Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala
wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Bw. Moses Mabamba, ametoa ufafanuzi kwa
Umma kuhusu hali ya utoaji wa huduma za vivuko katika eneo la Kigamboni,
akibainisha hatua madhubuti zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha wanafunzi
wanaorejea shuleni kesho wanavushwa kwa kipaumbele maalum.
Akizungumza leo tarehe 12
Januari 2026 katika eneo la Kivukoni, jijini Dar es Salaam, Bw. Mabamba alisema
kuwa kwa sasa kivuko cha MV. KAZI kipo kwenye ukarabati mdogo ambapo tayari
injini mbili mpya zimefungwa pamoja na mifumo mipya ya umeme na mifumo mingine
ya uendeshaji. Alibainisha kuwa matengenezo hayo yako katika hatua za mwisho na
kivuko kinatarajiwa kuanza kutoa huduma kesho mara baada ya majaribio ya awali
kukamilika.
Aidha, Bw. Mabamba alieleza
kuwa huduma za uvushaji zinaendelea kutolewa kupitia ushirikiano na wadau wa
sekta binafsi – Azam Sea Taxi, ambapo wamekubaliana kuwapa wanafunzi kipaumbele
katika huduma hiyo ili kuhakikisha wanawahi shule kwa wakati na kwa usalama.
“Matarajio yetu ni kwamba
Serikali imefanya maandalizi makubwa kuhakikisha wanafunzi wanarejea shuleni
bila changamoto. Tumewasiliana na wenzetu wa Azam Sea Taxi na wamekubali
kushirikiana nasi kuwavusha wanafunzi kwa kipaumbele wakati tukikamilisha
majaribio ya MV. KAZI,” alisema Bw. Mabamba.
Aliongeza kuwa ukarabati wa
MV. MAGOGONI unaoendelea mjini Mombasa, Kenya, umefikia zaidi ya asilimia 81.3
na kivuko hicho kinatarajiwa kurejea nchini mwezi Aprili 2026. Wakati huo huo,
MV. KIGAMBONI kinatarajiwa kumaliza ukarabati mwezi Oktoba 2026. Mara baada ya
kurejea kwa vivuko hivyo, TEMESA italipeleka MV. KAZI kwenye ukarabati mkubwa.
Alisisitiza kuwa Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imejipanga
kuhakikisha huduma kwa wananchi, hususan wanafunzi, hazikwami na zinaendelea
kama kawaida pia amewaomba radhi wananchi kwa usumbufu wowote unaoweza
kujitokeza katika kipindi hiki kifupi cha mpito na kuekeza kuwa Serikali,
kupitia TEMESA, inafanya kila jitihada kuhakikisha huduma za vivuko
zinaimarishwa kwa ufanisi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)





0 comments:
Post a Comment