Nafasi Ya Matangazo

June 19, 2026




Na Adelina Johnbosco - MAELEZO
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo itaendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya michezo nchini kwa kushiriki kikamilifu kufanikisha mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanayotarajiwa kufanyika nchini Tanzania mwaka 2027.

Dkt. Nsekela ametoa kauli hiyo Juni 19, 2026, alipotembelea banda la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kwenye viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Amesema CRDB iko tayari kushirikiana kwa karibu na wizara hiyo katika kuhakikisha maandalizi na utekelezaji wa AFCON 2027 unafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

"Sisi CRDB tunaahidi kuwa na wizara hii bega kwa bega kila hatua pale tutakapohitajika. Ni wadau wakubwa wa michezo na sekta nyingine zilizo chini ya wizara hii, hivyo nawahakikishia kwamba tutashiriki kwa nguvu zote kuifanikisha AFCON 2027," amesema Dkt. Nsekela.

Mbali na ahadi hiyo, Dkt. Nsekela ameipongeza Wizara kwa namna ilivyojipanga katika kutoa huduma na elimu kwa wananchi kupitia maonesho hayo, akieleza kuwa ushiriki wa taasisi zote chini ya wizara hiyo umeongeza ufanisi wa utoaji huduma.

"Hii ni wizara inayogusa sekta nyingi muhimu. Mmefanya vizuri kushiriki maonesho haya pamoja na taasisi zenu zote ili mwananchi anapohitaji msaada asikwame, bali apate suluhisho kwa haraka na urahisi," ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Bi. Savera Salvatory, ameishukuru Benki ya CRDB kwa ahadi ya ushirikiano na kuipongeza kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya michezo na maeneo mengine ya kijamii.

Bi. Savera amesema wizara itaendelea kuboresha huduma zake kwa wananchi na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha sekta zilizo chini yake zinapiga hatua zaidi.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 23, 2026.
Posted by MROKI On Friday, June 19, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo