Nafasi Ya Matangazo

March 04, 2025





Umoja wa madereva wa bodaboda wa Mbeya Mjini umemtaka Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, kurejea kugombea tena Ubunge wa Jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ili aendelee na kazi waliyomtuma ya kuwasogezea maendeleo ya haraka katika Jiji hilo. Katika kuthibitisha dhamira yao, wamechangia shilingi milioni moja kama mchango wa kuchukua fomu ya kugombea.

Kauli hiyo imetolewa leo, tarehe 4 Machi 2025, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ofisi za makao makuu ya Umoja huo katika Kata ya Ilolo. Mwenyekiti wa bodaboda, Ndg. Aliko Fwanda ambaye pia ni kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesema kuwa hawako tayari kumpoteza Dkt. Tulia, kwani ameonesha utendaji mzuri na wanahitaji amalizie kazi aliyoianza.

Kwa upande wake, Dkt. Tulia amewashukuru madereva wa bodaboda kwa imani waliyoonesha kwake na ameahidi kuendelea kuwatumikia kwa bidii ili kuhakikisha anatekeleza mahitaji ya wananchi wa Mbeya Mjini.

Aidha, amewaomba bodaboda na wakazi wote wa Mbeya kuendelea kumuombea afya njema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kujitokeza kwa wingi kumpigia kura mwezi Oktoba 2025 ili aweze kufanikisha yote wanayotamani kupata na kuendeleza juhudi za maendeleo nchini.

“Niwashukuru sana kwa mshikamano wenu. Ingawa kila mmoja wetu hapa ana chama chake cha siasa, tumethibitisha kuwa maendeleo hayana itikadi. Tuendelee kuwa wamoja kwa ajili ya ustawi wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla,” amesisitiza Dkt. Tulia.
Posted by MROKI On Tuesday, March 04, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo