Nafasi Ya Matangazo

June 17, 2025

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahimiza wafugaji nchini kushiriki kikamilifu katika Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo ili kulinda afya ya mifugo yao, kuongeza uzalishaji na kufungua fursa zaidi za biashara ya mifugo katika soko la ndani na nje ya nchi.

Akizindua kampeni hiyo leo, Rais Dkt. Samia amesema Serikali itagharamia nusu ya gharama za chanjo na utambuzi kwa lengo la kumuwezesha mfugaji mdogo kupata huduma bora kwa bei nafuu na aliongeza kuwa Serikali itabeba gharama zote za uwekaji wa hereni kwa mifugo ili kupata takwimu sahihi zitakazowezesha kupanga na kusimamia sekta hiyo kwa tija zaidi.

Rais Dkt. Samia amesema kuwa pamoja na Tanzania kuwa na idadi kubwa ya mifugo, mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa bado ni mdogo kutokana na changamoto za magonjwa, ukosefu wa takwimu na miundombinu hafifu.

Vilevile, Rais Dkt. Samia ameielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka utaratibu maalum utakaowezesha zoezi la utambuzi wa mifugo kuwa endelevu na kufikia maeneo yote nchini na amesema kuwa chanjo zote zitakazotumika kwenye kampeni hiyo zitazalishwa hapahapa nchini.
 
Aidha, Rais Dkt. Samia amezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo utakaotumika kama rejea kwa viongozi wa maeneo yote, wataalamu wa mifugo na wadau wa sekta binafsi katika kusimamia na kufanikisha kampeni hiyo.
 
Hali kadhalika, Rais Dkt. Samia amepongeza ushirikiano baina ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na makampuni ya ndani katika uzalishaji wa chanjo, hatua inayopunguza gharama za uagizaji chanjo kutoka nje na kuimarisha uwezo wa taifa kudhibiti magonjwa.
 
Pamoja na hayo, Rais Dkt. Samia ameziagiza mamlaka za Serikali kuhakikisha viwango vya ubora, usalama na ufanisi wa chanjo zinazozalishwa kabla ya kusambazwa kwa wafugaji.
 
Rais Dkt. Samia pia amesema hatua zinazochukuliwa hivi sasa, ikiwemo uanzishaji wa kanzidata ya kitaifa ya kilimo na mifugo, zinaanza kuleta mabadiliko chanya katika kupanga mipango ya kisekta, kufungua fursa za uwekezaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania kimataifa.
 
Rais Dkt. Samia pia amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi kushiriki katika kuendeleza mifumo ya uzalishaji, huduma na masoko ya mifugo kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali kupitia ubunifu wa kiteknolojia na huduma rafiki kwa mfugaji wa kawaida.
 
Mapema leo, Rais Dkt. Samia alianza ziara yake Mkoani Simiyu kwa kuzindua kiwanda cha kutengeneza mabomba ya maji na kiwanda cha kuchakata pamba vinavyomilikiwa na Kampuni ya NGS Tanzania Ltd.
 
Katika kuimarisha utawala bora, alizindua rasmi majengo mapya ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, na Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Simiyu.
 
Vilevile, Rais Dkt. Samia amefungua rasmi Shule ya Sekondari ya Wasichana ya mchepuo wa Sayansi ya Mkoa wa Simiyu, ambapo amesisitiza uwekezaji wa Serikali katika kuhakikisha watoto wa kike wanapata fursa zaidi ya kusoma masomo ya sayansi ili kuimarisha mchango wa wanawake katika ujenzi wa Taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua Mpango wa Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kitaifa kwa mwaka 2024/2025- 2028-2029 katika viwanja vya Nanenane Bariadi Mkoani Simiyu tarehe 16 Juni, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya heshima na shukrani kutoka kwa Mwenyekiti wa wafugaji Ndugu Mrida Mshote mara baada ya kuzindua Mpango wa Miaka Mitano wa Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika viwanja vya Nanenane Bariadi Mkoani Simiyu tarehe 16 Juni, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya heshima na shukrani kutoka kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji mara baada ya kuzindua Mpango wa Miaka Mitano wa Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika viwanja vya Nanenane Bariadi Mkoani Simiyu tarehe 16 Juni, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu akihutubia viongozi mbalimbali, wafugaji pamoja na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika viwanja vya Nanenane Bariadi Mkoani Simiyu tarehe 16 Juni, 2025.

Posted by MROKI On Tuesday, June 17, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo