
Na Mwandishi Wetu.
BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imesema kama vile Serikali inavyothamini taaluma ya Uandishi wa Habari na Waandishi wenyewe, ndivyo ambavyo waajiri/wamiliki wa vyombo vya habari wanavyotakiwa kuwapa thamani wanayostahili.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Televisheni cha Upendo tarehe 27 Machi, 2025, kwenye kipindi cha Wakeup Calls, Mjumbe wa Bodi hiyo Dkt. Egbert Mkoko, amesema kuwa kama Serikali inampa Mwandishi wa Habari Ithibati na Kitambulisho ina maana inamthamini.
“Serikali inamthamini huyu kwamba anastahili kuwa mwandishi wa habari kwa hiyo na yeye kama mwajiri ampe thamani inayostahili kwa sababu ukimwajiri halafu ukamwambia fanya kazi tutaangalia angalia mwisho mwa mwezi kama tutapata kitu, kama tukipata matangazo tutakupatia kitu, tusipopata tutaangalia mwezi ujao sasa hiyo itakuwa ajira au…," amesema na kuongeza;
“Sasa hiyo inakuwa unaishushia hadhi taaluma yenyewe. Kwa hiyo kwanza tutapeana elimu licha ya kwamba tunajua kuwa vyombo vya habari uchumi haujakaa vizuri, na kuna ripoti ilitoka mwaka jana kuhusu hali ya uchumi wa vyombo vya habari nadhani kuna mambo yatafanyika kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya vyombo vya habari kufanya kazi na kuwa na uchumi unaostahiki kuweza kuwalipa wana taaluma wake,” amesema Dkt. Mkoko.
Kwa mujibu wa Mjumbe huyo waandishi wa habari wanastahili kulipwa mishahara yao kwa wakati pia kupata haki zingine za msingi kama walivyo wafanyakazi wengine ikiwa ni pamoja na bima za afya.
“Na hilo ndilo moja ya jukumu lingine la bodi kuhakikisha ustawi wa waandishi wa habari katika vyombo vya habari wanavyofanyia kazi unazingatiwa na suala la afya ni la msingi sana kwani bila kuwa na afya njema huwezi kufanya lolote na kwamba ili uwe na uhakika wa afya njema ni muhimu kuwa na bima ya afya." Amesisitiza Dkt. Mkoko.
0 comments:
Post a Comment