" amesema Bi. Gervas na kuiomba Serikali kuongeza vizimba vya ziada kwa ajili ya jinsia ya kiume na mifugo.

Naye, Bw. Tabingwa Charles Kasao mkazi wa kitongoji cha Nampangala kata ya Kisorya ,Bunda mkoani Mara ameishukuru Serikali kwa kujali wananchi na kujenga kizimba katika eneo hilo na kuepusha vifo vya wananchi wakiwemo wanafunzi wanaotumia ziwa hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwiseni, Bw. Msiba Chiharata amesema kutokana na faida za vizimba katika kuzuia mamba wanaodhuru wananchi, wameweka adhabu kwa wananchi wanaojaribu kuharibu eneo la Kizimba.

"Tumeweka adhabu kwa mtu yeyote atakayefanya uharibifu wa aina yeyote ile iwe ni kuanika nguo au kuingiza mifugo eneo la vizimba faini ni shilingi laki moja" amesema Bw.Msiba.
Posted by MROKI On Monday, October 06, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo