Nafasi Ya Matangazo

March 04, 2025



Na Mwandishi Wetu
TUME ya Madini imefanikiwa kukusanya Shilingi 690, 763, 401,639.06  ndani ya miezi nane  sawa na asilimia 69.08 ya lengo la mwaka wa fedha 2024/2025.

Akielezea mafanikio ya Tume ya Madini kwa kipindi cha miaka minne leo Machi 4, 2025 Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na rasilimali umepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 kwa mwaka wa fedha 2023/2024. 

Amesema makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu. 

“Aidha katika kipindi cha kuanzia Julai, 2024 hadi Februari, 2025, Tume imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 690, 763, 401,639.06 sawa na aslimia 69.08 ya lengo la Mwaka wa Fedha 2024/2025,”amesema Mhandisi Lwamo.

Amesema, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.0 Mwaka 2023. 

“Hii ni kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za madini, ukuaji wa sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023,”amesema.

Amesema, ili kuendelea kuimarika kwa sekta ya madini, mwenendo wa mchango wa sekta ya madini na ukuaji wake unatarajiwa kufikia asilimia 10 mwaka huu wa 2025 kama ilivyoelezwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Amesema,  Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini imeendelea kusimamia utendaji kazi wa Masoko ya Madini na vituo vya ununuzi wa Madini nchini, hadi kufikia mwezi Februari, 2025 Tume ya Madini kwa kushirikiana na TAMISEMI imefanikiwa kuanzisha masoko 43 na vituo vya ununuzi wa madini 109.

Aidha, amesema jumla ya Mipango 1,076 ya ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini imepokelewa na kufanyiwa uchambuzi.

“ Kati ya mipango iliyowasilishwa, 1,047 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na mipango 29 haikukidhi vigezo hivyo ilirejeshwa kwa wahusika kwa ajili ya marekebisho;”amesema Lwamo.

Amesema,  Tume ya Madini imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania kutoka kwenye Kampuni mbalimbali za uchimbaji ambapo Kampuni zimeweza kuzalisha ajira   19,874 ambapo kati ya hizo 19,371 ni Watanzania   sawa na asilimia 97.5 na 503 ni wageni sawa na asilimia 2.5 ya ajira zote zilizozalishwa. 


“Vilevile, jumla ya bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,780,161,183.28 ziliuzwa na kusambazwa migodini ambapo kati ya bidhaa hizo Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,465,592,451.28 sawa na asilimia 91.68 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini,”amesema.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Lwamo amesema Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambapo imefanikiwa kutenga maeneo 58 katika mikoa mbalimbali.

Posted by MROKI On Tuesday, March 04, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo