TUME ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini, imekutana na wadau wa madini ikiwemo Wathaminishaji wa Madini, Wachimbaji Wadogo na Wanunuzi ili kupanga bei elekezi ya madini ya vito.
Akizungumza jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki amesema lengo la kukutana na wadau hao ni kufanya tathmini na kupanga bei mpya ya madini ya vito ambayo itatumika katika kipindi cha miezi mitatu na kuhakikisha biashara ya Vito inakwenda vizuri.
“FEMATA ni mzalishaji wa madini, CHAMMATA na TAMIDA ni wanunuzi wa madini ya vito, tumekutana ili kutengeneza bei elekezi, ambayo itatumika kwa kipindi cha miezi mitatu, ili pande zote ziweze kunufaika....; “Kikao kimeenda vizuri, bei zilizowekwa ni rafiki, zitanufaisha pande zote kwa maana ya wachimbaji, wanunuzi na serikali itapata stahiki zake ikiwemo Mrabaha na Ada ya Ukaguzi,”amesema Kasiki na kuongeza
“Bei zilizopendekezwa ni za wazi na zitapatikana kwenye mitandao na Tovuti ya Tume ya Madini, hivyo nawasihi wadau kupitia tovuti ya Tume ya Madini na ofisi za Afisa madini wakazi ili kujua bei elekezi,”amesisitiza
Aidha, Kasiki amesema pia wamebaini changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo wathaminishaji madini na kwamba watakuwa wanakutana nao kila robo ya mwaka lengo likiwa ni kutafuta suluhu ya changamoto hizo na kubadilishana uzoefu kutokana na mabadiliko ya teknolojia duniani katika tasnia ya uthaminishaji madini ili waende na wakati.
Naye mwakilishi kutoka Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA) Kalebi Gunda akizungumza kuhusiana na bei elekezi amesema ni rafiki kwa wachimbaji.
“Kikao kimeenda vizuri hakuna atakayelalamika na kila mmoja atapata manufaa kwa upande wake, wachimbaji watanufaika, wanunuzi watanufaika na serikali nayo itapata stahiki yake ya mapaato kupitia Mrabaha na halmashauri itapata tozo yake ya ‘service levy’,”amesema Gunda
Vyama vilivyoshiriki kikao hicho ni Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake (TAWOMA), Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMMATA)
0 comments:
Post a Comment