WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amefungua mkutano Mkuu wa 15 wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa Tanzania (TOA) na amewataka viongozi waendelee kuimarisha taasisi hiyo ili iwe na nguvu na iweze kuishauri Serikali ipasavyo.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameieleza TOA kuwa viongozi wa Kitaifa wanaitaka taasisi hiyo kuwa sehemu ya mabadiliko chanya ya mwelekeo wa utendaji ili ichagize maboresho katika Serikali za Mitaa. ”Endeleeni kuhimiza wanachama kufanya kazi kwa weledi na uzalendo ili kuleta matokeo yanayotarajiwa na wananchi.”
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili 15, 2025) kwenye Mkutano Mkuu wa 15 wa TOA unaofanyika katika Ukumbi wa Jiji la Dodoma ulipo mji wa Serikali Mtumba. “Kwa kuzingatia ukaribu na ushirikiano wenu na wananchi, naamini mnazitambua changamoto zinazowakabili na mnaelewa afua ambazo zikitekelezwa zitawaletea maendeleo.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kwamba utekelezaji wa maboresho ya kisera na mipango mbalimbali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zinasimamiwa na TAMISEMI na Wakuu wa Mikoa umewezesha kuleta mafanikio yanayogusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya wananchi kwenye sekta za huduma za kijamii.
Akizungumzia kuhusu mifumo ya kielektroniki, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita imesimamia matumizi yake ili kuimarisha ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Mifumo hiyo ni pamoja na Mifumo ya Uhasibu, Mifumo ya ukusanyaji wa mapato, Manunuzi na Malipo. Matumizi ya Mifumo yamesaidia kupunguza urasimu, kurahisisha ulipaji wa malipo na kodi mbalimbali za Serikali na kuboresha ukusanyaji wa mapato hadi kufikia ukusanyaji wa zaidi ya shilingi bilioni 900.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuagiza uongozi wa TOA uwajibike kuhamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutanua wigo wa mapato ili kuongeza uwezo wa kujitegemea kimapato na kugharamia shughuli mbalimbali za uendeshaji na utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amewataka viongozi wote wa Mikoa na watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini, waendelee kusimamia maadili na uzalendo, mifumo ya ukusanyaji wa mapato pamoja na mifumo mingine yote iliyoanzishwa na Serikali kwenye ngazi zao.
Pia, Waziri Mchengerwa amewasisitiza viongozi hao waendelee kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha za umma pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kwani katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kumekuwa na ufanisi zaidi katika Serikali za Mitaa.
Awali, Mwenyekiti wa Taifa wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa Tanzania, Albert Msovela alisema wataendelea kusimamia taasisi hiyo na kuhakikisha wanatekeleza shughuli zote za Serikali kwa weledi na ufanisi mkubwa.
0 comments:
Post a Comment